Pages


Photobucket

Thursday, December 13, 2012

Kagasheki Awashukia Vigogo Hifadhi Ngorongoro



Na: Mussa Juma, Arusha


WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki ametangaza kuwachukulia hatua za kinidhamu maofisa wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) waliokwamisha mradi wa kuwasaidia wafugaji wa hifadhi hiyo ulioahidiwa na Rais Jakaya Kikwete mwaka 2008.

Akizungumza na wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro na viongozi wa NCAA mara baada ya kuelezwa kuhusu kukwama kwa mradi huo, Balozi Kagasheki alisema lazima hatua kali zichukuliwe dhidi ya viongozi hao.

“Haiwezekani mradi ulioahidiwa mwaka 2008 leo hii ukwame, waliohusika kuukwamisha ni lazima wakae pembeni. Ninakwenda Dar es Salaam ila wakae wakijua kuwa barua zao zinakuja” alisema Kagasheki na kuongeza; “Kabla sijaondolewa wizarani kutokana na matatizo kama haya, mtaondoka ninyi kwanza.…, kukwama kwa mradi huu kutawafanya wananchi wamchukie Rais Kikwete na wanasiasa,” alisema Balozi Kagasheki.

Awali, Kaimu Mhifadhi wa Ngorongoro, Bruno Kawasange alisema mradi huo, ambao ulifikia hatua nzuri, umesitishwa na PPRA kwa maelezo kuwa taratibu hazikufuatwa katika kumtafuta mtaalamu mwelekezi.

Kawasange alisema awali, mtaalamu mwelekezi wa mradi huo, alipatikana nchini Ufaransa na tayari taratibu kadhaa zilianza ikiwa ni pamoja na kutolewa elimu kwa wafugaji kuhusu ufugaji wa kisasa.Hata hivyo, alisema katika hatua za mwisho, PPRA iliwataka kuanza upya taratibu za kumpata mtaalamu huyo, kwa maelezo kwamba taratibu za kisheria hazikufuatwa.

Akizungumza katika mkutano huo, aliyekuwa mmoja wa wasimamizi wa mradi huo, Justice Muumba alisema licha ya kutakiwa kuanza upya kwa taratibu za kumpata mtaalamu mwelekezi, mambo mengi ya msingi yalikuwa yamefikiwa.

Katika mradi huo, NCAA kwa kushirikiana na Baraza la Wafugaji, walikuwa waanzishe mradi mkubwa wa ufugaji wa kisasa na kiwanda cha kusindika nyama na maziwa ambacho kingesaidia kumaliza matatizo ya wakazi wa Ngorongoro hasa ya njaa.

Apokewa kwa mabango
Katika ziara yake hiyo, Waziri Kagasheki alipokewa kwa mabango na wakazi wa Tarafa ya Ngorongoro, yaliyokuwa yakieleza jinsi wanavyoshindwa kufanya shughuli za kilimo kutokana na kubanwa na NCAA.

Waziri Kagasheki, ambaye alikuwa ameambatana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, Mbunge wa Ngorongoro, Saning’o ole Telele na maofisa kadhaa wa Serikali, alikutana na mabango hayo alipofika katika Kijiji cha Mokilali Kata ya Ngorongoro.

Baadhi ya mabango hayo yalisomeka: “Njaa inatuuwa Ngorongoro,” “Tunalaani kauli ya Mkuu wa Mkoa Arusha kuwa Ngorongoro hakuna njaa,” “Tumechoka kuwa watumwa, tunataka uwiano Ngorongoro.”Katika mkutano huo, wananchi karibu wote, waliopewa nafasi ya kuzungumza walieleza tatizo kubwa la njaa ambalo linawakabili wakisema linasababisha watoto kufariki, kuugua magonjwa ya utapiamlo, wanaume kutelekeza familia zao na vijana kukimbilia mijini kufanya kazi za ulinzi.

Diwani wa Kata ya Enduleni, James Moringe alisema karibu kila kaya katika tarafa hiyo, sasa inakabiliwa na njaa kali na wananchi hawana chakula kutokana na kuzuiwa kwa shughuli za kilimo cha bustani bila kuwapo kwa utaratibu mwingine wa kuwapatia chakula.

“Kwanza tunakanusha taarifa ya Mkuu wa Mkoa wetu, Magesa Mulongo kuwa Ngorongoro hakuna njaa, sisi tunamshangaa sana mkuu wa mkoa na tunalaani kauli yake,” alisema Moringe.

No comments:

Post a Comment