Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe ya mjini Zanzibar, leo imetoa fursa
ya dhamana kwa Viongozi wa makundi mawili ya kidini Zanzibar
wanaotuhumiwa kwa makosa ya kufanya fujo na kupelekea ghasia na vitendo
vya uvunjifu wa amani na uharibifu wa miundombinu ya barabara.
Watuhumiwa hao ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar Sheikhe,
Faridi Hadi Ahmedi na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Uamsho Sheikhe, Mselem
Ali Mselem, Mussa Juma Issa, Suleiman Juma Suleiman, Azan Khalid Hamdan,
Khamis Ali Suleiman na Hassan Bakar Suleiman.
Akisoma uwamuzi huo huku kukiwa na ulinzi mkali eneo lote la Mahakama,
Hakimu wa Makahama hiyo Mh. Msaraka Pinja, amesema kuwa ingawa upande wa
Mashtaka ulikuwa haukutoa pingamizi ya dhamana kwa watuhumiwa, lakini
Mahakama ililazimika kusitisha utoaji dhamana baada ya kupitia mambo
kadhaa ya msingi.
Amesema kuwa pamoja na uzito wa tuhuma zinazowakabili watuhumiwa,
Mahakama ililazimika kusita kutoa dhamana kwanza kwa usalama wa
watuhumiwa wenyewe na kwa kuangalia mazingira yaliyokuwepo wakati huo na
uwezekano wa kuingilia upelelezi wa kesi inayowakabili.
Hakimu huyo alisema wasiwasi wa Mahakama ilikuwa kwamba watuhumiwa hao
wakiwa nje ya dhamana kuna uwezekano wa kutenda kosa lingine,
Kutohudhuria Mahakamani kwa wakati wanapotakiwa na kuangalia kwa mapata
uzito wa kosa wanaloshitakiwa nalo.
Baada ya kuridhika na Mahakama hiyo ilitoa dhamana kwa watuhumiwa wote
saba kwa mashariti ya kuwasilisha mahakamani fedha taslimu kiasi cha
shilingi milioni tatu kwa kila mmoja pamoja na kuwa wadhamini watatu
ambao ni watumishi wa Serikali kwa kila mmoja akitoa kiasi kama hicho
cha fedha mahakamani.
Watuhumiwa hao pamoja na Wadhamini wao, kwa pamoja wametakiwa
kuwasilisha barua kutoka kwa Sheha wa Shehiya anayoishi pamoja na kivuli
cha vitambulisho vya Zanzibar Mkazi na kwa wale wenye Hati za Kusafiria
pia wawasilishe vivuli vya hati hizo Mahakamani.
Pamoja na masharti hayo ya jumla, lakini pia wadhamini wometakiwa wawe
watumishi wa serikali na wawakilishe barua kutoka katika ofisi
wanazozifanyia kazi na vivuli vya vitambulisho vyao vya kazi ili view
kama kumbukumbu mahakamani.
Hata hivyo watuhumiwa wote wamerejeshwa rumande baada ya kushindwa
kutekeleza masharti ya dhamana pamoja na kukabiliwa na kesi nyingine
Mahakama Kuu ya Vuga, kesi ambayo dhamana yake imewekewa pingamizi kwa
hati maalum ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar kwa sababu za kiusalama.
Kesi hiyo imeahirishwa tena hadi Novemba 21, mwaka huu itakapotajwa tena.
Akizungumza mara baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo mmoja ya Mawakili wa
Watuhumiwa hao Bw. Abdallah Juma, amesema yeye pamoja na wakili
mwenzake Bw. Salum Toufik, wataendelea kuwatetea watuhumiwa hao hata
baada ya kutishia kujitoa katika kesi hiyo mwezi uliopita.
Chanzo: mzalendo.net
No comments:
Post a Comment