ADAI HAKUWA NA MAMLAKA YA KUGEUZA TAARIFA
YA NGWILIZi
MBUNGE wa
Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), amewasilisha barua ya
malalamiko kwenye ofisi ya Bunge, akipinga aumuzi wa Spika Anne Makinda,
kuhusu tuhuma za baadhi ya wabunge kujihusiha na vitendo vya rushwa.
Katika barua
yake hiyo ya Novemba 14 mwaka huu, Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, anasema kuwa Spika hakuwa na mamlaka ya
kugeuza taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuwa
‘uamuzi wa Spika.’
Novemba 9
mwaka huu, Spika Makinda alisoma taarifa ya ripoti hiyo iliyokuwa chini
ya ueneyekiti wa Brigedia mstaafu Hassan Ngwilizi, akisema imebainika
kuwa hakuna mbunge aliyetiwa hatiani kwa tuhuma hizo.
Badala yake
Makindi alitoa onyo kali kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini,
Eliakim Maswi akisema kuwa aliibua tuhuma za uongo kwa baadhi ya
wabunge na wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini.
Makinda pia
aliwapa kalipio kali wabunge watano pamoja na Waziri wa Nishati na
Madini, Prof. Sospeter Muhongo akidai walishindwa kuthibitisha madai ya
tuhuma zao kwa baadhi ya wenzao mbele ya kamati hiyo.
Ni katika
uamuzi huo, Lissu amewasilisha malalamiko yake akipinga uamuzi wote wa
Spika Makinda akitoa sababu kuu tatu za kufanya hivyo.
Lissu
alifafanua kuwa kwa mujibu wa uamuzi unaolalamikiwa, mamlaka ya Spika
kutoa uamuzi huo yanatokana na masharti ya kanuni za 5(1) na 72(1) za
Kanuni za Kudumu za Bunge, 2007.
Aidha,
mamlaka hayo yanadaiwa kutokana na masharti ya vifungu vya 12(1), (2) na
25(c) vya Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge, Sura ya 296 ya
Sheria za Tanzania.
“Kwa heshima
zote anazostahili, ni hoja yangu kwamba Mheshimiwa Spika hakuwa na
mamlaka ya kutoa uamuzi unaolalamikiwa kwa mujibu wa Sheria ya Kinga za
Bunge na Kanuni za Kudumu,” alisema.
Alisema kuwa
kanuni ya 5(1) ya Kanuni za Kudumu haimpi Spika mamlaka ya kutoa uamuzi
wa masuala yanayohusu kinga, madaraka na haki za Bunge bali inampa
Spika mamlaka ya ziada ya kutekeleza majukumu yake “pale ambapo Kanuni
hazikutoa mwongozo.”
Lissu
alifafanua kuwa mara baada ya Kamati kukamilisha majukumu yake,
ilitakiwa kwa mujibu wa kanuni ya 114 (16) ya Kanuni za Kudumu
kuwasilisha taarifa yake bungeni ili ishughulikiwe kwa kufuata mpangilio
wa shughuli za Bunge.
Aidha, chini ya kanuni ya 114(17), Spika alitakiwa aweke utaratibu wa kujadili taarifa hiyo bungeni.
“Kanuni ya
72(1) ya Kanuni za Kudumu nayo haimpi Spika mamlaka ya kugeuza Taarifa
ya Kamati kuwa uamuzi wa Spika. Kanuni hiyo ipo katika Sehemu ya Sita ya
Kanuni za Kudumu inayohusu ‘amani na utulivu Bungeni’ na inampa Spika
wajibu wa kuhakikisha kuwa utaratibu bora unafuatwa Bungeni.
“Uamuzi wa
Spika kuhusu mambo ya utaratibu, kwa mujibu wa kanuni hii ni wa mwisho.
Hoja yangu ya msingi hapa ni kwamba kanuni ya 72(1) inatumika pale tu
ambapo kuna uvunjifu wa ‘amani na utulivu Bungeni’ na Spika anatakiwa
kutumia mamlaka yake kuhakikisha amani na utulivu vinarejea na
‘utaratibu bora unafuatwa Bungeni,” alisema.
Kwamba Spika
hana mamlaka ya kutoa uamuzi unaolalamikiwa kwa mujibu wa Sheria ya
Kinga za Bunge vile vile. Kifungu cha 12(1) cha Sheria hiyo kinalipa
Bunge mamlaka na uwezo – kama itakuwa lazima.
Hivyo
litachunguza, kutoa hukumu na kuamua juu ya kutendwa kwa tendo, jambo au
kitu chochote, ambacho sio kosa chini ya Sheria hii, ambacho ni
ukiukwaji wa haki za Bunge.
“Kutokana na
hoja zangu za ufafanuzi wa sababu ya kwanza ya rufaa hii, ni wazi
kwamba uamuzi unaolalamikiwa sio Taarifa ya Kamati iliyochunguza tuhuma
za rushwa dhidi ya wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini.”
Lissu
alisema kuwa kwa sababu kanuni ya 120 ya Kanuni za Kudumu imeweka
masharti ya ‘Muundo wa Taarifa za Kamati.’ Kwa mujibu wa kanuni hiyo,
Taarifa ya Kamati inatakiwa iwe na sehemu tatu.
“Sehemu ya
kwanza ni ya utangulizi, Sehemu ya pili ya Taarifa ya Kamati inatakiwa
itoe maelekezo kamili kuhusu jambo au mambo yote yaliyofanyiwa uchunguzi
na Kamati wakati sehemu ya tatu inatakiwa itoe maoni na mapendekezo ya
Kamati ya Bunge,” alisema.
Aliongeza
kuwa uamuzi unaolalamikiwa licha ya kuwa na sehemu hizo tatu lakini ni
maoni tu ya Spika juu ya Taarifa ya Kamati na wala sio Taarifa ya Kamati
yenyewe.
“Kuna kila
haki na sababu ya kuhoji kama kweli yaliyoko kwenye uamuzi
unaolalamikiwa ndiyo kweli yaliyomo kwenye Taarifa ya Kamati na, kama ni
hivyo, kwa nini Taarifa ya Kamati haikutolewa Bungeni ili ijieleze
yenyewe kama inavyotakiwa na Kanuni za Kudumu? Alihoji.
Katika barua hiyo ambayo Tanzania Daima lina nakala yake, Lissu anadai kuwa Spika alitoa adhabu kinyume cha kanuni za Bunge.
“Katika
uamuzi unaolalamikiwa Spika alidai kwamba Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati na Madini, Eliakim Maswi, ametenda kosa la kuvunja haki za
Bunge, na anastahili adhabu”
Baada ya
kumpata Katibu Mkuu Maswi na ‘hatia’ hiyo, Spika alimpa ‘adhabu’ ya onyo
kali na kumtaka asirudie tena kosa hilo la kuzua tuhuma za uongo dhidi
ya Bunge na Wabunge.” Alisema.
Lissu
aligusia pia onyo walilopewa wabunge watano akiwemo yeye huku waziri
Muhongo akitakiwa kuwa mwangalifu na kusema kuwa ni hoja yake kwamba
‘hatia’ ambazo Spika aliwakuta nazo watajwa adhabu alizowapa ‘wenye
hatia’ hao ziko kinyume cha Kanuni za Kudumu.
Alisema kuwa
adhabu iliyotolewa kwa Maswi, ni kwamba Spika hana mamlaka yoyote kwa
mujibu wa Kanuni za Kudumu ya kuchukua hatua au kutoa adhabu kwa mtu
yeyote asiyekuwa Mbunge kwa kosa lolote alilofanya nje ya Bunge.
Kwamba hatua
pekee anazoweza kuchukua Spika dhidi ya ‘wageni bungeni’ ni kuwaondoa
ndani ya ukumbi wa mikutano wa Bunge kwa mujibu wa kanuni ya 136(3) na
138(1) ya Kanuni za Kudumu.
“Maswi
aliitwa kama shahidi wa Kamati ya Maadili. Hakuitwa kama mtuhumiwa wa
kosa lolote linalohusu haki au kinga za Bunge. Kwa msingi huo Maswi ana
kinga chini ya kifungu cha 18(1) cha Sheria hiyo,” alifafanua.
Lissu
alisema kuwa uamuzi unaolalamikiwa hauonyeshi mahali popote kwamba
ushahidi alioutoa Maswi kwenye Kamati ya Maadili ulikuwa wa uongo kitu
ambacho kingekuwa ni kosa la jinai kwa mujibu wa kifungu cha 21 cha
Sheria ya Kinga za Bunge.
Kwamba
hakuna kosa lolote chini ya Sheria ya Kinga za Bunge linaloitwa kuzua
tuhuma za uongo dhidi ya Bunge na wabunge! Badala yake, Sheria hiyo,
chini ya kifungu chake cha 23, inatambua kosa la jinai la kutoa nyaraka
za uongo kwa Bunge au Kamati yake.
CHADEMA BLOG
No comments:
Post a Comment