Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt.
John Pombe Magufuli (pichani) ambaye yuko katika ziara ya kikazi mkoani
Iringa ameagiza kufanyika kwa uchunguzi kuhusu utendaji wa vituo vya
mizani mkoani Iringa. Agizo hilo lilitolewa katika mkutano ambao Waziri
huyo wa Ujenzi alikutana na wafanyakazi wa taasisi zinazosimamiwa na
Wizara ya Ujenzi mkoani humo.
Wakati akisomewa taarifa za
utekelezaji wa majukumu ya kila taasisi mkoani humo ndipo lilipojitokeza
suala la tozo iliyokusanywa kwa magari yaliyokamatwa yakiwa yamezidisha
uzito kwa kipindi cha mwezi mmoja wa Julai mwaka huu wa 2013 katika
kituo cha mizani cha Wenda kilichop kati ya Iringa na Ifunda katika
barabara kuu ya TANZAM.
Meneja wa Tanroads wa mkoa wa
Iringa Injinia Poul Lyakurwa alimtaarifu Waziri Magufuli kuwa kiasi cha
Shilingi milioni 31.9 kilikusanywa katika kipindi hicho cha mwezi mmoja.
Akishitushwa na kiwango hicho
Waziri Magufuli alibainisha kuwa, kiasi hicho kilichosomwa katika
taarifa kimetokana na magari 735 yaliyokamatwa kati ya magari 20,700
yaliyopimwa sawa na asiliamia 3.5. “Takwimu hizi sizikubali kwani
wastani wa magari yanayokamatwa katika nchi nzima unakaribia asiliamia
40 iweje barabara kuu kama hii iwe na kiwango kidogo kiasi hicho cha
magari yaliyokutwa na makosa” hapa ni lazima pafanyike uchunguzi”
alisisitiza Mheshimiwa Magufuli na kueleza kuwa hali hiyo hawezi
kuiruhusu hata kidogo kuendelea.
Katika hatua nyingine Waziri
Magufuli amempongeza Meneja huyo wa Tanroads kwa kufukuza wafanyakazi 18
katika Kituo cha Mizani cha Makambako kwa kutokuwa waaminifu katika
kazi zao. Waziri huyo wa Ujenzi aliendelea kubainisha kuwa, takriban
asilimia 70 ya wafanyakazi waliokuwa katika vituo mbali mbali vya mizani
ya barabara nchi nzima wamebadilishwa baada ya kukamilika kwa zoezi la
kutangaza nafasi hizo upya.
Akisisitiza zaidi, Waziri Magufuli
alisema “Wizara ya Ujenzi itaendelea kushirikia na taasisi mbali mmbai
zikiwemo PCCB, Jeshi la Polisi, TRA na hata kwa kutumia makondakta na
wasaidizi katika magari ya usafirishaji ili kuendelea kubaini mbinu
mbali mbali ambazo zinaendelea kutumika katika suala zima la vitendo vya
rushwa katika vituo vya mizani hapa nchini”.
Kwa upande mwingine Wakala wa
Majengo Nchini pamoja na Wakala wa Ufundi na Umeme wametakiwa kuwa
wabunifu ili waweze kukabiliana kikamilifu na changamoto mbali mbali
zinazowakabili.
No comments:
Post a Comment