Pages


Photobucket

Saturday, October 20, 2012

SAKATA LA DKT. ULIMBOKA,IKULU YASEMA “HAYA MADAI NI UPUUZI”

      Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Stephen Ulimboka, akisaini tamko lake kwa watanzania ambalo lilisomwa kwa niaba yake na Wakili wake, Nyaronyo Kicheere, Dar es Salaam. Kulia ni Wakili na Kamishna wa Viapo, Rugemeleza Nshala. Tamko hilo alisaini Oktoba 07, jijini Dar es Salaam.

Siku chache baada ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Nchini, Dkt. Stephen Ulimboka, kusisitiza kwamba alitekwa na mtu anayefanya kazi Ikulu, Ramadhan Ighondu, Ikulu imehamanika na kujitetea kwamba madai hayo ni ya kipuuzi.

 *Tafadhali bofya hapa kurejea kuisoma nakala ya taarifa kamili aliyoitoa Dkt. Ulimboka.

Juzi Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, alisisitiza: “Ikulu iliishajibu. Tulisema haihusiki, na Rais Jakaya Kikwete amepata kuzungumza juu ya jambo hili mara nyingi.”

Rweyemamu, bila ya kufafanua zaidi alisema, “Naomba uninukuu; haya madai ni upuuzi… hiki kitu kilishajibiwa.”

Alipoulizwa kama anamfahamu Ramadhan Ighondu, Rweyemamu akisisitiza kuwa Ikulu haihusiki naye.

Mwandishi akamwuliza Rweyemamu ni hatua gani ambazo Ikulu itamchukulia Ighondu kama mfanyakazi wao.

Swali hilo lilionekana kumkera Rweyemamu aliyejibu kwa ukali, “Kama Ikulu haihusiki, hatuna cha kufanya juu ya jambo hilo; mnakaa mnalea maneno ya kipuuzi… Ikulu imwajibishe kuhusu nini? Haihusiki!”

Alipobanwa zaidi alisema kama kuna watu wanasema hivyo waende wakaripoti polisi.

Kauli ya juzi ya Rweyemamu ni ya pili kutolewa na Ikulu kuhusu Dkt. Ulimboka. Mara ya kwanza, ilipotolewa na Rais Jakaya Kikwete alipokutana na baadhi ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, akasema, “Dk. Ulimboka ana nini mpaka Ikulu imteke? Tumteke ili iweje?”

Rais Kikwete alikwenda mbali zaidi na kusema hata Dk. Ulimboka mwenyewe alipokwenda Ikulu akiwa na viongozi wenzake alinyamaza kimya tu na kwamba waliokuwa wakizungumza ni wengine.

Hata hivyo, kwa kuwa Ikulu imesema haihusiki, na Dk. Ulimboka mwenyewe ametamka kwamba anamjua aliyemtesa, na kwamba anafanya kazi Ikulu, ni juu ya umma kuamua nani anasema ukweli.

Wakati Ikulu ikisema hayo, Jeshi la Polisi ambalo lilimtia mbaroni raia wa Kenya na kumpeleka mahakamani kujibu tuhuma za kumteka na kumtesa daktari huyo, nalo limesita kubainisha kama litamkamata na kumhoji Ighondu, ambaye ametajwa rasmi na shahidi wa kwanza halisi katika suala hili, Dkt. Ulimboka.

Maofisa wa jeshi hilo wametupiana mpira kila mmoja akidai hahusiki na suala hilo.

Kwa upande wa polisi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alijitetea akisema suala hilo liko kwa mkubwa wake wa kazi, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Maanumba, na kwamba atafutwe kwa ajili ya kulitolea ufafanuzi, “Gazeti lenu( jumanne-Tanzania Daima) nililisifia sana nikalitolea mfano mzuri; watu hawawezi kutuchezea tu na kutishia mamlaka iliyopo kama hakuna sheria. Lazima kila mmoja afuate sheria. Hilo suala liko kwa DCI na sisi polisi tuna nidhamu ya kazi. Suala likiwa kwa mkubwa wako huwezi kulizungumzia. Tambua faili lipo kwao na mimi sina uwezo wa kulizungumzia,” alisema.

Alipobanwa zaidi kuwa Dkt. Ulimboka ameshamtaja aliyemtesa na kwamba yuko tayari kuwapa ushirikiano na kutoa ushahidi mbele ya tume huru, Kova alisema, “Hivi wewe unanitafuta nini? Nimekwambia sina uwezo nalo; au hutaki ushirikiano na mimi? Hilo swali lako ni sawa na kumuuliza kipofu pale unapaonaje!?”

Naye DCI Manumba alipopigiwa simu, alijibu kwa kifupi akisema aulizwe msemaji wa jeshi hilo. Akakata simu.

Msemaji wa jeshi hilo, Advera Senso, alipoulizwa alisema suala hilo liko kwenye uchunguzi, hivyo hawezi kulitolea ufafanuzi. Senso alipobanwa zaidi, alisisitiza, “Tafadhali, sina maelezo zaidi ya hayo. Kukiwa na kitu kipya tutaandaa.”


Source: WAVUTI.COM

No comments:

Post a Comment