Lowassa akizungumza jana mjini Babati alisema, mjadala kuhusu elimu 
kutolewa bure hadi sekondari haukwepeki, hivyo kuwataka wadau wa elimu 
kuanza sasa kujadili suala hilo na kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) 
kinapaswa kulifanya hilo kuwa moja ya ajenda zake katika Uchaguzi Mkuu 
wa 2015.
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema wakati umefika kwa sasa 
hapa nchini elimu ya Sekondari iwe elimu bure na kumwondolea mwananchi 
wa kawaida mzigo wa kubeba gharama za elimu hiyo.
Lowassa akizungumza jana mjini Babati alisema, mjadala kuhusu elimu 
kutolewa bure hadi sekondari haukwepeki, hivyo kuwataka wadau wa elimu 
kuanza sasa kujadili suala hilo na kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) 
kinapaswa kulifanya hilo kuwa moja ya ajenda zake katika Uchaguzi Mkuu 
wa 2015.
Alisema elimu ya sekondari ikifanywa bure, itakuwa ni fursa kwa kila 
mtoto wa Kitanzania kuipata. Hatua ambayo itaongeza weledi na uelewa wa 
mambo mengi katika jamii.
“Ninasema sasa wakati umefika elimu ya sekondari kuwa kama elimu ya 
msingi kwa watoto kusoma bure kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha 
nne,” alisisitiza Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli (CCM).
Kwa kauli hiyo, Lowassa ni kama ameunga mkono Sera ya Chama cha 
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao waliingia katika mgogoro na CCM 
kuhusu elimu kutolewa bure wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Chadema wamekuwa wakisisitiza kwamba elimu bure inawezekana hadi ngazi 
ya sekondari, lakini wakati wote CCM wamekuwa wakisema kuwa suala hilo 
haliwezekani na kwamba kauli za aina hiyo ni kuwahadaa wananchi.
Katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, aliyekuwa mgombea wa urais kupitia 
Chadema, Dk Willibrod Slaa alitumia sera ya elimu bure kuanzia chekechea
 hadi sekondari kama kete ya kusaka ushindi, huku akisema chama chake 
kingetenga asilimia 35 ya bajeti kwa ajili ya kuboresha elimu na kutoa 
elimu bure.
Hata hivyo, aliyekuwa mgombea wa CCM na baadaye kupata ushindi, Rais 
Rais Jakaya Kikwete alikuwa akiwatahadharisha wapigakura kuwa kwamba 
ahadi ya Chadema ni hewa na kwamba hilo lisingewezekana.
Mvutano huo uliwaingiza makada wengine ambao ni Katibu Mkuu wa CCM, 
Abdulrahman Kinana ambaye wakati huo alikuwa Meneja Kampeni wa CCM na 
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta na kwa upande wa
 Chadema, Dk Kitila Mkumbo naye alijitokeza kutetea sera ya chama chake.
Katika mkutano wa kampeni za CCM uliofanyika Novemba 10, 2010 katika 
Kata ya Mchangimbore katika Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma, Rais 
Kikwete alisema “Serikali haiwezi kutoa huduma za jamii bure” na kwamba 
lazima wananchi wachangie.
“Nimebahatika kukaa serikalini muda mrefu hiyo sera ya bure tulijaribu 
na ikatushinda na wakati huo Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, 
tulikaa naye tukaona hilo haliwezekani tukaamua tubadilishe sasa 
nawashangaa wenzetu wanawadanganya eti watatoa bure.”
Kwa upande wake Dk Slaa akiwa mjini Arusha katika moja ya mikutano yake 
alisema kwamba CCM walikuwa wakipinga sera ya elimu bure hadi sekondari 
kutokana na kulea ubadhirifu na kuthamini anasa kuliko maendeleo kwa 
wananchi.
Kauli ya Lowassa
Jana akizungumza muda mfupi kabla ya kuanza kuendesha harambee ya ujenzi
 wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Babati, 
Lowassa alisema wakati umefika kwa kila Mtanzania kuzungumzia suala hilo
 bila ya woga.
Chanzo: mwananchi.co.tz
 
 


No comments:
Post a Comment