Pages


Photobucket

Sunday, October 21, 2012

SOPHIA SIMBA AMLIZA KILANGO UWT,SHY ROSE AZUA TAFRANI

      Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake ya CCM, (UWT), ambaye anamaliza muda wake, Sophia Simba , akiingia ukumbi wa Mipango tayari kwa uchaguzi mkuu wa Jumuiya hiyo mjini Dodoma, Jumamosi Oktoba 20, 2012  Kabla ya kuibuka kidedea  dhidi ya Anna Kilango.

Mbunge wa bunge la Afrika Mashariki, Shy-Rose Bhanji, (Aliyekaa), akitulizwa hasira na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwkezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary Nagu, wakati wa kikao cha uchaguzi mkuu wa Jumuiya ya Wanawake ya CCM, UWT, kwenye ukumbi wa chuo cha Mipango Dodoma Jumamosi Oktoba 20, 2012.
Mwenyekiti wa UWT  Mh.Sophia Simba  na Makamu wake  Mh Asha Bakari Khamis wakifurahia jambo  baada ya kuibuka kidedea.
 Mwenyekiti mpya wa UWT Sophia Simba akipongezwa na mke wa Rais wa Zanzibar mama Mwanamwema Shein baada ya kuibuka mshindi kwenye uchaguzi wa UWT usiku wa kuamkia leo
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Sofia Simba, amefanikiwa kutetea kiti chake baada ya kuibuka mshindi na kumbwaga mpinzani wake, Anne Kilango Malecela.
Uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkali kati ya Mama Sofia Simba na Kilango, ulifanyika jana mjini Dodoma na kutawaliwa na vituko vingi, vikiwamo vijembe, kashfa na kugubikwa na tuhuma za rushwa.
Sofia Simba, ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, aliibuka na ushindi wa kura 716, Kilango kura 310 wakati Mayrose Magige aliambulia kura saba.
Awali kabla ya matokeo hayo, hali ya hewa ndani ya ukumbi ilichafuka baada ya Mbunge wa Afrika Mashariki, Shy-Rose Bhanji na Sophia Simba kutaka kupigana.
Hali hiyo ilisababisha shughuli za mkutano huo kusimama kwa muda huku baadhi ya wapambe wa wagombea hao wakipiga kelele na kutoleana maneno ya kashfa, kejeli na lugha chafu.
Hali hiyo ilisababisha Shy-Rose ashikwe mkono na kuondolewa karibu na alipokuwa Mama Sophia Simba, kwani alipandwa jazba kiasi cha kutaka kuanza kumshushia makonde Waziri Simba.
Timbwili hilo lilianza baada ya Waziri Simba kumaliza kujinadi kwa wajumbe kwa ajili ya kuomba kura.
Mara baada ya kujinadi, mwenyekiti wa mkutano huo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maenedeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, aliruhusu maswali, ndipo Shy-Rose aliibuka na swali chungu kwa Waziri Simba.
Katika swali hilo, Shy-Rose Bhanji alianza na maelezo kwamba hivi sasa wapo katika changamoto ya vyama vingi na kina mama wana uwezo wa kutetea chama, hivyo ni vema wakabadili mfumo wa kuchagua viongozi.
Akiwa bado anaendelea kujenga hoja ya swali lake, Waziri Tibaijuka amkatiza na kumtaka aache kuhutubia bali aulize swali, asimwonee mgombea.
Kwa mwongozo huo, Shy-Rose alijibu kwa kusema hamuonei mgombea huyo bali anauliza swali.
Hali hiyo iliwafanya baadhi ya wajumbe, wapambe wa Simba kuanza kurusha vijembe kwamba ‘ametumwa huyo’.
Aidha, Tibaijuka alimruhusu tena Shy-Rose kuulizwa swali, ndipo akauliza hivi: “Simba utakivusha chama vipi maana hujawahi kusimama jukwaani kuihamasiha UWT na kukitetea chama.”
Akijibu swali hilo, Waziri Simba alianza kwa kusema: “Muuliza swali hajui siasa za chini, na yeye amekuwa akifanya mikutano katika wilaya mbalimbali katika kuihamasisha jumuiya hiyo na hali hiyo imesaidia CCM kupata ushindi wa kishindo mwaka 2010.
“Mimi kama waziri siwezi kusimama jukwaani au bungeni na kuanza kubwatuka kiasi cha kukibomoa chama changu au kukikosoa, bali mimi nimekuwa nikiwafuata kina mama wa UWT maeneo walipo na kukihamasisha chama na jumuiya yangu,” alisema Simba.
Jibu hilo liliwafanya wapambe wa Sofia kuinuka vitini na kushangilia kwa vigelegele huku wakiita, ‘Simba,… Simba… Simba’ mithili ya mashabiki wa timu ya soka ya Simba wanapoishangilia timu yao inapofunga goli.
Baada ya kushuka kujibu swali hilo, Waziri Simba alimfuata Shy-Rose mahala alipoketi na kuanza kurushiana vijembe na kama si baadhi ya wajumbe kuingilia kati, wawili hao wangetwangana makonde.
Awali akifungua mkutano huo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Mohamed Gharib Bilal, aliwaasa wajumbe wa jumuiya hiyo kuchagua viongozi watakaosaidia ushindi wa CCM mwaka 2015.

Chanzo: Tanzania daima

No comments:

Post a Comment