Wakati
vyombo vya sheria vikiendelea kupambana na biashara ya dawa za kulevya
nchini, wasafirishaji hao kila siku wanaendelea kuwa wabunifu na kubuni
mbinu mpya na za kutisha za kusafirisha dawa hizo kutoka eneo moja hadi
lingine. Imebainika
kuwa miongoni mwa mbinu mpya wanazotumia ni kusafirisha dawa hizo kwa
kutumia ndege za mizigo ambapo huweza kuweka dawa za kulevya kwenye
mdoli, jarida, makopo ya maziwa ya watoto, vinyago vya kimakonde na
kuutuma kama kifurushi kwenda sehemu nyingine.
Pia,
wasafirishaji hao kwa sasa wanaweza kuvaa kama watawa (masista na
mapadre) na kujifanya wameshika rozari zao wakisali na kumbe wamehifadhi
dawa hizo ndani ya mavazi yao makubwa.
Pia,
imebainika kuwa siku hizi si lazima kusafirisha dawa za kulevya zilizo
tayari bali kemikali zinazotumika kutengeneza dawa za kulevya(kwa mfano
amphetamine inayoweza kutengenezwa maabara), husafirishwa na baada ya
kufika kemikali huchanganywa katika maabara za siri na dawa za kulevya
huanza kusambazwa mitaani.
Kamishna
Mkuu wa Polisi Kitengo cha Dawa za Kulevya, Alfred Nzowa alisema
wasafirishaji hao wanabuni mbinu mpya kila kukicha lakini alitaja mbinu
kuu ya kusafirisha mzigo mkubwa ni kwa njia ya meli au ndege za kukodi,
za abiria au binafsi kupeleka mzigo kutoka nchi moja hadi nyingine.
“Dawa nyingi
zinazosambazwa hapa zinakuja kwa njia ya meli. Zinapofika kwenye mipaka
ya bahari ya nchi za Afrika Mashariki kama Mombasa na Dar es Salaam
hupakuliwa na kuwekwa katika boti ndogo ndogo ziendazo kwa kasi na
kusambazwa,” alisema Kamishna Nzowa.
Kwa mfano,
ripoti ya mwaka 2013 ya Umoja wa Mataifa kitengo cha Uhalifu na Dawa za
Kulevya (UNODC) inaeleza kuwa kwa sasa njia inayotumika kupitisha dawa
za kulevya kufika Tanzania ni maeneo ya visiwani hasa Tanga na Zanzibar,
ambapo wasafirishaji hutumia boti binafsi ndogo. Mzigo unaposhushwa
hapa hupelekwa kama mizigo midogo midogo Dar es Salaam.
Nzowa
alisema mbinu nyingine iliyobuniwa na inayotumiwa na wafanyabiashara
wakubwa wa dawa za kulevya ni kusafirisha kwa kutumia ndege ndogo
binafsi, ambazo huweza kupita bila kukaguliwa.
Nzowa
alisema wasafirishaji hao wanaendelea kubuni mbinu nyingi kila siku ili
kuwazidi ujanja wakaguzi walio katika viwanja vya ndege na katika
mipaka, ambapo kwa sasa wasafirishaji wadogo wanaweza kuzificha katika
soli za viatu, sehemu za siri au katika matiti.
“Tuliwahi
kumkamata msichana mmoja wa Kifilipino ambaye kwa wakati mmoja alitumia
mbinu tatu kuficha dawa aina ya heroin. Aliweka gramu 400 katika viatu,
ambapo gramu 200 kiatu kimoja na gramu 200 katika kiatu cha kushoto.
Alificha kiasi kingine kwenye matiti na kiasi kingine sehemu za siri,”
alisema Nzowa.
Nzowa
alisema wasafirishaji hao wanaendelea kubuni njia mpya kila siku, ambapo
kwa sasa wamejikita zaidi kusafirisha kwa njia ya meli na ndege ili
kuweza kusafirisha kiasi kikubwa bila kugundulika.
“Wale
wasafirishaji wa ndani ya nchi wanatumia njia kama hizo za kumeza,
lakini wale manguli wanatumia meli za kukodi na ndege binafsi. Wanaweza
kusafirisha hata kilo 800 kwa wakati mmoja,” alisema Nzowa.
Msemaji wa
Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini Florence Mlay, alisema
wasafirishaji hao kwa sasa wanatumia meli binafsi kusafirisha dawa hizo
na baada ya kufika Tanzania zinashushwa katika bandari ndogo ndogo
ikiwamo Oysterbay.
Mlay alisema
kutokana na watuhumiwa wanaokamatwa Tume hiyo imegundua mbinu nzito
zinazotumika kusafirisha dawa za kulevya, kwa mfano kuweka dawa za
kulevya katika chupa za poda, biblia au majani ya chai.
“Wanaweka
poda, katikati unga, kisha poda juu, ni vigumu kubainika. Lakini wengine
wanatumia ma ‘hotpot’ ya vyakula kuzisindika dawa hizo” alisema Mlay.
Tume hiyo
imegundua mbinu nyingine kama ya kutumia biblia ambapo wanachana
karatasi katikati ya biblia kisha wanazifunga dawa kwa utaalamu mkubwa
kiasi cha ‘scanner’ kutoweza kuzibaini.
Karatasi maalumu
Mlay alisema
wasafirishaji wanatumia mbinu ya kuifunga mizigo hiyo kwa kutumia
karatasi maalumu, ambayo huzuia mashine ya kukagulia mizigo kubaini
utofauti wa mzigo huo na dawa za kulevya.
Kwa mfano bangi huweza kufungwa katika pakiti za majani ya chai na kufungwa kwa karatasi hiyo bila ‘scanner’ kugundua.
Chanzo
kimoja cha habari ambacho kiliwahi kuwa mfanyabiashara mkubwa wa dawa za
kulevya na mtumiaji, alizungumza na Mwananchi na kusema kuwa njia
nyingine ya kushangaza inayotumiwa na wasafirishaji hao ni kuwatumia
watoto wadogo ambao bila kufahamu hubebeshwa dawa hizo na kupita uwanja
wa ndege au mipakani bila kukaguliwa.
“Dawa
zinafungwa vizuri, zinawekwa katika begi la mgongoni la mtoto, kisha
dawa zinapuliziwa marashi ili kuficha harufu. Si rahisi watoto kuhisiwa
kuwa wamebeba dawa hizo,” kilisema chanzo chetu.
Alieleza
mbinu nyingine kuwa wanaposafirisha dawa hizo kwa njia ya ndege za
mizigo huweza kufunga boksi lenye dawa hizo kisha nje kuandika ni
chakula cha mbwa, vitabu, matunda au mboga za majani na kumbe ndani kuna
dawa hizo. Imebainika kuwa wakati mwingine wasafirishaji huweza
kushonea dawa za kulevya katika ngozi ya mnyama, kisha kuificha na mbwa
wa uwanja wa ndege wasiweza kubaini.
Chanzo hicho
kilitaja mbinu kama kuficha dawa katika soli za viatu, katika chupa za
maziwa ya watoto, au kuzisafirisha kwa kutumia mtu ambaye hajui
alichobeba ni nini lakini watumaji wanakuwa wameufunga kwa ujanja.
Wasafirishaji
hao inaelezwa kuwa wakati mwingine wanatumia magamba ya konono wa
baharini kusweka dawa hizo, kisha huziba kwa gundi na kuweka katika
mizigo yao na kuipitisha mipakani.
Ripoti ya
UNODC inaeleza kuwa kwa mwaka 2012 pekee, Watanzania zaidi ya 400
walikamatwa kwa kujaribu kusafirisha kilo 260 za heroin na kilo 151 za
cocaine.
Hivi
karibuni watanzania wawili walikamatwa nchini Ethiopia wakisafirisha
dawa za kulevya huku meli ya Tanzania ya Mv Gold Star ilikamatwa na tani
30 za bangi.
Pia Julai
mwaka huu wasichana wawili wa kitanzania walikamatwa uwanja wa ndege wa
OR Tambo wakiwa na mzigo mkubwa wa dawa za kulevya aina ya
methamphetamine (Tik).
No comments:
Post a Comment