Hatimaye mazishi ya mwanafunzi wa Udaktari aliyefariki jana jumamosi
katika hospitali ya Mount Elizabeth nchini Singapore yamefanyika huko
India. Juhudi za Madaktari kuokoa maisha yake zilishindikana kutokana na
kuathiriwa zaidi na unyama aliofanyiwa na kundi la wanaume sita
katikati ya mwezi huu.
Maombolezo nchini India
Mwili wa mwanamke huyo aliyekuwa na umri wa miaka ishirini na mitatu
tayari uliwasili nyumbani mapema leo asubuhi na kupokelewa kwa heshima
kubwa ambapo Waziri Mkuu wa India Manmohan Singh naye alikuwepo katika
mapokezi hayo.
Maelfu ya raia nchini India jana jumamosi waliendelea kukusanyika katika
mji mkuu New Delhi wakiwa na mishumaa kama ishara ya maombolezo ya kifo
cha mwanafunzi huyo aliyebakwa ndani ya basi katikati ya mwezi huu.
Kwa takribani majuma mawili kumekuwa na ghasia kubwa nchini humo
waandamanaji wakipinga unyanyasaji dhidi ya wanawake na kutaka adhabu ya
kifo itekelezwe kwa wanaotuhumiwa kwa tukio hilo.
Wanaume sita wanaoshikiliwa kwa kufanya unyama huo sasa wanakabiliwa na
kesi ya mauaji ya binti huyo aliyefariki jana asubuhi katika hospitali
ya Mount Elizabeth nchini Singapore ambako alipelekwa kwa matibabu
zaidi.
No comments:
Post a Comment