Serikali
imesisitiza kuanza rasmi ujenzi wa Bandari ya Mwambani katika kipindi
cha miezi mitatu ijayo hatua ambayo itaenda sambamba na uunganishwaji wa
reli kutoka Tanga-Arusha mpaka Musoma. Hayo
yalibainishwa jana na Waziri wa Uchukuzi Dk.Harrison Mwakyembe wakati
wa kikao cha wadau wa sekta ya uchukuzi mkoa wa Tanga kilichofanyika
jijini hapa. Dk.Mwakyembe
alisema kimsingi serikali imeshakamilisha zoezi la ulipaji fidia katika
eneo hilo ambapo zaidi ya shilingi bilioni 6 zililipwa kwa wananchi ili
kupisha ujenzi wa Bandari hiyo na kwamba makampuni 22 yamejitokeza kwa
ajili ya uwekezaji kwenye eneo hilo.
“Upembuzi
yakinifu ulishafanyika na tafiti mbalimbali zilishafanyika kwa ajili ya
kuangalia mahusiana ya bandari na reli sasa kilichobaki ni kuanza
ujenzi na na upembuzi yakinifu na kwamba tayari makampuni 22 na 12
yamekuwa short listed,”alisema.
Hata hivyo, aliutaka uongozi wa mkoa wa Tanga kuhakikisha unatumia fursa
ya Jukwaa la uwekezaji Kanda ya Kaskazini linalitarajiwa kufanyika
Septemba 26 na 27 mwaka huu katika kufungua fursa za uwekezaji kwenye
sekta mbalimbali ikiwemo miundo mbinu ya reli na Anga.
Aidha aliiagiza Kampuni hodhi ya Rasilimali za Reli( RAHCO) kufanya
ukarabati wa njia ya reli katika eneo la Mombo-Mkomazi mpaka Taveta
ilikurahisisha usafairishaji wa mizigo unaofanyika katika njia hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Ushirika wa Kampuni hodhi ya
Rasilimali za Reli( RAHCO) Mbuttolwe Kabeta alisema kuwa mpango wa
ujenzi wa Reli kutoka Mwambani-Arusha mpaka Musoma upo katika mkakati wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) na kwamba tafiti mbalimbali
zilishafanyika kwa ajili ya mchakato huo.
Kabeta alisema kwa sasa Washauri elekezi kwa ajili ya usanifu,utafuti na
upembuzi yakinifu wameshapatikana kutoka nchini Ujerumani na kwamba
shilingi bilioni 5.2 zimetengwa kwa ajili ya usanifu na utafiti na
shilingi bilioni 4.9 zimetengwa kwa ajili ya kulipa fidia.
“Mradi wote kwa ajili ya shughuli mbalimbali unatarajiwa kutumia zaidi
ya shilingi bilioni 15.5 na kwa upande wa fidia mpaka sasa bilioni 4.6
zimeshalipwa hivyo tayari tumeanza mchakato wa utekelezaji wa mradi
huo”,alisisitiza Mkurugenzi huyo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment