WAKILI wa Serikali Mkuu Timon amedai kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha
ilikosea kutengua ubunge wa aliyekuwa Mbunge wa Arusha mjini, Godbless
Lema, kwa madai ya kutumia lugha za matusi kwa kuwa Bunge limeruhusu
wanasiasa kutukanana kwenye kampeni.
Wakili
Vitalis alitoa madai hayo jana, wakati wa usikilizwaji wa rufaa ya
Lema, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema),katika Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam.
Wakati wakili huyo wa serikali akitoa madai hayo, Wakili wa wajibu
rufaa, ambao walishinda katika kesi ya msingi, Alute Mughway, naye
alidai kuwa Mahakama Kuu, Arusha ilikosea katika uamuzi wake, pamoja na
mambo mengine, kwa kukataa baadhi ya madai yao.
Lema alivuliwa ubunge April 5, 2012, katika hukumu iliyotolewa na Jaji
Gabriel Rwakibalia, kufuatia kesi iliuyofunguliwa makada watatu wa Chama
cha Mapinduzi (CCM), Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel,
wakipinga ushindi wake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Lema kupitia kwa Wakili wake Method Kimomogoro alikata rufaa Mahakama ya
Rufani, lakini Novemba 8, 2012 mahakama ilitupilia mbali rufaa hiyo
baada ya kuini kuwepo kwa dosari za kisheria, kutokana na pingamizi
lililowekwa na upande wa wajibu rufaa.
Hata hivyo mahakama hiyo ilimpa nafasi nyingine ya kukata rufaa tena
baada ya kumpa siku 14 kufanya marekebisho ya dosari hizo za kisheria na
kuiwasilisha mahakamani ndani ya muda huo, amri ambayo aliitekeleaza.
Wakati Lema akikata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu kumvua ubunge,
wajibu rufaa nao walikata rufaa (Cross Appeal) kupinga uamuzi wa
mahakama hiyo, huku wakibainisha hoja nne.
Katika hoja ya kwanza hadi ya tatu walidai kuwa Jaji alikosea katika
hukumu yake kwa kuchanganya vituo vilivyotolewa ushahidi na mashahidi
wanne na hatimaye akakataa ushahidi wapo, pamoja na tarehe za ratiba ya
kampeni ya CCM nay a Chadema.
Hoja ya nne walidai kuwa Jaji alikosea kwa kuamua kuwa hata kama Lema
kwenye kampeni zake alidai kuwa Dk. Buriani ni mkazi wa Zanzibar
hatafaa, wakidai kuwa ukazi si sifa ya kuchaguliwa kuwa mbunge.
Hatimaye rufaa hizo zilisikilizwa jana na jopo la Majaji watatu wa
Mahakama ya Rufani, lililoundwa na Jaji Salum Massati, Jaji Bernard
Luanda, chini ya uongozi wa Jaji Nathalia Kimaro.
Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, mawakili wawili ambao ni ndugu,
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lisu na kaka yake Mghway, walipambana
vikali kwa hoja za kisheria.
Lisu, Kada wa Chadema ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, alikuwa akimtetea Lema mrufani (Lema), akisaidiana na Wakili
Method Kimomogolo, huku Mughway akiwatetea wajibu rufani ambao ni makada
wa CCM.
Mwananchi
Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment