Pages


Photobucket

Thursday, October 25, 2012

BALOZI IDDI ASEMA SEREKALI HAITOMVUMILIA YOYOTE ATAKAYEBAINIKA KUHUSIKA NA UVUNJIFU WA AMANI

 

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitamuonea haya wala kumuogopa mtu ye yote ambae atabainika kuhusika na uvunjifu wa amani baada ya Serikali kuvumilia vya kutosha, uvumilivu ambao umefikia kikomo.

Kauli hiyo imetolea na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akiufunga mkutano wa Tisa wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar uliokuwa ukifanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Seif alisema Serikali kupitia vyombo vya ulinzi itaendelea kuvisaka vikundi vya kihuni vinavyoendesha vitendo vya kuwatisha Wananchi na kuwanyang’anya vitu na mali zao, kuchoma moto baadhi ya Majengo sambamba na kuharibu miundo mbinu ya Bara bara.

Alisema hali hiyo ya vurugu sio Utamaduni wa Wananchi wa Visiwa hivyi ambayo ni ya kusikitisha iliyopelekea wananchi kuacha shughuli zao za kujitafutia riziki kutokana na kusimama kwa harakati zao za maendeleo

“ Tutafanya kosa kubwa sana ikiwa tutaanza kuichezea amani tuliyonayo kwani kuvunjika kwa amani Nchini mwetu ndio chanzo cha kuvunjika kwa Umoja wetu.” Alisisitiza Balozi Seif.

Aliwanasihi Wananchi kuacha kujiingiza katika vitendo vya uvunjifu wa amani kwani kutenda hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria na Serikali haitasita kumchukulia hatua mtu ye yote atakayejihusisha na vitendo hivyo.

Aidha Balozi Seif aliwaomba Wananchi kutoa Taarifa kwa vyombo vya dola mara tu watakapoona dalili za watu wenye nia ya kutaka kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani.

Akizungumzia suala la Rushwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali inaendelea kuchukuwa hatua za kuimarisha Taasisi za kupambana na Rushwa.

Alisema Viongozi pamoja na Wananchi wana wajibu wa kutoa ushirikiano kwa Taasisi ya kupambana na Rushwa iliyopitishwa na Baraza hilo hivi karibuni ili iweze kutekeleza majukumu na wajibu wake kwa mujibu wa sheria na kwa kwa faida ya maendeleo ya Taifa.

“ Kama sote tunavyojua rushwa ni adui wa haki na hivyo haina budi kupigwa vitailiitokomezwe kabisa. Lakini hizi hazitafanikiwa bila ya ushirikiano wa wananchi wenyewe”. Alifafanua Balozi Seif.

Kuhusu kundi la watu wenye Ulemavu Balozi Seif alisema Serikali imeweka mikakati katika kujenga usawa na kuheshimu haki za watu wote wenye ulemavu.

Alieleza kwamba kuwapatia watu wenye nulemavu haki zao za msingi ni jambo la Kikatiba na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha azma hii inafikia malengo yaliyowekwa.

Balozi Seif aliipongeza Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais waZanzibarkwa juhudi kubwa inayochukuwa katika kuimarisha mazingira kwa watu wenye ulemavu na kuwajengea uwezo wa kushiriki katika maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi.

Akigusia suala la tume ya kukusanya na kuratibu Maoni ya Mabadiliko ya Katiba ya Muungano Balozi Seif aliwaomba Wananchi ambao bado hawajatoa maoni yao kuitumia fursa hiyo itakayoamua mambo muhimu yatakayokuwa na maslahi kwa Jamii yetu.

Alisema si vyema kwa baadhi ya vikundi vya Wananchi kuiacha fursa hii na kuendelea kutoa matamshi yanayochochea nchuki, uhasama na vurugu kwa kisingizio cha kuukataa Muungano.

ASlisisitiza kwamba jambo la kubwa la kuzingatia ni kuitumia fursa hii ili Wananchi wote waweze kuitoa maoni yao kwa uhuru bila ya kubughudhiwa na kutishiwa maisha yao.

Kuhusu Sekta ya Umeme Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema suala la mgao wa umeme karibu litakuwa historia katika Kisiwa cha Unguja kufuatia kutandikwa kwa waya mpya wa umeme wenye uwezo wa kuchukuwa umeme wa Mega Watts 100 kazi ambayo inatarajiwa kukamilika mwezi Disema mwaka huu wa 2012.

Alisema hatua hii ni faraja kubwa kwa Wananchi waZanzibarhasa ikizingatiwa kwamba umeme ndio nishati muhimu kwa shughuli za uzalishaji na maendeleo ya Taifa hili.

Aliwataka Wananchi wote waendelee kuitumia nishati ya umeme kwa shughuli zao za kujiajiri kwa nia ya kujikomboa kutoka kwenye umaskini.

Baraza la Wawakilishi Zanzibar limeahirishwa hadi jumatano ya Tarehe 16 Januari mwaka 2013 saa 3.00 za Asubuhi.

Chanzo: Mzalendo.net

No comments:

Post a Comment