SEKRETARIETI mpya ya Chama Cha 
Mapinduzi (CCM) iliyoingia madarakani hivi karibuni chini ya uongozi wa 
Rais Jakaya Kikwete, imesema itahakikisha vitendo vya rushwa hasa kwenye
 chaguzi za chama hicho vinakoma mara moja, tofauti na ilivyokuwa 
imezoeleka. 
Kauli hiyo ya viongozi wa juu wa 
CCM, Mwenyekiti Taifa (Rais Kikwete), Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara 
(Phillip Mangula) na Katibu Mkuu (Abdulrahman Kinana) imetolewa jana na 
viongozi hao wakati wakizungumza na wana-CCM Mkoa wa Dar es Salaam 
katika mkutano wa kumpongeza Rais Kikwete kuchaguliwa kushika nafasi 
hiyo tena.
Akizungumza na umati wa wanachama 
hao, Rais Kikwete aliwataka viongozi wapya kufanya kazi ya ziada ya 
kuhakikisha wanarejesha imani ya Watanzania kwa CCM, ambayo haiko kama 
ilivyokuwa zamani. “Lazima kujiuliza nini kimekifanya chama hiki kufikia
 hapo kilipo na kuangalia nini cha kufanya ili kuondokana na hali hiyo. 
Pale mnapohisi hali ya kuungwa mkono inapungua lazima tujiulize, 
kulikoni..! Nini cha kufanya ili kuimarisha chama,” alisema na kuongeza 
kuwa kazi nyingine ni kuhakikisha wanakijenga chama na kuimarisha zaidi 
ili kiendelee kuwaongoza Watanzania.
“Chama chetu hakifanyi 
mikutano…wenzetu wanafanya kwanini sisi hatufanyi, sasa tutatengeneza 
utaratibu maalumu kuhakikisha viongozi wa chama kwa nafasi zao wanafanya
 kazi yao ipasavyo ndani na nje ya chama,” alisema Rais Kikwete. Alisema
 ipo haja ya kujipanga na kuangalia namna ya kupambana na propaganda 
hasi za baadhi ya vyombo vya habari na wapinzani ili kukabiliana na hali
 hiyo. Aliwataka wanaCCM kuacha makundi na chuki ambayo yamekuwa 
yakikigawa chama hicho.
Awali akizungumza Kinana alisema 
vitendo vya rushwa ndani ya CCM watahakikisha vinakoma mara moja ili 
kurejesha imani ya Watanzania iliyopungua kutokana na tuhuma za wachache
 dhidi ya vitendo viovu. Alisema chini ya uongozi wake atahakikisha 
mashaka yaliotawala kwa wananchi dhidi ya CCM yanaondoka kwa kuwaengua 
wale wanaoendeleza vitendo vya rushwa, majumbu na vitendo vinavyo leta 
sifa mbaya ya chama hicho.
“Hatuwezi kuiongoza nchi yetu 
wakati watu wanamashaka na sisi, lazima tuondoe mashaka akisimama 
mwana-CCM wote waseme naam huyu anaweza kusema…sio akisimama mwana-CCM 
kusema watu wanahoji haaah, na huyu naye anakemea rushwa? Aliwataka 
wana-CCM kushirikiana katika kukisafisha chama na si kuwaachia viongozi 
jukumu hilo, ambalo wao kama viongozi wamekubali kuongoza mapambano 
hayo.
 
 


No comments:
Post a Comment