VIGOGO WAPYA, MAWAZIRI KUANZA ZIARA MIKOANI
KATIKA mikakati yake ya kupambana na nguvu za operesheni za CHADEMA 
mikoani, Chama cha Mapinduzi (CCM), kimelazimika kuwatumia viongozi wake
 wapya wakiongozana na mawaziri ili kwenda mikoani kufafanua kwa 
wananchi jinsi serikali ilivyotekeleza ilani yake.
Hii itakuwa ni mara ya pili kwa chama hicho kujaribu kukabiliana na 
upinzani wa CHADEMA mikoani, ambapo mwaka jana baada ya mkutano wao wa 
maazimio ya kujivua gamba, walijitahidi kuzunguka baadhi ya mikoa bila 
kufua dafu.
Operesheni zinazofanywa na CHADEMA za Sangara na sasa Vuguguvu la 
Mabadiliko (M4C), zimeitikisa CCM na hivyo wajumbe wake kutumia muda 
mwingi kwenye mkutano mkuu wao uliomalizika mjini Dodoma, kujitapa kuwa 
lazima wafanye mashambulizi ya kuwasambaratisha.
Akitangaza mkakati huo mpya jana kwa waandishi wa habari wa kuchanja 
mbunga kwa kutumia anga kwa helikopta kama CHADEMA, Katibu wa 
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema 
wameanda ziara ya siku nne katika mikoa minne.
Alisema ziara hiyo itaongozwa na sekretarieti mpya chini ya Katibu wake 
Mkuu, Abdullahman Kinana, na kuwashirikisha baadhi ya mawaziri.
Nape alisema kuwa ziara hiyo ni ya chama na sio ya kiserikali na kwamba 
itaanza kesho hadi Novemba 24 katika mikoa ya Mtwara, Arusha, Geita na 
Rukwa.
Akifafanua zaidi alisema Kinana ataanzia Mtwara ambako atakuwa na 
mawaziri husika wanaoshughulikia masuala ya kilimo ili kuzungumzia zao 
la korosho na waziri wa uchukuzi atakayezungumzia bandari na 
miundombinu.
Nape aliongeza kuwa wakiwa Sumbawanga watazungumzia miundombinu na kwa 
Geita watafuatilia migogoro ya migodi na kumalizia Arusha kwa kuangalia 
harakati za kufufua viwanda kwani vinaathiri ajira.
Nape alisema kuwa lengo la kuongozana na baadhi ya mawaziri ni kutoa 
maelezo ya papo hapo hasa kwa mambo yanayosuasua ikiwemo kuwawajibisha 
bila kusubiri Bunge kufanya hivyo.
“Lengo tunasukuma spidi ya utekelezaji wa maendeleo na ilani ya uchaguzi
 na tunajikita kwa baadhi ya mambo na kuendeleza mageuzi ndani ya chama 
na ndio azimio tuliloondoka nalo katika mkutano mkuu wa nane,” alisema.
Akizungumzia kung’atuka kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Wilson
 Mukama, Nape alisema kiongozi huyo ameondoka ili akasimamie uanzishwaji
 wa chuo cha uongozi cha CCM, ambacho kitasaidia makada kuwa na nidhamu 
na uwajibikaji.
Akijibu hoja za CHADEMA zinazodai CCM imetekeleza ilani ya chama hicho 
hususan katika suala la elimu na kupunguzwa kwa bei za vifaa vya ujenzi,
 Nape alisema kuwa suala la elimu bure ni la CCM.
“Suala hilo lilianza wakati wa TANU chini ya Mwalimu Julius Nyerere na 
hata hao kina Dk. Slaa wamesomeshwa bure na TANU,” alisema.
CHADEMA wajiimarisha
Wakati CCM ikianza ziara mikoani, Chama cha Demokrasia na Maendeleo 
(CHADEMA), kimeanza kujiimarisha kwa kuendesha mafunzo ya darasani na 
vitendo, kwa lengo la kuwajengea uwezo wenyeviti na makatibu wa mikoa 32
 ya kichama.
Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi 
wa Mafunzo na Oganaizesheni wa CHADEMA, Benson Kigaila, alisema kuwa 
mafunzo hayo yatafanyika Novemba 22 hadi 23, mwaka huu, wilayani 
Karagwe, mkoa wa Kagera.
Kigaila alisema baada ya mafunzo hayo wataingia kwenye vitendo ambapo 
makatibu na wenyeviti hao watasambaa kushambulia vitongoji na vijiji 
vyote vya wilaya ya Karagwe, kwa kufanya mikutano ya hadhara katika 
maeneo hayo.
Alibainisha kuwa mafunzo hayo ya vitendo ni sehemu ya utekelezaji wa 
mikakati mbalimbali ya ujenzi na uimarishaji wa chama, hususan 
operesheni ya M4C ambayo imesaidia viongozi kuzungumza na wananchi 
kupitia mikutano ya ndani na hadhara.
Kuhusu M4C, Kagaila alisema wakati viongozi hao waliopata mafunzo 
wakiendelea, chama kitatoa ratiba ya operesheni hiyo kubwa 
itakayoendelea kufanyika kwa nchi nzima.
Habari hii imeandaliwa na Happiness Mnale na Shehe Semtawa
Chanzo; Chadema.blog
 
 


No comments:
Post a Comment