Pages


Photobucket

Sunday, November 11, 2012

BASHE: “LOWASSA ATAGOMBEA URAIS 2015, NITAMPIGIA KAMPENI, NITAMPA KURA YANGU”; AMTAJA MEMBE (MB, W) KUHUSIKA NA VIPEPERUSHI DHIDI YA RAIS KIKWETE

Picture
Wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM taifa, Ma' Salma Kikwete, Bernard Membe (Mb, W) na Ridhwani Kikwete wakijadiliana jambo muda mfupi kabla ya ufunguzi rasmi wa mkutano wa Halmashuari kuu ya CCm taifa katika jengo la White House, mjini Dodoma, Novemba 10, 2012.
Habari imeandikwa na Danson Kaijage, Dodoma via TanzaniaDaima

WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinaanza mkutano wake mkuu leo mjini Dodoma, vita ya makundi ya urais 2015, imeshika kasi kwa makada wake kutajana hadharani kuhusika kusambaza vipeperushi vya kutaka kumhujumu na kumng’oa Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Rais Jakaya Kikwete.

Makundi yaliyoingia katika mzozo huo, moja linadaiwa kuwa la wafuasi wa Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na lingine la Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe, kila moja likitaka kuwa karibu na Rais Kikwete.

Hatua ya makada wa makundi hayo ya CCM kutajana na kushutumiana hadharani kutaka kumhujumu mwenyekiti wao wa taifa, imekuja siku chache baada ya hivi karibuni gazeti hili kufichua uasi huo, ili wajumbe wa mkutano mkuu wampigie kura za maruhani kuonyesha kutokuwa na imani nae.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana mjini hapa, mjumbe wa Mkutano Mkuu, Husein Bashe alimtaja hadharani Waziri Membe kwamba anahusika kusambaza vipeperushi vya kumhujumu Rais Kikwete.

Bashe aliamua kumlipua Membe baada ya yeye pamoja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, kutajwa kuhusika na uasi huo.

Wengine waliotajwa kuhusika na vipeperushi hivyo ni Beno Malisa, na Fred Lowassa kuwa ndio wanahusika na njama hizo.

Vipeperushi hivyo vimeandikwa kuwaomba wanachama wa CCM kumpigia kura ya hapana Kikwete kwa madai kwamba chama kinayumba, hivyo apunguziwe mzigo ili abaki na urais tu.
Picture: Ujumbe wa baadhi ya wana CCM kutaka kumng'oa Mwenyekiti kofia yake
picha via Lukwangule blog
Akikanusha kuhusika na hilo, Bashe alisema hana mpango wa kufanya kampeni kwa ajili ya kupunguza kura za Rais Kikwete, na hausiki kwa namna yoyote kutengeneza na kusambaza vipeperushi hivyo.

Alisema vipeperushi hivyo vimeandaliwa na watu wa kundi la Waziri Membe, lakini ametumia ujanja kujifanya hausiki navyo, na badala yake wameamua kuwataja yeye na Mgeja kwamba wanahusika, jambo ambalo alisema sio kweli.

Bashe alisema tayari ameshaandika barua kwa Katibu Mkuu wa CCM, Willison Mkama kumlalamikia kuhusishwa na tuhuma hizo na kutaka chama kifanye uchunguzi.

“Ikithibitika kuwa nimehusika na njama hizo, hatua kali zichukuliwe dhidi yangu,” alisema.

Bashe alimshambulia Waziri Membe kuwa ni kiongozi mnafiki na amekuwa akitumia makundi kuwachafua wengine na kujenga chuki miongoni mwa wana CCM.

Huku akitumia lugha kali na isiyo na staha kwa Waziri Membe, alisema kiongozi huyo amekuwa akifanya siasa za kihuni na kinafiki, hivyo hana sifa ya kushika madaraka ndani ya CCM.

Mwanasiasa huyo machachari ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), alitoa tuhuma nzito kwamba Waziri Membe amekuwa akiwatumia watu ambao alidai hawana akili za kufikiria, kukivuruga chama.

Alimtaja Naibu Waziri wa Malisili na Utalii, Lazaro Nyalandu kwamba anashirikiana na Waziri Membe kuihujumu CCM.

Kwa mujibu wa Bashe, wengine wanaotumiwa na Waziri Membe ni Beno Malisa na Martin Shigela na kuongeza kwamba ndio wanaotumika kupandikiza chuki kwa vijana ili kuidhoofisha CCM.

“Membe amekuwa na fikra za kukihujumu chama na kuandaa mazingira ambayo tusipokuwa makini, yatasababisha nchi ichukuliwe na wapinzani mwaka 2015,” alisema.

Bashe hakuishia hapo, kwani alisema Waziri Membe ni mwanasiasa aliyezoea kubebwa kwenye uchaguzi wa ndani na nje ya chama, na kuwataka wana CCM wasimpigie kura katika uchaguzi wa NEC, kupitia kapu maalumu, unaotarajiwa kufanyika kuanzia kesho mjini hapa.

Akizungumzia unafiki wa Waziri Membe, Bashe alimshangaa kwa kushindwa kuwataja vigogo wanaodaiwa kutorosha mabilioni ya fedha nchini Uswisi kwani aliahidi kufanya hivyo.

Bashe aliapa kuwa kamwe hawezi kumpigia kura na kwamba atafanya kampeni kwa wajumbe wasimpigie kwa madai kuwa hana sifa ya kuwa kiongozi.

“Kamwe Membe hawezi kufanikisha mbinu zake chafu, na kimsingi nitafanya kampeini kuhakikisha hapati nafasi ya ujumbe wa NEC kwani ni kiongozi anayesababisha makundi ndani ya chama,” alisema Bashe.

Alipoulizwa kama yeye ni kibaraka wa Lowassa, Bashe alikana, lakini alisema anamuunga mkono kwa kila jambo analofanya.

“Mimi sio kibaraka wa Lowassa, lakini atagombea urais mwaka 2015, nitampigia kampeni na nitampa kura yangu kwani ni mwanasiasa mvumilivu, mzalendo na kama asingekuwa mvumilivu ni wazi kwamba nchi ingekuwa katika sura nyingine, hata mimi nimejifunza mambo mengi kutoka kwake,” alisema.

Waziri Membe alipotafutwa kwa simu hakuweza kupatikana, lakini msaidizi wake aliliambia gazeti hili kuwa yuko mkoani Shinyanga, kuhudhuria mazishi ya Askofu Aloysius Balina.

Kwa muda mrefu sasa, ndani ya CCM kumekuwa na mitazamo tofauti kuhusu muundo wa uongozi ndani ya chama hicho.

Wapo wanaotaka nafasi ya mwenyekiti itenganishwe na urais ili kutoa nafasi kwa rais kusimamia mambo ya serikali na mwenyekiti abaki na mambo ya chama.

No comments:

Post a Comment