KUNDI kubwa la Waislamu wenye imani kali, jana lilizusha vurugu kubwa
zilizoambatana na kuchomwa moto na kuharibiwa kwa makanisa manne ya Kikristo
jijini Dar es Salaam, katika kile kilichoelezwa kuchukizwa na kitendo cha
kijana mmoja wa Kikristo aliyedaiwa kukimwagia haja ndogo kitabu kitakatifu cha
Kurani.
Waislamu hao waliokuwa na jazba kubwa, walichukua hatua ya kufanya uharibifu
huo, baada ya kushindwa kwa jaribio la kukiteka kituo kidogo cha polisi cha
Mbagala wilayani Temeke kwa nia ya kumchukua kijana anayetuhumiwa kufanya tukio
hilo, Emmanuel Josephat (14) ili wamuue kwa kumchinja hadharani kama adhabu kwa
kosa hilo.
Vikosi vya polisi wenye silaha na mabomu ya machozi na maji ya kuwasha
walipambana na Waislamu hao ambao walizidi kuongeza kila dakika, hivyo kufunga
shughuli zote za kijamii katika barabara ya Kilwa, eneo lote la Mbagala.
Wakiwa na silaha za mawe, kundi hilo lilivamia mitaani na kuchoma Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Mbagala Zakhem, na lile la Assembly of
God (TAG), huku wengine wakiharibu Kanisa la Anglican, kuvunja vioo katika
kanisa la Wasabato, na kuchukua vifaa vya muziki na ibada na kuviunguza
hadharani.
Waislamu hao waliyaponda mawe na kuyaharibu magari ya polisi namba T 142
AVV, PT 0966 na T 325 BQP, basi la Kampuni ya Usafirishaji Dar es Salaam (UDA)
na gari la waandishi wa habari kutoka Clouds.
Jitihada za Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Polisi wa Temeke, David Misime,
kujaribu kuzuia kuenea kwa ghasia hizo kwa kuwatumia viongozi wa Kiislamu,
zilionekana kugonga mwamba kutokana na viongozi hao kuwatetea waumini wao.
Viongozi wa dini hiyo wakiwemo Sheikh wa Wilaya ya Temeke, Mohamed Kingo,
Katibu wa Vijana Bakwata, Abdulkarim Michael Fulano na Sheikh wa Taasisi na
Jumuiya za Waislamu, Faridi Salehe Ahmed kukaa kikao na Kamanda Misime,
walifikia muafaka wa kuwatuliza Waislamu hao, lakini hali iliendelea kuwa
mbaya.
Chanzo cha vurugu hizo ni ubishani wa kitoto uliozuka baina ya mtoto
Emmanuel na mwenzake Zakaria Hamis (12) anayesoma Shule ya Msingi Chamazi,
Jumatano wiki hii.
Inadaiwa kwamba, Zakaria alimwambia Emmanuel ambaye pia ni jirani yake,
kwamba msahafu huo ni mtakatifu na kwamba mtu yeyote ambaye angeuharibu kwa
jambo lolote, iwe ni kuuchana kwa makusudi, kuutemea mate ama kuukojolea
angekufa pale pale, au kugeuka mjusi.
Katika ubishi huo, Emmanuel aliamua kukojolea msahafu huo, akitaka kuona
kama kweli angekufa ama kudhurika, jambo ambalo halikumpendeza rafiki yake
ambaye alikwenda kuwaeleza wazazi wake.
Baba mzazi wa Zakaria, aliwaambia waandishi wa habari kwamba, kutokana na
tukio hilo alilazimika kwenda kwa wazazi wa Emmanuel na kisha kwenda kwa mjumbe
ambaye aliwaelekeza kwenda kituo cha polisi kuandikisha maelezo.
Wazazi wote walikubaliana kuyamaliza mambo hayo, kwa kumwonya mtoto huyo,
lakini habari za kuaminika zinasema kuwa baadhi ya viongozi wa Kiislamu hasa
msikiti wa Chamazi, waling’aka na kutaka jambo hilo lifikishwe ngazi za juu za
uongozi wa Kiislamu.
BAADHI YA PICHA ZA TUKIO HILO
No comments:
Post a Comment