Pages


Photobucket

Saturday, September 14, 2013

Hatujawarejesha wakimbizi wa Burundi kinguvu

Serikali imekanusha taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari vya nje, vikinukuu Umoja wa Mataifa (UN) kuikosoa Tanzania kwa kuwarejesha kwa nguvu wakimbizi 25,000 kutoka Burundi, mwezi mmoja uliopita. Taarifa hiyo imetajwa kutokuwa ya ukweli na yenye nia ya kuchafulia jina la nchi ambayo kwa muda mrefu, imekuwa kimbilio na makazi ya wakimbizi kutoka nchi za ukanda wa Maziwa Makuu.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isaac Nantanga, alitoa taarifa hiyo jana na kusema, hakuna mkimbizi aliyerejeshwa Burundi, kwa hiari wala kwa nguvu katika kipindi kilichotajwa. 
Alisema kipindi cha mwisho cha kuwarejesha kwao kwa hiari wakimbizi wa Burundi, ilikuwa 2012.
Alisema hadi mwezi Desemba mwaka huo, kiasi cha wakimbizi 34,000 waliohifadhiwa kwenye kambi ya wakimbizi ya Mtabila, wilayani Kasulu mkoani Kigoma, walirejeshwa kwao kwa hiari.
Alisema kazi hiyo ilitekelezwa kwa ushirikiano wa Tanzania, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) na serikali ya Burundi. 
Aidha, alisema Tanzania haina utaratibu wa kuwarejesha wakimbizi kwa nguvu na inapoonekana inafaa, zoezi la kuwarejesha linafanyika kwa hiari na ushirikiano kati ya wadau hao.
“Ukiacha wale ambao wamesharejeshwa kwao kwa hiari, wakimbizi wote ambao nchi yetu imewapatia hifadhi ya ukimbizi, wapo na wanaendelea kuishi kwenye kambi na makazi ya wakimbizi yaliyopo hapa nchini,” alisema.
Alitoa mfano kuwa, hadi sasa wapo wakimbizi wa DRC wapatao 64,172 kwenye kambi ya Nyarugusu wilayani Kasulu.
Pia wapo wakimbizi 175,473 kutoka Burundi waliopo kambi za Mishamo na Katumba wilayani Mpanda, mkoa wa Katavi na makazi ya Ulyankulu mkoani Tabora na 2,128, kutoka Somalia wapo Chogo, wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya serikali, jumla ya wakimbizi wote waliopo nchini ni 264,000.
Nantanga alisema UNHCR Dar es Salaam, imewasiliana na wawakilishi wengine wa shirika hilo waliopo Uganda, Burundi, Rwanda na DRC, na kuthibitishiwa kwamba hakuna mkimbizi aliyerudishwa siku za hivi karibuni.
“Ni dhahiri kuwa taarifa iliyotolewa kwenye Idhaa ya Kiswahili ya Radio Deustche Well sio ya kweli, na ni upotoshaji wa hali ya juu.,” alisema.
Alisema, `zoezi’ linaloendelea sasa nchini linahusiana na kuwabaini na kuwarejesha kwao wahamiaji haramu, ambao wamekuwa wakiishi nchini kinyume cha sheria. 
Alisema zoezi hilo lilianza Agosti mwaka huu ambapo wahamiaji hao walipewa muda wa wiki mbili kurejea kwao kwa hiari, ama kupata vibali halali vya kuwawezesha kuendelea kuishi hapa nchini.
Hadi Septemba 4, 2013 zaidi ya wahamiaji haramu 27,000 walikuwa wamerejea kwao kwa hiari. Wahamiaji hao haramu walikuwa katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Rukwa.
Baada ya muda waliopewa wa kuondoka au kujisajili kihalali kuisha, serikali sasa imeanza operesheni ya kuwabaini wahamiaji haramu ambao walikaidi wito wa kuwataka kuondoka kwa hiari.
Alisema operesheni hiyo inafanywa kwa uangalifu mkubwa ili kuhakikisha kuwa wanaokamatwa na kurejeshwa kwao, ni wahamiaji haramu kweli na siyo raia au wageni wenye hati halali za kuishi hapa nchini. 
SOURCE: NIPASHE

No comments:

Post a Comment