SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kumtangaza Dk
Willibrod Slaa kuwa ndiye mgombea wa urais mwaka 2015 kwa tiketi ya
chama hicho, makada wa chama hicho wamegawanyika baadhi wakimponda na
wengine kumuunga mkono.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya makada wa chama hicho
walisema mwenyekiti wao amekosea kumtangaza mgombea kabla ya wakati,
huku wanaomuunga mkono wakisema hajakosea kwa sababu hatua hiyo
itasaidia kuondoa makundi ndani ya chama hicho.
Juzi, Mbowe akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Karatu mkoani
Arusha, alisema Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willibrod Slaa atapewa fursa
ya kuwania tena urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015, huku mwenyewe
akijiweka kando kuwania nafasi hiyo
Hata hivyo, Dk Slaa alipoulizwa iwapo ana nia ya kuwania nafasi hiyo
alihoji: “Kwani mwaka 2010 nilijitangaza mwenyewe,? Iwapo wanachama wa
Chadema watanipendekeza nitafikiria kufanya hivyo.”
Mwasisi wa chama hicho Edwin Mtei, Wajumbe wa Kamati Kuu; Profesa
Mwesiga Baregu na Dk Kitila Mkumbo, Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe,
Mwenyekiti wa Bavicha John Heche na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless
Lema walitoa maoni yanayopingana kuhusu kauli hiyo ya Mbowe.
Wanaounga mkono
“Ninaunga mkono Dk Slaa kuwania tena nafasi ya urais mwaka 2015.
Mwenyekiti amemtangaza baada ya kupata baraka ya vikao vya chama,”
alisema Mtei.
Ingawa Mtei hakuwa tayari kusema ni kikao gani kilichopitisha jina la Dk
Slaa kuwania nafasi hiyo, alisisitiza: “Kuna vikao vya Kamati Kuu
vimefanyika hivi karibuni, vinaweza kuwa vimefanya uamuzi huo.
Mwenyekiti hawezi kuzungumza jambo bila baraka za vikao vya chama.”
Hata hivyo, kauli hiyo ya Mtei inapingana na ile aliyoitoa Oktoba 6,
mwaka huu baada ya Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini
kutangaza kutogombea tena ubunge badala yake kusema anataka kugombea
urais katika uchaguzi wa mwaka 2015.
Mtei alisema hatua ya Zitto kutangaza kuwania urais mapema kungesababisha mzozo na mpasuko ndani ya chama hicho.
Mtei alisema amekuwa akimshauri Zitto mara kwa mara kuhusu hatua yake
hiyo akimtaka kuwaunganisha wana Chadema na siyo kuwagawa au kuwavuruga.
“Hakuna shida kuonyesha hisia, lakini unatengeneza mzozo mkubwa sana
ukitangaza sasa. Mimi nimeshamshauri sana Zitto, ahakikishe
anakiunganisha chama na siyo kukigawa wala kukivuruga.”
Alisema mbunge huyo kutangaza kutogombea tena ubunge na badala yake
kujipanga kuwania urais mwaka 2015 kumekuja mapema mno na kuonya kuwa
itaibua mzozo ndani ya Chadema.
Mtei ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Fedha na Gavana wa Benki Kuu enzi za
utawala wa Mwalimu Julius Nyerere, alisema kwamba wakati mwafaka
ukiwadia, Chadema kitaamua ni nani mwenye sifa za kugombea urais huku
akisema kina utaratibu wake wa kuwapata wagombea mbalimbali wa uongozi.
Hata hivyo, Zitto jana alikataa kuzungumzia suala hilo akisema:
“Nimesikia hata mimi kwenye vyombo vya habari ila sina cha kuzungumza
kuhusu hilo.”
Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), John Heche
alisema kauli hiyo Mbowe siyo yake binafsi, bali ni ya wananchi.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment