FAMILIA ya aliyekuwa mwandishi wa Habari wa Kituo cha Televisheni cha
Channel Ten, Daud Mwangosi anayedaiwa kuuawa na polisi akiwa kazini,
inakusudia kuishtaki serikali na Idara ya Polisi kwa kusababisha mauaji
hayo.
Marehemu Daud Mwangosi
Mwangosi aliuawa Septemba 2, mwaka huu wakati akikusanya habari za
ufunguzi wa tawi la Chadema Kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi.
Kusudio la kuishtaki serikali limekuja huku askari anayedaiwa kumuua
Mwangosi, Pacificius Cleophase Simon akiwa amefikishwa katika Mahakama
ya Wilaya ya Iringa, kesi inaendelea.
Akizungumza kwa simu jana, mke wa Mwangosi, Itika alisema familia hiyo
imeamua kuchukua uamuzi huo baada ya kuona viongozi wa serikali
hawajali.
Itika alisema hadi sasa familia hiyo inajiuliza maswali ya
kilichosababisha polisi watumie nguvu kubwa kumuua mume wake na kwamba,
wanadhani wanao wajibu wa kuishtaki serikali na polisi.
“ Ukiangalia picha ile unaona kwamba Mwangosi kabla ya kuuawa alikuwa
amezungukwa na askari saba, ni kwanini aliuawa kama jambazi, bado wingu
zito limetanda katika familia na tunadhani haki itapatikana mahakamani,”
alisema Itika.
Alisema wako katika mazungumzo na wanasheria watakaowasaidia katika kesi hiyo na kwamba, wakikamilisha wananchi watajulishwa.
Ripoti ya kamati iliyoundwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa
la Wahariri Tanzania (TEF) kuchunguza kifo hicho, ilisema Mwangosi
aliuawa kwa makusudi na polisi chini ya usimamizi wa Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda.
Edited by Midraji Ibrahim
Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment