Vifaa
vya Ofisini mali kampuni ya Scandinavia Express vikiwa vimetolewa nje
jijini Dar es Salaam jana. Vilitolewa na madalali wa mahakama kwa madai
ya kushindwa kulipa mkopo ambao hata hivyo haikufahamika ni kiasi gani.
Picha na Fidelis Felix
“Hii ni operesheni endelevu, kwa hiyo, wadaiwa wengine sugu wajiandae.
Kama walijua kuwa Serikali hii haiwezi kuwachukulia hatua zozote, basi
tutawaondoa wote bila kujali hadhi wala wadhifa wa mpangaji,”
alitahadharisha Tarimo.
Kampuni ya Usafirishaji ya Scandnavia imetimuliwa katika majengo
ilimokuwa imepanga kwa matumizi ya shughuli zake za kiofisi, kutokana na
kushindwa kulipa kodi ya pango zaidi ya Sh200 milioni.
Kampuni hiyo iliyokuwa imepanga katika majengo yanayomilikiwa na Wakala
wa Majengo Tanzania (TBA) yaliyoko Kariakoo eneo la Kamata, jijini Dar
es Salaam, ilitimuliwa na TBA, katika operesheni inayoendeshwa na TBA
dhidi ya wapangaji wake ambaoni wadaiwa sugu.
Mbali na Scandnavia, kampuni nyingine tatu ambazo ni jirani yake,
zilizokuwa zimepanga katika majengo hayo ya TBA yaliyopo Kamata, pia
zilitimuliwa kutokana na kushindwa kulipa kodi ya pango kwa muda mrefu.
Kampuni hizo zilizotimuliwa katika operesheni hiyo iliyoendeshwa chini
ya ulinzi mkali wa askari Polisi wenye silaha, ni pamoja na Shems &
Sons, Desktop Computers (kwa sasa Panorama Communications Institute) na
Sky Net.
Mwananchi lilifika eneo la ofisi hizo zote mchana na kushuhudia samani
na vifaa mbalimbali vya ofisi hizo vikiwa vimetapakaa nje, huku maofisa
wa TBA wakiweka makufuli katika milango ya vyumba vilivyokuwa vinatumiwa
kama ofisi za kampuni hizo.
Maofisa wa kampuni hizo walikuwapo eneo la tukio wakati hawakuwa tayari
kuzungumza lolote, wakidai kuwa wao si wasemaji na kwamba wasemaji
hawakuwepo na hawakujua walikokuwa wamekwenda.
Ofisa mmoja wa Kampuni ya Scandnavia ambaye hata hivyo hakutaka
kujitambulisha alisema anayeweza kuzungumzia operesheni hiyo ni
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Mohamed Abood lakini akasema hayupo
na wala hajui mahali alikokwenda.
Katika ofisi za Chuo cha Mawasiliano cha Panorama (Desktop) maofisa
waliokuwapo waligoma kuzungumza lolote na kurushiana mpira huku wakidai
kuwa mzungumzaji ambaye ni mmiliki wa chuo hicho alikuwa ametoka muda
mfupi baada ya operesheni.
Ofisa Miliki wa TBA Erasmi Tarimo aliliambia Mwananchi kuwa Scandnavia
inadaiwa kiasi cha Sh220 milioni, ambazo ni malimbikizo ya kodi ya pango
ya miaka takribani minane.
Alisema kuwa kampuni hiyo inatakiwa kulipa kodi ya Sh3 milioni tu kwa
mwezi, lakini imekuwa ikilimbikiza deni hilo hadi limefikia kiasi hicho.
Tarimo aliongeza kuwa kampuni hiyo pamoja na nyingine ambazo zilitupiwa
virago jana licha ya kuandikiwa barua mara kadhaa kuzikumbushia kulipa
deni lake lakini zimeshindwa kufanya hivyo.
“Tumeshawaandikia barua nyingi sana kuwakumbushia, wengine wamekuwa
wakilipa kidogo kisha wanaendelea kulimbikiza na wengine hawajalipa
kabisa. Katika hali kama hii inabidi hatua kama hizo zichukuliwe, na
hata Sheria za Kodi zinaturuhusu kuwaondoa wasiolipa,” alisema Tarimo.
Akizungumzia operesheni hiyo, Tarimo alisema kuwa kwa jana ilifanyika
katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, kama vile Ilala,
Mikocheni, Mbezi, Kurasini na kwingineko ambako kuna wadaiwa wake sugu.
“Hii ni operesheni endelevu, kwa hiyo, wadaiwa wengine sugu wajiandae.
Kama walijua kuwa Serikali hii haiwezi kuwachukulia hatua zozote, basi
tutawaondoa wote bila kujali hadhi wala wadhifa wa mpangaji,”
alitahadharisha Tarimo.
Hata hivyo alisema kuwa operesheni hiyo jana iliendeshwa vizuri bila
vipingamizi, kwa kuwa walipata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa Jeshi
la Polisi waliohakikisha usalama, Serikali za Mitaa na hata kwa
wapangaji wenyewe.
Chanzo: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment