Ibrahim Haruna Lipumba -Mwenyekiti Chama Cha Wananchi CUF
----
Siku ya Alhamis nikielekea Muhimbili kumpeleka shangazi yangu
hospitali nilipata taarifa kuwa Imam wa msikiti wa Masjid Haq (ulioko
jirani na Afisi Kuu ya CUF na ambapo nasali sala ya Ijumaa nikiwa Afisi
Kuu) na watu wengine watatu akiwemo Sheikh Ramadhan S. Sanze (ambaye
namfahamu kwa muda mrefu). Sadik Gogo na Mzee Abdillah wamekamatwa na
wamefikishwa kituo cha polisi cha kati (Central Police Station).
Nilistushwa na kamata kamata hii na nikahofia kuwa inaweza kuongeza
jazba miongoni mwa waumini wa Kiislam. Baada ya shangazi kupata tiba
katika hospitali ya Muhimbili nilimrudisha nyumbani na nikampigia simu
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na mahusiano ya umma, Abdul Kambaya,
tukutane kituo cha polisi cha kati kuulizia sababu za kukamatwa Imam wa
Masjid Haq na wenzake watatu na kama tunaweza kuwawekea dhamana.
Tulipofika kituo cha polisi tulibaini kuwa Imam wa Msikiti wa Masjid
Haq hajakamatwa bali kuna muumini mwingine kwa jina la Mkadam Swalehe
ndiye aliyekamatwa. Tulizungumza na RPC Kova na RCO Msangi kuhusu
kuachiliwa kwa wale waliokamatwa. Tukafahamishwa kuwa itabidi wafanyiwe
mahojiano na baadaye wataachiliwa isipokuwa Mkadam Swalehe ambaye ana
faili jingine pale polisi linaloendelea kufanyiwa upelelezi.
Tulifahamishwa kuwa nitume mtu saa 10:30 jioni ili aweze kufuatilia
utaratibu wa kuachiliwa watuhumiwa watatu akiwemo Sheikh Ramadhan Sanze,
Sadik Gogo na Mzee Abdillah.
Nilishauriana na Wakurugenzi wa CUF walioko Dar es Salaam na Naibu
Katibu Mkuu, Julius Mtatiro hatua za kuchukua. Taarifa za kukamatwa
Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake zilikuwa zinaenea na kupandisha jazba
ya Waislam wengi. Tulipata wasiwasi kuwa jazba hii inaweza kupelekea
Waislam wengi kuandamana baada ya sala ya Ijumaa. Ikiwa Sheikh Ramadhan
Sanze na wenzake wataachiwa na Waislam wakapata taarifa hiyo inaweza
kusaidia kupunguza jazba na watu wasishiriki maandamano baada ya sala ya
Ijumaa.
Nilimpa jukum Abdul Kambaya afuatilie Central PoliceStation, suala la
kuachiliwa Sheikh Sanze na wenzake. Niliwasiliana naye kwa simu na
kuzungumza na RCO na nikaamini kuwa Sheikh Ramadhan Sanze, Sadik Gogo na
Mzee Abdillah wataachiwa baada ya kukamilisha mahojiano. Ilikuwa
inakaribia saa 12 jioni. Muda wa kuitisha Press Conference haukuwepo.
Tukakubaliana Naibu Katibu Mkuu awasiliane na wahariri wa habari wa
vituo vya televisheni Channel 10, TBC1, Star TV, Mlimani TV na ITV ili
niweze kutoa taarifa ya kuwasihi Waislam warudi majumbani na kwenye
shughuli zao baada ya sala ya Ijumaa.
Niliweza kufanya mahojiano na
Channel 10, TBC1, na ITV. Kwa bahati mbaya Camera person wa Star TV
alikuwa kwenye shughuli nyingine na kwa hiyo sikuweza kufanya mahojiano
na Star TV. Vilevile wapiga picha wa Mlimani TV hawakuwepo kwenye
studio. Pia nilipata bahati ya kuzungumza na Radio Iman inayosikilizwa
na Waislam wengi na kueleza maoni yangu kuwa Waislam wasiandamane baada
ya sala ya Ijumaa.
Baada ya kutoa taarifa kwenye vituo vitatu vya televisheni na Radio
Iman kuwa Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake wataachiliwa na kuwasihi
Waislam wasishiriki maandamano baada ya sala ya Ijumaa nilimpigia simu
Abdul Kambaya kuulizia kama naweza kuzungumza na Sheikh Ramadhan Sanze.
Kambaya akanieleza mambo yamebadilika na hawajaachiwa. Niliwasiliana na
RCO na nikabaini kuwa suala hilo haliko tena chini ya uamuzi wake na
litakamilishwa siku ijayo.
Usiku wa alhamisi kuamkia Ijumaa nilijaribu kuwasiliana na Rais
Kikwete kupitia wasaidizi wake ili nimfahamishe mantiki na sababu ya
hatua nilizochukua na atumie uwezo wake alionao Sheikh Ramadhan Sanze na
wenzake waachiliwe. Kwa bahati msaidizi mmoja alipata ujumbe wangu wa
simu na akanipigia simu saa 6:50 usiku na kunifahamisha atajitahidi
kuufikisha ujumbe wangu kwa Mhe. Rais ili nipate kuongea naye kuhusu
jamaa wanaoshikiliwa na polisi waachiwe ili kupunguza jazba na kuepusha
shari. Niliyezungumza naye alikuwa Dodoma na Rais alikuwa Arusha na
ratiba yake ilikuwa imebana sana na kwa hiyo hakuweza kupata fursa ya
kunipigia simu siku hiyo ya Ijumaa.
Siku ya Ijumaa Abdul Kambaya aliendelea kufuatilia kuachiwa kwa
Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake Central Police Station. Nami katika
kuhangaika ili waliokamatwa waachiliwe nilipata fursa ya kuzungumza na
IGP na kumfahamisha sababu ya juhudi nilizochukua na mategemeo yangu
kuwa Sheikh Sanze na wenzake wangeachiwa. Ninakiri kuwa katika
mazungumzo ya simu, IGP Mwema alikuwa msikivu na mkarimu sana katika
kauli yake. Alinishukuru kwa kauli niliyoitoa katika vituo vya
televisheni na kuwa atafuatilia suala nililomueleza. Hatimaye Sheikh
Ramadhan Sanze na wenzake waliachiwa.
Naamini kama Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake wangeachiwa ingesaidia
sana kupunguza jazba. Hata hivyo Waislam wengi na wananchi wengine kwa
ujumla walipokea vizuri wito wangu na hawakushiriki katika maandamano.
Baadhi wamenikosoa na kushauri kuwa ilifaa nisubiri mpaka baada ya
maandamano kufanyika na kama patatokea majeruhi na vifo ndipo nitoe
tamko la kulaani vitendo vya polisi na serikali.
Katika mitandao ya kijamii wengine wamekejeli juhudi zangu.
Nilikubali kushiriki katika kipindi cha Makutano show kinachoendeshwa na
Bi. Fina ambapo hupata maswali toka Jamii Forum. Moja ya swali
lililotolewa ni “Muulize very very solid, kuna agenda gani kati ya Cuf
na uislam? mtaani leo wanasema kauli ya Lipumba ya jana kusitisha
maandamano wameitii, na ukiangalia mikutano yake pale jangwani utafikiri
kuna mawaidha ni balaghashia na baibui.” Fina hakupata muda wa
kuniuliza swali hili. Jibu lake ni la wazi.
CUF inasimamia Haki Sawa kwa Wananchi Wote. Kuna Watanzania wengi
ambao ni Waislam na wao pia wanastahiki kutendewa haki katika nchi yao.
Kuhusu balaghashia na baibui ni vyema vijana wakatazama picha za umati
wa watu uliokuwa unahutubiwa na Mwalimu Nyerere wakati wa kupigania
uhuru wa nchi hii. Picha hizo pia zinaonyesha waliokuwa wakipigania
uhuru wengi walivaa balaghashia na baibui hata Mwalimu Nyerere alipewa
zawadi nyingi za balaghashia na akaamua kuzivaa.
Kushamiri kwa demokrasia ya kweli msingi wake mkubwa ni amani na
utulivu. Amani ya kweli haipatikani bila kuwepo haki. Kesi ya Sheikh
Ponda msingi wake na madai ya kiwanja. Ki msingi kesi ya madai ya
kusuluhishwa na Mahakama ya ardhi. Sheikh Ponda ana haki ya msingi ya
kupewa dhamana hata kama kauli zake haziifurahishi serikali.
Nasikitika sana katika kipindi hiki tete, viongozi wa serikali
wameshindwa kuchukua juhudi za makusudi kuzungumza na Maimam wa misikiti
na viongozi wa asasi za Kiislam kupunguza jazba. Badala yake wameachia
kauli za vitisho vya Kamanda Kova ndiyo viwe mawasiliano kati ya
serikali na Waislam. Ni vyema serikali ikatumia busara na kuwasiliana na
Maimamu wa misikiti na viongozi wa asasi za Kiislam kuelewa hoja na
malalamiko yao.
Hatimaye nimepata fursa ya kuzungumza na Mheshimiwa Rais leo asubuhi
na nikamueleza juhudi nilizozichukua kuweza kupunguza jazba na kuwaomba
Waislam wasishiriki kwenye maandamano baada ya sala ya Ijumaa. Ni wazi
hali hii ya mtafaruku ndani ya jamii inamsononesha sana Mheshimiwa Rais
na ninaamini atajitahidi kwa uwezo wake wote kutafuta suluhisho.
Katika kutafuta suluhu ya mtafaruku huu nitaendelea na jitihada za
kutafuta fursa niweze kubadilishana mawazo na Rais Kikwete. Nitazungumza
na viongozi wa asasi za Kiislam. Nitazungumza na viongozi wa Makanisa
ya Kikristo. Madhumuni ya mazungumzo yangu ni kuwafahamisha mantiki ya
juhudi nilizofanya na kushauriana misingi muhimu ya Waumini wote
kuheshimiana na kuvumiliana ili tujenge Tanzania yenye haki sawa kwa
wote.
Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti
Novemba 4 2012
Mwenyekiti
Novemba 4 2012
No comments:
Post a Comment