HOJA tatu za msingi zinatarajiwa kutumiwa na Jopo la Majaji watatu wa
Mahakama ya Rufani, kuamua rufaa ya kesi ya aliyekuwa mbunge wa Arusha
Mjini, Godbless Lema katika hukumu inayotarajiwa kusomwa leo jijini Dar
es Salaam.
Kati ya hoja 18 zilizowasilishwa na upande wa rufaa kupinga hukumu hiyo,
zipo hoja tatu ambazo zinaonekana za msingi katika hukumu ya leo
itakayotolewa na majaji waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo; Salum Massati,
Bernard Luanda na kiongozi wao, Nathalia Kimaro.
Lema alivuliwa ubunge Aprili 5, 2012 katika hukumu iliyotolewa na Jaji
Gabriel Rwakibalira, kutokana na kesi iliyofunguliwa na makada watatu wa
CCM; Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel, wakipinga ushindi wake
katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Kutokana na hukumu hiyo, Lema, kupitia kwa Wakili wake, Method
Kimomogoro alikata rufaa Mahakama ya Rufani, akiwasilisha hoja 18 za
kupinga hukumu hiyo.
Hoja ya kwanza ni kama mpigakura anaweza kufungua kesi mahakamani
kupinga matokeo ya uchaguzi kwa niaba ya mgombea husika aliyeshindwa
katika kinyang’anyiro cha uchaguzi.
Wakili Mkuu wa Serikali, Timon Vitalis alidai kuwa Mahakama Kuu Kanda ya
Arusha ilikosea kutengua ubunge wa Lema, kutokana na kesi
iliyofunguliwa na walalamikaji wanaodai kuwa ni wapigakura.
Wakili Vitalis, aliyemwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),
ambaye pia alikuwa upande wa Lema, alidai kuwa wajibu rufaa hawakuwa na
haki ya kufungua kesi kupinga ushindi wa mrufani (Lema) kwa kasoro
zilizotokea wakati wa kampeni.
Vitalis alidai kuwa, wajibu rufani hao hawakuwa wahusika katika mchakato
huo wa kampeni na hivyo hawakuwa na haki ya kupinga matokeo hayo
mahakamani.
Akifafanua zaidi, Wakili Vitalis alidai kuwa anayepaswa kufungua kesi
mahakamani kwa madai ya lugha ya matusi ni yule aliyetukanwa kwa kuwa
hayo ni maumivu ya mtu binafsi na kwamba hata anapokufa, madai yake nayo
hufa wala hayawezi kuendelezwa na mtu mwingine.
“Sasa iweje kwa mtu ambaye yuko hai, lakini watu wengine ndio waje mahakamani kufungua kesi? Alihoji Wakili Vitalis.
Hoja hiyo iliungwa mkono na mawakili wa mrufani, Method Kimomogoro na
mwenzake ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu
Lissu.
Wakili Kimomogoro alidai kuwa, Jaji alikosea kuamua kuwa mtu yeyote
aliyejiandikisha kupiga kura ana haki isiyo na mpaka ya kufungua kesi
kupinga matokeo.
Alidai kuwa, hoja yao ni kwamba mtu anakuwa na haki hiyo pale ambapo
haki yake imevunjwa au inaelekea kuvunjwa na si pale aliyeathirika na
ukiukwaji wa haki hiyo ni mtu mwingine.
Kwa upande wake, Lissu alidai kuwa mpigakura ana haki ya kupinga matokeo
mahakamani kwa madai kuwa haki zake pale ambapo madai yao yanaambatana
na haki zilizotajwa kwenye Katiba ambazo ni pamoja na haki ya kupiga
kura.
Majibu ya Warufaniwa
Akijibu hoja hiyo, Wakili wa warufaniwa, Alute Mughway alidai kuwa haki
hiyo inaelezwa katika kifungu cha 111 (1) (A) cha Sheria ya Uchaguzi
(2010) pamoja na Katiba na sheria nyingine za nchi na Kanuni za Maadili
ya Uchaguzi zinazokataza siasa za majitaka.
Uamuzi wa Mahakama kuhusu hoja hiyo ndiyo ama utahitimisha hukumu hiyo
bila kujadili na kuzitolea uamuzi hoja nyingine, ikiwa mahakama itaamua
kuanza na hoja hiyo, au utakaoruhusu kuendelea na mjadala na kisha
uamuzi wa hoja nyingine kutolewa.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment