Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM, Martine Shigela akizungumza
na waandishi wa habari leo mjini Dodoma kuhusu maandalizi ya Mkutano
Mkuu wa UVCCM. Kulia ni Cosmas Hinju, Mwenyekiti wa Kamati ya habari na
mapambo wa maandalizi ya Mkutano huo.Picha na Bashir Nkromo-Dodoma
WAKATI Uchaguzi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) umemalizika juzi,
huku ukidaiwa kugubikwa na ubabe na rushwa, Umoja wa Vijana wa CCM
(UVCCM) umejitapa kwamba, utahakikisha vitendo hivyo havitokei katika
uchaguzi wake mkuu utakaofanyika kuanzia kesho mjini Dodoma.
UVCCM imeapa kwamba mgombea au hata mpambe atakayebainika kujihusisha na
kampeni zilizo nje ya utaratibu na kanuni za UVCCM au kujihusisha na
vitendo vya rushwa atashughulikiwa mara moja ikiwemo kuchukuliwa hatua
za kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Katibu Mkuu wa Umoja wa
Vijana wa CCM,Martine Shigela alisema, wameweka mtandao mpana wa kutosha
kukabiliana na aina yoyote ya ukiukwaji wa tararibu, kanuni na sheria
za uchaguzi wa UVCCM.
"Sisi hatuwezi kuzungumzia hayo mnayosema, yamejitokeza kwenye uchaguzi
wa UWT,lakini kwa upande wetu tunawahakikishieni kwamba tutamkabili
vilivyo tena bila mzaha,mgombea au mpambe yeyote atakayejaribu kutumia
mbinu chafu za kampeni ikiwemo kutoa rushwa", alisema Shigela.
Shigela alisema, taratibu za mkutano mkuu utakaoambatana na uchaguzi
huo, zimekamilika na utafanyika kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere, uliopo
Chuo Cha Mipango ambako ndiko ulikofanyika pia ule wa UWT.
Alisema, mkutano unaanza kesho, Oktoba 23, na utafunguliwa na Mwenyekiti
wa CCM, Rais Jakaya Kikwete."Hadi sasa maandalizi yamekamilika, leo
Oktoba 22, tunakazi kupokea wageni mbalimbali kutoka maeneo kadhaa
wakiwemo wa kutoka nchi za nje amabao watahudhuria mkutano wetu. alisema
Shigela.
Katika nafasi ya Mwenyekiti wanachuana wagombea watatu, Lulu Mushamu
Abdallah, Sadifu Juma Khamis na Rashid Simai Msaraka wakati katika
nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni Ally Salum Hapi, Paul Christian Makonda
Mboni Mohamed Mhita.
Nafasi zingine ni, Halmashauri Kuu ya Taifa Viti sita (Bara) wagombea
40, Viti Vinne (Zanzibar) wagombea 22, Nafasi ya Baraza Kuu la Vijana
Taifa Viti vitano Bara wagombea 39 na viti vitano Zanzibar wagombea 14,
Uwakilishi Wazazi Taifa na Jumuia ya Wanawake Tanzania (UWT) wagombea
16 kila nafasi.
No comments:
Post a Comment