Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph
Mbilinyi ‘Sugu’ amesema tukio la kupigwa ngumi na askari ndani ya Ukumbi
wa Bunge lilisababishwa na amri ya Naibu Spika, Job Ndugai na wala siyo
askari.
Aidha Sugu alisema ilikuwa vigumu
kuvumilia konde alilopigwa na askari wakati akitolewa nje kwenye vurugu
zilizotokea bungeni hivi karibuni, ndiyo maana aliamua kulipiza kisasi
kwa kutaka kumpiga ngumi na si kichwa kama anavyodai askari.
‘Sugu’ alitoa kauli hiyo wakati
akiwahutubia wakazi wa Chunya Mjini kwenye mkutano wa hadhara
ulioongozwa na Katibu Mkuu wa Chadema Taifa, Dk Willibrod Slaa ambapo
viongozi hao wapo ziarani mkoani Mbeya wakifanya mikutano na wananchi
kwa lengo la kuwaeleza ukweli wa kilichomtokea Sugu na wabunge wengine
bungeni hivi karibuni.
‘ Sugu’ alidai kuwa Ndugai ni adui wa
wapinzani bungeni na kwamba kwa vyovyote vile ilikuwa vigumu kuvumilia
kwa mtu yeyote baada ya askari kuanza kupiga wabunge kutokana na amri ya
Ndugai.
Naye Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Slaa
akizungumzia suala hilo alisema kitendo alichofanyiwa Sugu hakikuwa
kibaya kwake peke yake, bali hata wananchi waliomchagua.
Hata hivyo, Dk Slaa alisema kwa upande
mwingine ili heshima ya Bunge lolote lile duniani iwepo, ni lazima
wabunge watandikane makonde ndani ya Bunge na si vinginevyo hivyo
hashangai kwa kilichotokea kwa Sugu bungeni.
Dk Slaa, alimjia juu Ndugai akisema
alikiuka Kanuni za Bunge kwa kitendo hicho na kubainisha kwamba kanuni
za Bunge zipo wazi kabisa kwamba iwapo itatokea vurugu ndani ya Bunge
anachotakiwa kukifanya ni kuahirisha Bunge kwa wakati huo.
Pia alisema askari ambao ni wapambe wa
Bunge ‘Sargent at arms’ ndio wenye mamlaka ya kuingia ukumbini na endapo
itatokea nguvu ya ziada hao ndio wanaotakiwa kisheria na siyo kuwaita
askari wa nje ya Bunge kuingia ndani.
Dk Slaa alisema kitendo kilichofanywa na
Sugu pamoja na wabunge wengine ni cha kijasiri na aliwataka kutokurudi
nyuma na misimamo yao bali waendelee kusonga mbele.
Chanzo: Mwananchi.
No comments:
Post a Comment