Pages


Photobucket

Monday, November 5, 2012

TANESCO SASA KUMEKUCHA...




Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi

WAFANYAKAZI MAMIA WAPANGULIWA, WENGINE WAFUKUZWA, KISA TUHUMIWA ZA WIZI, HUJUMA


TETEMEKO limeendelea kulikumba Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kutokana na mamia ya wafanyakazi wa shirika hilo kupanguliwa kama hatua ya kuvunja mtandao wa wizi na hujuma ndani yake.

Habari ambazo Mwananchi lilizipata na kuthibitishwa na uongozi wa juu wa Tanesco zinasema hadi sasa wafanyakazi 190 wa Tanesco wameshakabidhiwa barua za kuhamishwa na nusu ya watumishi hao ni katika Mkoa wa Dar es Salaam pekee.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, wafanyakazi 95 wamepanguliwa kutoka katika mikoa ya Tanesco iliyopo katika Jiji la Dar es Salaam pekee na wamehamishiwa mikoani ambako wanatakiwa wawe wameripoti katika vituo vyao vipya vya kazi ifikapo Novemba 15, mwaka huu.

Kadhalika idadi kama hiyo ya watumishi kutoka mikoani wamehamishiwa Dar es Salaam, hatua ambayo inalenga kuimarisha utendaji katika jiji hilo ambalo licha ya kuwa kitovu cha uchumi wa nchi, huduma za Tanesco zimekuwa zikilalamikiwa kuwa haziridhishi.

Hatua hiyo ya kupangua wafanyakazi hasa wa Dar es Salaam, imekuja siku chache tangu Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco ilipomwachisha kazi rasmi aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu, William Mhando kutokana na ukiukwaji wa maadili ya uongozi.

Kadhalika tayari Tanesco imeshawafukuza kazi wafanyakazi wake 29 waliothibitika kufanya makosa ya wizi wa fedha za shirika na hujuma katika miundombinu ya umeme, huku wafanyakazi wengine 19 wakiwa wamesimamishwa kazi wakati uchunguzi wa tuhuma zao ukiwa bado unaendelea.

Wafanyakazi waliosimamishwa ni tofauti na vigogo waliosimamishwa pamoja na Mhando ambao pia hatima yao inaweza kujulikana wiki hii, baada ya uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili kukamilika.

Hao ni pamoja na Naibu Mkurugenzi Mtendaji Huduma za Shirika, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi Ununuzi, Harun Mattambo.


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Felchem Mramba akizungumza na gazeti hili, alikiri kuwapo kwa uhamisho wa wafanyakazi hao na kwamba huo ni utaratibu wa kawaida wa shirika.

“Ni kweli kwamba tunafanya marekebisho ya utendaji wetu wa ndani, ni suala la kawaida tu, kwani kuna ajabu gani kuwahamisha watu? Tunaimarisha utendaji wetu, kwa hiyo mimi sidhani kama hilo ni jambo kubwa,” alisema Mramba na kuongeza:

“Nadhani ninyi mnafahamu kwamba tuna changamoto ya kukabiliana na malalamiko ya wateja wetu, tunatakiwa kutoa huduma kukidhi mahitaji yao, kwa hiyo tunajitizama hapa na pale, ili kuona kama tunaweza kuimarisha utendaji na kukidhi matakwa ya tunaowapa huduma.”

Sababu za Kupanguliwa

Habari kutoka ndani ya Tanesco zinasema kuwa sababu kubwa za kupanguliwa kwa wafanyakazi hao, wengi wakiwa ni wasimamizi wa ndani na nje (supervisors & foremen), ni kuvunja mtandao wa wizi na hujuma hasa katika Jiji la Dar es Salaam.

“Watu wengine wamekaa kwenye vituo kwa miaka mitano mpaka saba, wamejenga mitandao mikubwa ya wizi wa umeme na ndiyo maana kwenye operesheni zimefanyika mmeona jinsi watu ambavyo wamekuwa wakiiba umeme,” alisema mmoja wa watumishi wa Tanesco ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe na kuongeza:

“Kwa hiyo kwa hatua hii, mtandao wa wizi na hujuma kwenye shirika ni kama umevunjwa maana nasikia kwamba uhamisho kwa ngazi za juu zaidi nao unafuata na lengo ni hilohilo”.

Mtumishi mwingine ambaye pia aliomba jina lake lihifadhiwe alisema, Tanesco huenda ikawa imepata hasara kubwa ya kifedha kutokana na wizi wa umeme ambao umekuwa ukifanywa na maofisa wa shirika hilo kwa kusadia wateja kuchezea mita, hivyo kupata umeme bure.

“Hata wale jamaa waliokutwa wakiuza kadi za Luku kule Mwananyamala, hawawezi kufanya hivyo bila kusaidiwa na wafanyakazi wa ndani ya shirika. Hivyo wapo watu waliobambwa, hao wamefukuzwa lakini wengine ambao tuhuma zao hazikuthibitishwa wamehamishwa,” alisema mtumishi huyo.

Habari zaidi zinasema wizi wa umeme ndani ya Tanesco umekuwa ukifanywa kupitia mtandao wa wafanyakazi wa idara tofauti ambazo hufanya kazi kwa kutegemeana, hivyo siyo rahisi kwa mtu mmoja kufanikisha wizi huo.

“Wizi wa hapa ni kwa mtandao, kwa mfano mtu wa hapa Kinondoni hawezi kufanikisha wizi wa units za umeme bila kushirikiana na watu wa makao makuu, nao lazima wawe wawili au zaidi, halafu hata yeye wa hapa hawezi kuwa peke yake, kwa hiyo huu ni mtandao mkubwa sana,” kilisema chanzo chetu.

Uchunguzi zaidi wa gazeti hili umebaini kwamba baadhi ya watumishi katika vituo vya Dar es Salaam ni kama wameshushwa vyeo, kwani wamehamishwa kutoka vituo vikubwa kama makao makuu ya mikoa na kupelekwa katika vituo vidogo, ambako hakuna majukumu makubwa kama waliyokuwa nayo mwanzo.

Kadhalika habari zaidi zinasema uhamisho huo, pia unawagusa watumishi walioguswa na tuhuma zaidi ya 175 zilizowasilishwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi wakati wa kikao cha uongozi wa wizara na wafanyakazi wa Tanesco kilichofanyika Mei 19 mwaka huu.

Mramba akizungumzia tuhuma hizo jana alisema: “Hatujazikalia kimya, tuhuma hizo, tumezifanyia kazi na tuko katika hatua mbalimbali kulingana na makosa yaliyotajwa.”

Mramba katika maelezo yake alisema kati ya watumishi 29 waliofukuzwa au kuachishwa kazi na wale ambao wamesimamishwa kwa ajili ya kuchuguzwa, baadhi yao ni wale waliotajwa katika mkutano wa wafanyakazi na viongozi wa wizara.

Habari zaidi zinasema katika maeneo ambako kulikuwa na tuhuma za upotevu wa fedha, Tanesco walilazimika kufanya ukaguzi wa hesabu na kwamba katika sehemu ambako wizi au upotevu wa fedha ulithibitika, wahusika wamefukuzwa au kuachishwa kazi.

Mkutano wa Mei

Katika mkutano wa Mei, wafanyakazi wa Tanesco walimkabidhi Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo majina ya vigogo wa wizara yake wanaodaiwa kulihujumu shirika hilo.

Tukio hilo lilitokea wakati waziri huyo akiwa na Manaibu Waziri wake, George Simbachawene na Steven Masele pamoja na Maswi, walipozungumza na wafanyakazi wa Tanesco Kanda ya Dar es Salaam na Pwani.

Agizo la kukusanya majina hayo lilitolewa na Maswi muda mfupi baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Majadiliano ya Shirika hilo, Abdul Mkama kutoa taarifa kwa niaba ya wafanyakazi iliyoeleza kuwa kuna vigogo katika wizara hiyo na wafanyakazi wengine wa Tanesco, wanaojihusisha na vitendo vya hujuma.

Katika mkutano huo, Mkama alisema Kamati yake ya Majadiliano inawafahamu kwa majina vigogo wa wizara  hiyo wanaojihusisha na njama za kulihujumu shirika hilo kwa lengo la kuingiza wawekezaji wanaowataka katika sekta hiyo.

Miezi miwili baada ya tuhuma hizo, Bodi ya Tanesco ilimsimamisha Mhando pamoja na watendaji wakuu wengine wa Tanesco ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.

Nafasi ya Mhando imechukuliwa na Mramba ambaye alikuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Masoko na Usambazaji wa Tanesco.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment