
Tamko hilo limo kwenye  taarifa ya Chadema iliyotolewa na Mkurugenzi wa 
Ulinzi na Usalama Wilfred Lwakatare, iliyotolewa jana jijini Dar es 
Salaam.
Katika andiko hilo, walimtaka Rais Kikwete atekeleze mambo yaliyoandikwa
 kwenye barua ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliyetaka 
serikali ifanye uchunguzi wa matukio ya utesaji yaliyofanywa na vyombo 
vya dola dhidi ya wanaoipinga serikali.
Waraka huo  ulitaka uchunguzi ufanyike dhidi ya polisi waliotumika 
kuteka, kutesa na kuua kwa malengo ya kisiasa ya kupambana na wakosoaji 
wa chama tawala na serikali yake.
Katika taarifa yake, Chadema ilisema walimwandikia Rais wakitaka 
kufanyike uchunguzi huru kwa kuunda Tume ya Kimahakama/Kijaji ili ukweli
 ujulikane na haki ionekane ikitendeka badala ya kutoa lugha ya kisiasa 
kwa nia ya kujikosha mbele ya umma, wakati  CCM na polisi, wanakaa na 
kupanga mikakati inayopelekea kudhulumu haki na roho za Watanzania.
Aidha, wakati uchunguzi huo ukifanyika, watuhumiwa wote, wakiwemo 
viongozi wa CCM, serikali na watendaji wa Jeshi la Polisi waliokubali 
kutumika, hata kuvunja haki za binadamu, katiba na sheria, wanawajibika 
kwa wao kujiuzulu au kufukuzwa kazi.
Rwakatare alisema kauli  iliyotolewa na Mwenyekiti wa CCM, Rais  Kikwete
 kuwataka viongozi na wanachama wa chama hicho waache kutegemea Jeshi la
 Polisi katika kukabiliana na wapinzani ni ushahidi wa tuhuma ambazo 
Chadema imekuwa ikitoa dhidi ya chama hicho.
Hivi karibuni Rais Kikwete, alikitahadharisha chama hicho kuwa 
kikitegemea zaidi polisi kwamba ndiyo msaada kwake katika kujibu mapigo 
ya wapinzani kitashindwa.
Akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa Nane CCM baada ya kuchaguliwa kwa 
mara nyingine kuwa Mwenyekiti kwa miaka mingine mitano, alisema viongozi
 wa CCM lazima wajipange na kuwa wepesi wa kujibu mapigo ya wapinzani.
Alisema jawabu la siasa siyo polisi bali ni wanasiasa wenyewe na kwamba 
polisi hawawezi kuwa jibu la suala la siasa lazima kila kiongozi 
ajitambue yeye mwenyewe ndiyo mwenezi katika eneo lake.
Chadema ilisema Watanzania wanajua kuwa matukio ya vyombo vya dola 
kuhujumu wapinzani na wakosoaji wa serikali ya CCM, kwa nia ya kuilinda 
CCM, yamekwenda kwa sababu watu na makundi ya kijamii pia wameanza 
kuandamwa.
“Mtu, watu au makundi mbalimbali ya kijamii ambayo yanaonekana kutoa 
mawazo mbadala, kudai haki na uwajibikaji yameanza kuandamwa. Mifano 
mizuri hapa ni kufungiwa kwa Gazeti la Mwanahalisi na kutekwa na kuteswa
 kwa kiongozi wa madaktari, Dk. Steven Ulimboka. “  ilisema taarifa ya 
Rwakatare.
Chadema ilisema ukweli huo umesaidia kumaliza fumbo lililokuwepo juu ya 
madai ya muda mrefu kuwa Jeshi la Polisi linatumika kisiasa na viongozi 
wa CCM na watendaji wa serikali.
“Kauli hiyo ya Kikwete imetufikisha kwenye kilele cha ushahidi kuwa 
Jeshi la Polisi linatumika kisiasa kukabiliana na hoja na shughuli 
halali za kisiasa zinazofanywa na Chadema ,  chama mbadala kwa sasa 
kinacholenga kuiondoa CCM madarakani”.
Aidha imesaidia kufumbua fumbo la kwa nini Jeshi la Polisi Mkoani Iringa
  lilitumia nguvu kubwa kuingilia shughuli halalli za  Chadema kufanya 
mikutano ya ndani, ikiwemo ufunguzi wa matawi katika Kijiji cha Nyololo,
 mkoani Iringa, na hatimaye kusababisha kifo cha Mwanandishi wa Habari, 
Daudi Mwangosi, Septemba  mwaka huu.
chanzo : NIPASHE 
 
 

No comments:
Post a Comment