Pages


Photobucket

Sunday, September 22, 2013

HUYU NDIYE DAKTARI FEKI ALIYEKAMATWA MUHIMBILI

Picture


MUHIMBILI -- Dismas John Macha akiwa chini ya ulinzi baada ya kukamatwa.
Daktari anayedaiwa kuwa bandia amekamatwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili akiwa na vitambulisho bandia vya mwanafunzi wa  Chuo Kikuu cha Muhimbili cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) akisomea Shahada ya Pili.

'Daktari' huyo ambaye amekuwa akitafutwa na uongozi wa chuo kwa zaidi ya mwaka alikamatwa jana asubuhi akiwa hospitalini hapo karibu na jengo kilimo kitengo cha meno.

Katika kitambulisho chake cha kupigia kura anatambulishwa kwa jina la Dismas John Macha aliyezaliwa mwaka 1979 Kilimanjaro na anaishi maeneo ya Upanga Magharibi, Dar es Salaam.

Mwandishi wa habari hizi alimshuhudia mtuhumiwa huyo akiwa katika kituo cha usalama cha Muhas  na kupekuliwa na  
askari Polisi Anthony Mwamatepela na kukutwa akiwa na vifaa vya udaktari.

Baadhi ya vifaa alivyokutwa navyo ni pamoja na koti jeupe la udaktari na stetoskopu ambacho ni kifaa cha kusikilizia mapafu yanavyofanya kazi na mapigo ya moyo.

Pia alikuwa na begi jeusi lenye aina mbalimbali za dawa, vitambulisho na karatasi nyingi, lakini alipoulizwa alidai kuwa hizo ni  dawa zake.

Macha alikutwa pia na vitambulisho vitatu tofauti, kimoja kikimtambulisha kuwa mwanafunzi wa Muhas wa Shahada ya Pili ya Udaktari (Masters of Medicine) yenye jina la Macha Dismas kikionesha kusajiliwa kwa namba 60520/2011 na kumaliza muda wake Septemba 30 mwakani.

Kitambulisho kingine kilimtambulisha kwa jina la Macha Rogers anayesoma Shahada hiyo hiyo ikionesha kuwa anamaliza masomo yake mwakani.

Alikutwa pia na kitambulisho kinachomwonesha kuwa mwanafunzi wa Shahada ya Kwanza na kadi ya anuani yenye jina la Amos Nnko ambaye ni Ofisa Rasilimaliwatu wa Chuo hicho.

Akizungumzia alivyomkamata askari wa chuo hicho, Fulgence Semfukwe alisema walimkamata baada ya kupata taarifa za yeye kuwa maeneo hayo na kupanga mbinu za kumkamata.

Alisema saa 4.45 asubuhi  jana alimkuta kwenye jengo la meno na kumwomba kwa nafasi yake ya udaktari  amsaidie tatizo lake na hivyo waongee pembeni, naye bila wasiwasi akakubali.

Alimwuliza anatibu magonjwa gani naye kumjibu anatibu maradhi ya aina nyingi na kumwomba kitambulisho na yeye kumpa cha kwake.

Baada ya hapo alishituka na kudai kuwa ni daktari wa Mwananyamala na amekuja hapo kwa ajili ya kuona wagonjwa wake wa dharura ndipo alipokamatwa na kupelekwa kituo cha Polisi.

Alisema amekuwa akiwachanga kwa muda mrefu kutokana na kuwa kila walipopewa taarifa yuko wodi au sehemu fulani hawakumkuta kwani walipishana naye baada ya kuvua koti na kuweka kwenye begi lake jeusi.

Akizungumza na gazeti la HabariLeo, Macha limweleza mwandishi wa habari hizi kuwa yeye ni mwanafunzi ambaye anaelewa masuala yote ya matibabu, lakini alifeli chuoni hapo mwaka jana.

Alidai kuwa dawa alizokutwa nazo ni zake kwani ana matatizo katika njia ya mkojo na kifua huku akiamua kufanya hivyo kutokana na ugumu wa maisha.

"Uwezo wa kutibu ninao na nimesoma katika chuo hiki, lakini mwaka jana nilifeli ndiyo maana nikaamua kuwa hivi," alisema.
Ofisa Uhusiano wa Muhas, Hellen Mtui alisema kutokana na kukamatwa na nyaraka akijitambulisha kuwa mwanafunzi wa 'Masters of Medicine', ambaye anaweza kutibu watu hawana uhakika na idadi ya watu ambao ameshatapeli hospitalini hapo.

Kuhusu kusoma Muhimbili, Mtui alikana akisema baada ya kupekua nyaraka za chuo  hawakubaini jina la mwanafunzi wa aina hiyo na katika vyeti vyake bandia vinaonesha kusainiwa na Mkuu wa Chuo aliyekuwapo kabla chuo hakijapanda hadhi na kuwa chuo kikuu.

Mtui alisema baada ya kumkamata na kumpiga picha akiwa na mavazi ya udaktari, kumpekua  na kumhoji walimpeleka katika kituo cha Polisi cha Selander Bridge kwa mahojiano.  --- via gazeti la HABARI LEO, Jumamosi, Septemba 21, 2013
Picture
KCMC -- Alex Sumni Massawe akiwa chini ya ulinzi baada ya kukamatwa.
Taharuki na hofu imewakumba wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ya Mkoa wa Kilimanjaro, baada ya uongozi wa hospitali hiyo kumkamata daktari feki aliyekuwa na nia ya kumfanyia upasuaji wa ngozi, mmoja wa wagonjwa aliyekuwa hospitalini hapo na kutapeliwa Sh200,000

Alikamatwa katika wodi ya upasuaji akijinadi kwamba ni daktari wa watoto ametambuliwa kuwa ni Alex Sumni Massawe, ambaye alikamatwa jana asubuhi na makachero wa Polisi waliokuwa wamevalia mavazi ya kiraia baada ya uongozi wa hospitali hiyo kumuwekea mtego.

Kabla ya kukamatwa kwa Massawe, Mama mzazi wa kijana aliyetakiwa kufanyiwa upasuaji wa ngozi, Pamvelina Shirima alikutana na daktari huyo katika baa moja maarufu mjini hapa (jina limehifadhiwa) na kumtaka ampatie Sh200,000 ambazo atazitumia kuharakisha mwanae Makasi Tipesa afanyiwe vipimo .

Ofisa Uhusiano wa Hospitali hiyo,Gabriel Chisseo aliwaambia waandishi wa habari kwamba Massawe aliwekewa mtego na uongozi wa Hospitali ya KCMC kutokana na baadhi ya wagonjwa kuripoti kutapeliwa na daktari huyo feki. Alisema mama wa mgonjwa alipewa taarifa na rafiki yake kuwa anaweza kumpatia daktari atakayemsaidia kupata huduma kwa haraka,ambapo alimkutanisha na Massawe kwenye baa hiyo na kumfanyia mtoto huyo vipimo baa.

“Alex Massawe tulimkamata jana asubuhi akiwa wodi ya upasuaji baada ya kupokea kiasi cha Sh200,000 kutoka kwa Pamvelina Shirima ambaye alimleta mwanae afanyiwe upasuaji wa ngozi. Tunawataka wagonjwa wote kufuata taratibu ikiwamo kutokubali kurubuniwa na watu ambao hawajavaa sare wala vitambulisho rasmi ,” alisema Chisseo.

Kufuatia tukio hilo,Hospitali ya KCMC imethibitisha kuwa mtu huyo alikamatwa ndani ya hospitali hiyo, si mwajiriwa wao na wala hakukutwa na sare wala kitambulisho cha kitengo chake cha kazi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alisema polisi itamfikisha mahakamani wakati wowote baada ya uchunguzi wa tukio hilo kukamilika. --- via gazeti la MWANANCHI, Alhamisi,Septemba5  2013.

No comments:

Post a Comment