Waziri wa Nishati na Madini Mhe.
Profesa Sospeter Muhongo akipitia taarifa kuhusu mikataba
iliyokwishaingiwa na Serikali ya Utafutaji mafuta na gesi mara baada ya kuipokea
kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC), Bw. Michael Mwanda.
Na: Afisa
habari, Wizara
ya Nishati na Madini
Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imekabidhi rasmi kwa Mheshimiwa Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ripoti kuhusu mikataba
iliyokwishaingiwa na Serikali ya utafutaji mafuta na gesi asilia. Ripoti hiyo
ilikabidhiwa Ijumaa iliyopita, Novemba 30 mwaka huu ofisini kwa Waziri jijini
Dar es Salaam.
Ripoti hiyo iliandaliwa kufuatia
agizo la Mhe. Waziri kwa Bodi hiyo kuipitia mikataba yote 26 ya utafutaji mafuta
na gesi asilia. Lengo mahsusi lilikuwa ni kuhakikisha kwamba endapo kuna
mapungufu katika mikataba hiyo, mapungufu hayo yasijirudie tena katika mikataba
mipya ya baadaye, pamoja na kuwezesha Bodi hiyo kuelewa vizuri kazi iliyo mbele
yao.
Akipokea ripoti husika kutoka kwa
Mwenyekiti wa Bodi Bw. Michael Mwanda, Waziri Muhongo aliahidi kuisoma na
kuyafanyia kazi mapema mapendekezo yote. Aidha, aliipongeza Bodi hiyo kwa
kufanya kazi hiyo na kuwasilisha kwa wakati akisisitiza kuwa suala la kujali
muda ni moja ya mambo ya msingi anayoyasimamia ili kuwa na utekelezaji makini wa
majukumu mbalimbali hususan katika Wizara anayoiongoza.
Waziri Muhongo pia alisema ni vyema
kwa Wajumbe wa Bodi wakajifunza kwa haraka kutoka nchi zilizofanikiwa kutokana
na rasilimali za mafuta na gesi asili, kama Uholanzi, Oman, Malaysia na Norway.
Kwa upande mwingine alisema ni vyema
pia kujifunza kutoka nchi ambazo hazijafanikiwa katika kusimamia rasilimali
husika kama Nigeria ili kupata ufahamu wa makosa waliyofanya ambapo ufahamu huo
utawasaidia kuepuka makosa ambayo nchi hiyo ilifanya.
No comments:
Post a Comment