MZOZO wa kidiplomasia alioibua Rais wa
Rwanda, Paul Kagame kwa Rais Jakaya Kikwete, sasa unaonekana kuchukua
mwelekeo mpya, baada ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC),
kumuonya kiongozi huyo kuacha mara moja fikra zozote mbaya dhidi ya
Tanzania, MTANZANIA Jumatano limedokezwa.
Habari za uhakika na za kuaminika kutoka
miongoni mwa viongozi wa juu wa SADC na maofisa wa Serikali, waliokuwa
katika ujumbe wa Rais Jakaya Kikwete aliyekuwa akihudhuria Mkutano wa
viongozi wa Maziwa Makuu huko Uganda hivi karibuni, zinaeleza kuwa
tayari Jumuiya hiyo imekwisha mpatia ujumbe huo mmoja wa mawaziri
aliyekuwa ameandamana na Kagame muda mfupi baada ya kikao chake na
Kikwete.
Taarifa ambazo MTANZANIA Jumatano
imezinasa, zinaeleza kuwa, kiongozi mmoja wa juu wa Msumbiji ambaye
alikuwa pia Uganda, alikaririwa akimueleza Waziri huyo wa Kagame kuacha
kabisa fikra za kuishambulia Tanzania, kwa sababu ya uamuzi wake wa
kupeleka vikosi vyake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC.
“Uamuzi wa Tanzania na Afrika Kusini
kupeleka majeshi DRC, ni msimamo wa pamoja wa SADC. Vitisho vyovyote
dhidi ya Tanzania au uvamizi wa kijeshi, utachukuliwa ni uvamizi dhidi
ya SADC, hivyo tutakuwa tayari kuingia vitani kupigana upande wa
Tanzania,” alikaririwa akisema ofisa huyo wa juu wa Msumbiji.
Inaelezwa kuwa, SADC imetoa msimamo huo
baada ya kubaini kuwa hasira ya sasa ya Kagame dhidi ya Rais Kikwete,
msingi wake unatokana na hatua ya Tanzania kupeleka vikosi vyake nchini
Kongo kwenda kupambana na vikundi vya waasi vikiwemo vile vinavyodaiwa
kuwa na ushirika na majeshi ya Rwanda.
Taarifa hizi zinathibitishwa na habari
ambazo gazeti hili ilizinasa jana kupitia gazeti la The Namibian la
nchini Namibia, ambalo liliandika kuwa Jeshi la nchi hiyo (NDF), ambalo
linaunda kikosi maalumu cha SADC, lilikuwa limeanza kushiriki mazoezi
huko Jangwani karibu na Walvis Bay. Mazoezi hayo yatadumu hadi Oktoba 15
mwaka huu.
Inaelezwa kuwa wakati mazoezi hayo
yakiendelea, Mkuu wa majeshi ya Namibia (NDF), Luteni Jenerali, Epafras
Ndaitwah aliwakumbusha washiriki hao kuwa kwa sasa wanachama wenzao kama
Wanajeshi wa Tanzania na Namibia, wanapambana na maadui wa amani Kongo
na kwamba lazima wajiandae kwa hali yoyote ambayo haitabiriki.
Hatua hiyo ya sasa ya SADC, na sifa
ambazo imepata kummwagia Rais Kikwete kwa namna alivyosimamia mizozo
wakati akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi, inaonyesha wazi jinsi
Jumuiya hiyo ilivyotayari kuwa upande wa kiongozi huyo.
Kutokana na hilo, baadhi ya wachambuzi
na wafuatiliaji wa mambo wanasema kuwa si ajabu basi Kagame na Serikali
yake wakawa wanafahamu msimamo huo wa SADC, ambao haujawekwa hadharani
hasa kwa kuzingatia uamuzi wake wa kuungana na Uganda na Kenya katika
usharika wao wa hivi karibuni.
Pia hatua ya nchi yake kusaini mkataba
wa kiusalama na nchi nyingine tano wa kusaidiana kijeshi endapo mmoja
wao atavamiwa na nchi nyingine, imeelezwa kuwa na mwelekeo huo huo wa
Kagame kuanza kujihami.
Nchi ambazo zimeingia mkataba huo na Rwanda ni pamoja na Ethiopia, Kenya, Uganda na Sudan Kusini.
Hata hivyo wachambuzi na wafuatiliaji wa
mambo, wamekosoa muungano huo wa kusaidiana kijeshi na Rwanda, wakidai
kuwa ni wa mashaka ukilinganisha na ule unaounda SADC ambao unajengwa na
matendo ya kihistoria.
Wameitolea mfano Ethiopia, kwamba ni
rahisi kuasi kutokana na mfumo wake wa kijeshi unaoongozwa kwa mkono wa
chuma, huku wanajeshi wake wakiwa katika hali mbaya ya kiuchumi.
Wameulinganisha mfano huo na nchi moja
tu ya Zimbambwe ambayo inaunda SADC kwamba, pamoja na matatizo yote ya
migogoro ya kisiasa na kidiplomasia inayoyakabili, lakini jeshi lake
lipo imara na linatunzwa vizuri.
Wakati wadadisi na wachambuzi wa mambo
wakiwa na mtizamo huo, hatua ya sasa ya SADC imekuja wakati ambapo
tayari Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma aliwahi kuionya Rwanda akisema
kuwa endapo nchi hiyo itajaribu kuigusa Tanzania, atakuwa tayari hata
peke yake kupeleka jeshi lake kupambana nchini humo.
Nje ya SADC, nchi zinazounda Jumuiya
hiyo kama Afrika Kusini, Msumbiji, Zimbabwe, Namibia na Angola zinaguswa
moja kwa moja na hisia za Tanzania, kutokana na historia yake ya
kushiriki kwenye ukombozi na uhuru wa nchi hizo.
Kutokana na hilo, wachambuzi hao
wanasema kuwa si rahisi kwa wao kukaa kando pale watakapoona maslahi ya
Tanzania yanachezewa, hasa linapokuja suala la kuichokoza.
Taarifa hizo za SADC zimekuja ikiwa ni
siku chache baada ya Rais wa Marekani, Barack Obama, kuinyooshea kidole
cha lawama Rwanda, kitendo hicho kinaonekana kuungwa mkono kwa kasi na
makundi mengine ya kimataifa.
Kagame ambaye kwa miaka mingi amekuwa
kiongozi kipenzi cha mataifa mengi tangu alipofanikiwa kumaliza mapigano
yaliyosababisha mauaji ya halaiki nchini kwake mwaka 1994, katika siku
za hivi karibuni taswira yake inaonekana kubadilika na kuchukua mwelekeo
wa uadui zaidi kuliko urafiki.
Hilo linatokana na kile kinachodaiwa
kuwa Serikali yake imekuwa ikihusika kuwasaidia waasi wa kundi la M23,
wanaoendesha mapambano dhidi ya majeshi ya Serikali ya Kongo, jambo
linalopingwa na Jumuiya ya Kimataifa pia wanatuhumiwa kwa ubakaji na
mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.
Tuhuma hizo ndizo ambazo zinamuweka Rais
Kagame katika hatari na wingu la mashaka kwa sasa, hasa baada ya
uhusiano wake na Tanzania kupita katika wakati mgumu kutokana na kuingia
kwenye mgogoro na Rais Kikwete ambaye alimshauri kukaa meza moja ya
mazungumzo na waasi wa FDLR.
No comments:
Post a Comment