Pages


Photobucket

Friday, December 28, 2012

Maelfu waandamana Mtwara kupinga gesi kwenda Dar es Salaam


Hizi ni Baadhi ya picha za maanadamano  yaliyofanyika Mtwara
 
 
Wakazi wa Mtwara wakiwa kwenye maandamano ya Kupinga Ujenzi wa Bomba la Gesi na wakiwa wamebeba mabango ili kufikisha ujumbe kwa serikali.

MAELFU ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara jana waliandamana wakipinga uamuzi wa Serikali kusafirisha gesi kwa njia ya bomba kutoka hapa kwenda Dar es Salaam.

Maandamano hayo ambayo yaliwashirikisha wananchi wa wilaya za mkoa huu zikiwamo Tandahimba na Newala, yalianzia katika Kijiji cha Mtawanya hadi Mtwara mjini kupitia barabara ya kwenda Msimbati eneo ambako gesi asilia inapatikana.

Waandamanaji hao waliotembea umbali wa kilomita sita, walitoa maazimio tisa mojawapo likihoji sababu za mitambo ya kuzalisha umeme kutojengwa Mtwara ambako ni jirani na inakochimbwa gesi hiyo.

Katika tamko hilo lenye kurasa mbili, waandamanaji hao wamesema Serikali haijaweka wazi namna gani wakazi wa Mtwara watanufaika na gesi hiyo, huku tayari Rais Jakaya Kikwete akiwa ameshazindua ujenzi wa bomba kwenda Dar es Salaam. Wametaka ujenzi huo usitishwe.

Pia wamesema uamuzi wa kupeleka gesi Dar es Salaam unapingana na tamko la Rais Kikwete alilolitoa kwenye ziara yake mkoani hapa mwaka 2009 kwamba ujiandae kuwa ukanda wa viwanda.

Aidha, wanataka vinu vya kuzalishia gesi vijengwe Mtwara kwa kuwa wanayo maeneo ya kutosha ya ujenzi huo tofauti na Dar es Salaam.

“Tunahitaji viwanda vikubwa vijengwe Mtwara ili kuleta ajira kwa wakazi wa Mtwara na mikoa ya jirani, tuna hofu kutokana na ilivyokuwa kwa wakazi wa Songongo (Lindi) kubaki maskini wakati gesi inazalishwa hapo, yasije yakatukuta sisi, hivyo ni lazima tusimamie rasilimali hii ili iweze kuleta maendeleo,” walisema katika azimio lao.

Wamesema pia kwamba Serikali haijaeleza athari zitakazopatikana kutokana na uchimbaji wa gesi katika eneo hilo na namna itakavyoweza kusaidia kuziondoa, huku wakitaka gharama za uunganishaji wa umeme wa nyumbani zisizidi Sh50,000 ili kila mwananchi aone ananufaika na gesi hiyo.

Waandamanaji hao wamesema gharama za mradi huo wa kusafirisha gesi hadi Dar sa Salaam ni kubwa, hivyo wakashauri Serikali ichimbe gesi ya Dar es Salaam katika kisima namba 7 ili kuepuka hasara.

Katika azimio lao la mwisho, wamemwomba Rais Kikwete kumwondoa madarakani Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Joseph Simbakalia kwa madai kwamba amewakashifu kutokana na madai yao ya kupinga gesi kwenda Dar es Salaam.

Ilielezwa kuwa, awali Simbakalia aliombwa kuwa mgeni rasmi katika maandamano hayo, lakini alikataa na badala yake yalipokewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vyama vya Siasa, Hussein Mussa Amiri.

Desemba 21, mwaka huu katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mtwara (RCC), kilichoketi kwenye Ukumbi wa Boma, Simbakalia alisema hawezi kushiriki katika maandamano hayo.
Maandamano hayo yaliratibiwa na vyama vya siasa vya Chadema, NCCR-Mageuzi, Sau, TLP, APPT Maendeleo, ADC, UDP na DP, yakiwa na kaulimbiu ya ‘gesi kwanza vyama baadaye, hapa hakitoki kitu.’
Kutokana na maandamano hayo, Soko Kuu la Mtwara lilifungwa kwa muda kutoa fursa kwa wafanyabiashara hao kushiriki na barabara kadhaa zilifungwa kwa muda.

Mbali ya watu kujitokeza kwa wingi, pia walibeba mabango yenye ujumbe mbalimbali.
“Bandari Bagamoyo, Viwanda Bagamoyo, Gesi Bagamoyo, Mtwara wapuuzi?.... Gesi haitoki hata kama hatujasoma.... Gesi kwanza vyama baadaye, hapa hakitoki kitu.... Kusini tumedharauliwa vya kutosha sasa basi.”

Akisoma tamko la vyama hivyo, Katibu wa umoja huo, Seleman Litope alisema kwa muda mrefu Kusini imekuwa ikiondolewa fursa mbalimbali za maendeleo.

Alitoa mfano wa kung’olewa kwa reli, ukosefu wa usimamizi mzuri wa zao la korosho, ukosefu wa miundombinu ya barabara, kuondolewa kwa Mradi wa Maendeleo ya Ukanda wa Mtwara (Mtwara coridor) na hilo la gesi.

Alisema hali hiyo imesababisha mikoa ya Kusini kuwa nyuma kimaendeleo na kwamba umoja wao unalenga kuhakikisha rasilimali yao hiyo haitoki kwenda kokote kabla ya kuwanufaisha.

MWANANCHI

No comments:

Post a Comment