RAIS MSTAAFU MH ALI HASSAN MWINYI
RAIS mstaafu wa awamu ya pili, Ally Hassan Mwinyi, ameibiwa sh
milioni 37.4 na hivyo kulazimika kupanda kizimbani katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, kutoa ushahidi wake.
Kwa hatua hiyo, Mzee Mwinyi anafuata nyayo za Rais wa Awamu ya Tatu,
Benjamin Mkapa, aliyepanda kizimbani hivi karibuni kutoa ushahidi katika
kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Balozi wa
Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na Grace Martin.
Mzee Mwinyi ambaye alipanda kizimbani jana, anadai kuibiwa sh
37,440,000 na Abdallah Nassoro Mzombe (39) ambaye ni wakala wake.
Mbele ya Hakimu Mkazi, Genivitus Dudu, mshtakiwa huyo, mkazi wa
Kinondoni Mkwajuni, anashtakiwa kwa makosa ya kumuibia Mzee Mwinyi kiasi
hicho cha kodi ya pango ya nyumba mbili zinazomilikiwa na Rais huyo
mstaafu.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka ambayo Tanzania Daima Jumatano ina
nakala yake, Mzombe anadaiwa kufanya makosa hayo kinyume na kifungu cha
258 na 273 (b) (e) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya Sura ya 16 ya mwaka
2002.
Siku hiyo ya Agosti 21, mwaka huu, ilidaiwa kuwa kati ya Januari Mosi,
mwaka 2011 na Julai 2012 huko Mikocheni, Mzombe akiwa wakala wa Rais
huyo mstaafu, alimwibia sh 17,640,000 ambazo ni pato la kodi ya nyumba
yake iliyoko eneo la Mikocheni, wilaya ya Kinondoni.
Iliendelea kudai kuwa kiasi hicho cha fedha ambacho Mzombe alimwibia
Rais Mwinyi kilikuwa ni kodi ya pango la nyumba namba 481, iliyoko
kwenye ploti A huko Mikocheni ya mwaka 2011/2012 na 2012/2013.
Aidha anadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, mwaka 2011 na Julai 10,
mwaka huu huko Msasani Village wilaya ya Kinondoni, mshtakiwa huyo
alimwibia tena Rais huyo mstaafu sh 19,800,000 ambazo zilikuwa ni kodi
ya nyumba namba 55 iliyoko kwenye Kitalu C .
Kiasi hicho cha fedha kilikuwa ni kodi ya pango la nyumba hiyo la mwaka 2011/2012 na 2012/2013.
Hata hivyo mshtakiwa huyo alikana mashtaka yote na yuko rumande hadi Oktoba 22 kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kusikilizwa.
Rais Mwinyi jana alitua katika mahakama hiyo huku akiongozwa na
maofisa Usalama wa Taifa (TISS) kuja kutoa ushahidi katika kesi hiyo ya
jinai Na. 201/2012 iliyofunguliwa na serikali dhidi ya wakala wa Mwinyi,
Abdallah Nassoro Mzombe (39).
Kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa, Mwinyi alihifadhiwa kwa muda
kwenye chumba namba moja cha mahakama hiyo ili kutoa muda kwa wakili wa
serikali, Charles Anindo, kumuandaa.
Waandishi wa habari waliokuwepo mahakamani hapo kwa ajili ya kuripoti
kesi hiyo, walizuiliwa kuingia, jambo ambalo lililalamikiwa vikali na
wana habari hao.
“Msiingie humu ndani haiwahusu,” alisema ofisa habari mmoja, akiwazuia waandishi kuingia ndani ya mahakama hiyo.
Mzee Mwinyi aliondoka katika viwanja vya mahakama hiyo majira ya saa
6:21 mchana na kisha kupanda gari aina ya Land Cruiser lenye namba za
usajili T 914 BJT.
Hati ya mashtaka ya kesi hiyo ilifunguliwa mahakamani hapo Agosti 21 mwaka huu.
Mei 7 mwaka huu Rais Mkapa alifika mbele ya Hakimu Mfawidhi wa
Mahakama ya Kisutu, Elvin Mugeta, kutoa ushahidi katika kesi ya uhujumu
uchumi iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia,
Profesa Costa Mahalu, na Grace Martin. Mahalu aliachiwa huru katika kesi
hiyo.
No comments:
Post a Comment