HALI si shwari kwenye wodi za wazazi katika hospitali karibu zote kubwa
nchini baada ya kubainika kuwa wagonjwa wanalala kati ya wawili na
watatu (maarufu kama mzungu wa nne), kwenye kitanda kimoja na wengine
sakafuni wakisubiri kujifungua.
Wakimama wakiwa wamelala zaidi ya mmoja kwenye kitanda katika hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam.Picha na Maktaba
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika baadhi ya hospitali za rufaa na
baadhi ya hospitali za mikoa, umebaini kuwa kama hali hiyo
haitashughulikiwa haraka, kuna hatari ya wazazi hao na vichanga vyao,
kuambukizana magonjwa.
Hospitali hizo ni Muhimbili, KCMC (Moshi), Bombo (Tanga), Hospitali za
Mikoa ya Morogoro, Dodoma, Mwananyamala, Temeke na Amana za Dar es
Salaam.
Hospitali zilizopo Dar es Salaam
Mgonjwa Zawadi Salehe aliyelazwa Wodi namba 38 Muhimbili, alisema siku
ya kwanza alilazwa kwenye kitanda kilichokuwa na mgonjwa mwingine na
baada ya kujifungua kwa upasuaji, alitakiwa kulala sakafuni ili kupisha
kitanda kitumiwe na wagonjwa wengine.
“Ukifika (wodini) unapelekwa kwenye kitanda ambacho tayari kina mgonjwa.
Inapofika siku ya Jumanne na Jumapili wanaletwa wagonjwa wengi zaidi
ambao wamepewa rufaa ya kuja hapa. Wakishaingia, sisi ambao tulikuwapo
tunaambiwa na wauguzi tulale chini ambako godoro moja wanalala watu
watatu na wanaokosa nafasi kwenye godoro wanatandika kanga zao na kulala
sakafuni.”
Ofisa Habari wa Hospitali hiyo, Aminieli Aligaesha alikiri kuwapo kwa
tatizo hilo na kueleza kuwa inatokana na uhaba wa nafasi wodini na siyo
vitanda. Alisema Muhimbili inapokea zaidi ya wagonjwa 70 kila wodi.
“Kila wodi ina vitanda 26. Wagonjwa wanapozidi huwezi kuwarudisha
nyumbani. Kutokana na ukosefu wa vitanda hulazimika kuwalaza chini
kwenye magodoro huku tiba ikiendelea.”
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Amana, Dk Meshack Shimwela alisema
kwamba wodi ya wazazi katika hospitali hiyo inapokea wagonjwa wengi,
lakini wengi wao hawana matatizo makubwa na walipaswa kwenda katika
vituo vya afya.
“Hii ni Hospitali ya Rufaa, tunapokea wagonjwa wenye matatizo makubwa tu
hivyo wagonjwa wanaojifungua kwa njia ya kawaida wanatakiwa waende
katika vituo vya afya vilivyopo katika maeneo yao, lakini utakuta kila
mgonjwa anakimbilia hapa ndiyo maana kuna huu msongamano wa mkubwa,”
alisema Dk Shimwela.
Katika Hospitali ya Mwananyamala, mgonjwa Elizabeth Mgimwa alisema:
“Kwenye wodi hii ya wazazi kinachoangaliwa ni hela, kama hauna huyo
mzazi atatukanwa na nesi na hata huduma muhimu hatapatiwa kwa wakati.”
Katibu wa Afya katika Hospitali hiyo, Edwin Bisakala alikiri kupata
taarifa za baadhi ya wagonjwa kutoa fedha kwa wauguzi lakini akaeleza
kuwa malipo hayo hutolewa kama asante. Hata hivyo alisema: “Tunataka
mama ambaye ameombwa fedha atoe ushirikiano kwenye uongozi wa hospitali
kwa kuwa haitakiwi mgonjwa kutoa asante. Hawa wauguzi wameajiriwa kwa
kazi hiyo.”
Hospitali ya Mkoa Dodoma
Wajawazito katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma wanalalamikia kile
wanachokiita manyanyaso kutoka kwa wauguzi wa wodi ya wazazi, huku
baadhi wakielezea kitendo cha kulazwa sakafuni kuwa ni kero.Akizungumzia
malalamiko hayo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Ezekiel Mpuya
alisema uongozi una tabia ya kuwaita wauguzi wanaolalamikiwa na wagonjwa
kisha kuwaonya.
“Kwa sasa malalamiko ya kunyanyaswa wajawazito kwa kiasi kikubwa
yamepungua baada ya uongozi kuanza kumshughulikia mtu mmoja baada ya
mwingine,” alisema.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment