Pages


Photobucket

Monday, October 1, 2012

KASI YA VIJANA WANAOSHIRIKI KWENYE MAANDAMANO YA KUDAI MAISHA BORA NCHINI, IMEMTISHA RAIS MSTAAFU WA AWAMU YA PILI, ALHAJI ALI HASSAN MWINYI

                    Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi

KASI ya vijana wanaoshiriki kwenye maandamano ya kudai maisha bora nchini, imemtisha Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, na hivyo kushauri utafutwe ufumbuzi wa haraka wa kupunguza idadi ya vijana wasio na kazi wanaohama vijijini na kukimbilia mijini.
Mzee Mwinyi alisema kuwa tatizo la ajira kwa vijana hao lipo katika nchi nyingi duniani, na kwamba kuandamana si suluhisho wala dawa ya kulimaliza, hivyo aliwataka vijana kujitengenezea ajira zao wenyewe.
Alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana, katika mkutano wa kuhamasisha vijana wa Kata ya Kwadelo wilayani Kondoa Mkoa wa Dodoma, wanaoishi Dar es Salaam, akiwataka warudi kwenye kata yao ili kushiriki kilimo na kujikwamua na hali ngumu ya maisha.
Vijana hao waliambatana na Diwani wa Kata hiyo, Alhaji Omar Kariati, ambaye Rais Mwinyi alimmwagia sifa kutokana na juhudi mbalimbali anazozifanya katika kuhakikisha wanapata mahitaji, na hasa katika kuhamasisha shughuli za kilimo mkoani Singida.
Mwinyi alitolea mfano nchi ambazo zimeingia katika maandamano na migomo kuwa ni Hispania na Ureno ambapo wananchi wake wanadai serikali yao kuwaboreshea maisha bora ilhali wangejiajiri wenyewe yasingetokea maandamano makubwa kama hayo.
Alisema kuwa kila nchi inakabiliwa na tatizo la ajira kwa vijana na kwamba halikwepeki, hivyo aliwataka viongozi katika maeneo husika kuhakikisha vijana wanajituma katika kujitafutia na kutengeneza ajira zao wenyewe bila kuitegemea serikali kwa kiasi kikubwa.
“Sasa hivi katika nchi mbalimbali kumekuwa na maandamano ya vijana, wakiwa wanahitaji ajira na maisha mazuri, hivyo kufanya maandamano haisaidii, kinachotakiwa kila mtu, kila kiongozi ana wajibu wa kutengeneza ajira yeye mwenyewe,” alisema Alhaji Mwinyi.
Japo hakutaja moja kwa moja, Mzee Mwinyi alionekana kuguswa na idadi ya vijana wanaojitokeza kwenye maandamano kama hayo yanayoendeshwa hapa nchini na vyama vya upinzani na hivyo kuashiria kuwa tatizo la ukosefu wa ajira ni kubwa.
Rais huyo mstaafu maarufu kama Mzee Ruksa, aliongeza kuwa vijana wanatakiwa wasikimbilie mijini bali wabaki vijijini walime sana na kwamba waache kulalamika huku akiwataka pia kuweka mbele maombi kwa Mungu.
Kuhusu hali ya mfumuko wa bei nchini, alisema kwa sasa nchi nyingi zimekuwa katika hali ngumu ya maisha kutokana na kupanda kwa bei za vyakula, nauli na mafuta, hivyo aliwaasa vijana kuelekeza nguvu zaidi katika kilimo.
Naye Kariati aliwataka vijana wa kata yake waishio mijini kuacha kulalamika na kukaa vijiweni badala yake warudi kijijini kwa ajili ya kilimo baada ya serikali kuwawekea fursa za kilimo chenye tija kwa kuwakopesha ekari tano za kilimo kila mmoja.
Akitolea ufafanuzi, alisema kuwa akari hizo tano kwa makadirio, mkulima atavuna magunia 100 yakiwa na thamani ya sh milioni tano ambapo marejesho yake ni gunia tano na sh 150,000 jambo ambalo ameliita ni uwezeshwaji mkubwa uliofanywa na serikali.
Katika mkutano huo, Mzee Mwinyi alikabidhi kitanda cha kujifungulia akina mama na tenki la maji lenye ujazo wa lita 5,000 kwa wakazi wa Kijiji cha Kerere Chang’ombe na Kwadelo.
Pia mwanafunzi wa Chuo cha Ualimu Ununio, Kassimu Athumani, alikabidhiwa sh 200,000 ili zimsaidie katika masuala mbalimbali ya elimu.

No comments:

Post a Comment