MBUNGE wa
Singida Mashariki Tundu Lissu (CHADEMA), ambaye pia ni mnadhimu mkuu wa
kambi ya upinzani bungeni, amesema anakusudia kuleta hoja binafsi
bungeni kumshitaki Rais Jakaya Kikwete kwa madai kuwa amevunja katiba
kwa kuteua majaji wasio na sifa.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana mjini hapa, Lissu alisema anakusudia kufanya
hivyo katika Bunge la Februari mwakani baada ya rais kuendelea kuteua
majaji wasio na sifa.
Alisema
anakusudia kuwasilisha hoja ya kumsitaki rais bungeni kwa kutumia kanuni
za kudumu za Bunge sehemu ya 11 na Ibara ya 46A na 46B ya katiba ya
sasa kifungu cha 121,122,123,124,125 na 126 ya azimio la kumwondoa rais
madarakani.
Lissu
alisema pamoja na mambo mengine, rais amekuwa kiongozi wa kuvunja katiba
ya nchi kwa kiasi kikubwa kwa kitendo chake cha kuendelea kuteua majaji
‘vihiyo’.
Aidha,
alisema hata kama Bunge litashindwa kufanya maamuzi ya kumwondoa rais
madarakani kutokana na uvunjifu wa katiba kwa uteuzi mbovu wa majaji,
ataangalia utaratibu wa kumshitaki katika vyombo vya sheria.
Katika hatua
nyingine, Lissu alimtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda, kusoma ripoti ya
Tume ya Ngwilizi iliyokuwa ikimchunguza na kumhoji kwa madai kuwa
alitoa kauli ya kuwadhalilisha majaji na kudhalilisha muhimili wa
mahakama kwa kile alichosema kuwa, majaji wengi hawafai kwani hawana
sifa.
Alisema
kutokana na kauli yake ya Julai 13, mwaka huu ambayo aliitoa bungeni
wakati akiwasilisha hotuba ya Waziri kivuli wa Katiba na Sheria, Lissu
aliwataja majaji walioteuliwa na rais kwamba hawana uwezo na sifa za
kuwa majaji jambo ambalo lilimfanya Spika Makinda kuunda kamati ya
kumshitaki katika Kamati ya Bunge ya Maadili na kinga bungeni ili atoe
maelezo na ushahidi.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment