Mwenyekiti wa tume ya mabadiliko ya katiba Jaji warioba
Vurugu hizo ambazo chanzo chake ni siasa, zilitokana na wafuasi wa
baadhi ya vyama vya siasa, kuvamia mikutano iliyokuwa ikifanyika Unguja
na kusababisha hofu za kiusalama.
Baadhi ya maeneo ambayo wanasiasa hao walivamia mikutano ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba na kusababisha ivunjike ni Shehia za Magomeni na
Mpendae Mkoa wa Mjini Magharibi.Hii ni mara ya kwanza ghasia kuzuka
katika mikutano ya kukusanya maoni ya Katiba Mpya visiwani humo.
Tukio la kuchomana visu, lilitokea katika Shehia ya Mpendae baada ya
vurugu zilizosababishwa na vijana kuvamia mkutano uliokuwa ufanyike jana
mchana.
Vijana hao walianzisha ghasia hizo baada ya kutaka kuvunja utaratibu
uliokuwa umewekwa. Walitaka wakae mbele ya wengine waliokuwa
wametangulia katika mkutano huo.
Hatua hiyo ilipingwa na kuibua ghasia ziliozababisha watu kadhaa kujeruhiwa kwa visu.
Tukio jingine lililovuruga mkutano huo ni lile lililotokea katika Shehia
ya Magomeni, Jumatatu wiki hii baada ya kuibuka kwa mvutano baina ya
makundi mawili yenye misimamo tofauti juu ya mfumo wa Muungano; kuna
wanaopinga na wanaoukubali.
Misimamo hiyo imeelezwa kujikita katika misingi na sera za vyama vyao vya kisiasa.
Katika misimamo hiyo, CUF kinaamini katika Serikali ya Zanzibar na
Tanganyika kila moja kuwa na mamlaka kamili na Muungano uwe wa mkataba
wakati, CCM kinasimamia kwenye Serikali mbili; Muungano na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
Shehia ya Magomeni
Saa mbili kabla mkutano kuanza, watu wengi walifika Uwanja wa Mzalendo
ambako mkutano ulitakiwa kufanyika. Walijipanga kwa kuzingatia utaratibu
uliowekwa na Tume ambao ni aliyewahi kufika ndiye anayetangulia kutoa
maoni.
Hali hiyo ilisababisha wakazi wa Shehia hiyo waliokuwa wenyeji wa
mkutano, kukosa nafasi ambayo ingewawezesha kutoa maoni kwa mazungumzo
ya ana kwa ana.
Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni, Salmin Awadh Salmin, alisema hawakuwa
tayari kuwa wenyeji wa mkutano ambao hawatashiriki akisema waliokuwa
wamejipanga wote walifikishwa kituoni hapo kwa magari kwa lengo maalumu
la kuwakosesha wenyeji kutoa maoni yao, kwa kuwa inafahamika kuwa wengi
wao ni wana CCM.
Hoja hizo alizitoa kwa wajumbe wa Tume ambao pia hawakuridhishwa na hali
ya usalama katika eneo hilo kutokana na vurugu zilizokuwa zikifanywa na
wafuasi wa CCM na CUF.
“Kwa hali ilivyo, hatuwezi kupata utulivu utakaowezesha tufanye kazi kwa
ufanisi na kumaliza mkutano kwa amani bila fujo. Natangaza rasmi kuwa
leo hakuna mkutano,” Mwenyekiti wa Timu ya Tume hiyo inayokusanya maoni
visiwani hapa, Profesa Mwesiga Baregu.
Akizungumza baada ya kuvunjika kwa mkutano huo, Salmin alisema waliokuwa
wamefika kutoa maoni walikuwa wakitaka kunadi misimamo ya vyama vyao
akisema hiyo ni hali ya kihistoria inayowakabili wakazi visiwani humo.
Chanzo: Mwanachi
No comments:
Post a Comment