Pages


Photobucket

Wednesday, January 2, 2013

MBUNGE WA CCM AMPINGA JK GESI KWENDA DAR

MBUNGE wa Mtwara Mjini (CCM), Hasnain Murji na Mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Mikindani, Ali Chinkawene wamepinga kauli ya Rais Jakaya Kikwete kwamba wakazi wa Mkoa wa Mtwara hawapaswi kuzuia gesi kwenda Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi James Mbatia akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuunga mkono wakazi wa Mtwara kupinga usafirishaji wa gesi kwenda Dar es Salaam. Kulia ni Katibu wa Kampeni na Uchaguzi NCCR, Faustine Sungura. Picha na Michael Jamson

Juzi, katika salamu zake za Mwaka Mpya, Rais Kikwete alipinga madai ya wakazi wa Mikoa ya Kusini kutaka gesi hiyo isisafirishwe kwenda Dar es Salaam, akisema madai hayo hayakubaliki popote.

“Rasilimali inayopatikana popote katika nchi hii ni mali ya taifa zima na hutumika kwa manufaa ya taifa na katu si mali ya watu wa pale ilipogundulika au pale shughuli inapofanyika,” alisema Rais Kikwete.

Viongozi hao mbali na kuonyesha misimamo ya kuzuia nishati hiyo hata kabla ya kauli hiyo ya Rais Kikwete, jana walisisitiza kwa nyakati tofauti kwamba, wataendelea kuunga mkono jitihada za wananchi kupinga usafirishwaji wake kwa kuwa hiyo ni haki yao.

Murji alisema yupo tayari kuvuliwa ubunge kwa kutetea masilahi ya Wanamtwara wanaopinga gesi hiyo inayovunwa katika Kijiji cha Msimbati, mkoani Mtwara huku Chinkawene akisema msimamo wa chama chake ni kuungana na wananchi kupinga gesi kupelekwa Dar es Salaam.

Alisema Serikali inapaswa kujenga mitambo ya kuzalisha umeme mkoani Mtwara badala ya Dar es Salaam... “Tulipoona hali inakuwa tete, niliitisha kikao cha Kamati ya Siasa kujadili nini msimamo wa chama katika hili. Kamati ya Siasa wakasema hawawezi kukisemea chama kwa sababu chama ni wanachama, hivyo nikaitisha kikao cha Halmashauri Kuu ambapo pia tuliwaalika mabalozi wa mitaa.”

“Katika kikao hicho, wajumbe walipinga kwa nguvu zote suala la gesi kupelekwa Dar es Salaam. Wakaniambia niseme msimamo wao kuwa hawataki gesi iende Dar es Salaam hadi pale masilahi ya Wanamtwara yatakapowekwa wazi na Serikali.”

Mwenyekiti huyo alisema kwa maana hiyo, msimamo huo si wake binafsi, bali ni maazimio ya vikao halali vya chama hicho vinavyowakilisha wanachama na kwamba historia ya Mikoa ya Kusini jinsi ilivyonyimwa maendeleo ilitumiwa na wajumbe kujenga hoja hiyo.

“Wakati sisi hatuna umeme hakuna aliyefirikia kutuunganisha kwenye gridi ya Taifa… Barabara ya kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam miaka 51 ya Uhuru sasa, haijakamilika. Lakini bomba wanataka kujenga kwa miezi 18. Hivi kuna Watanzania muhimu zaidi ya wengine?” alihoji Chinkawene akinukuu kauli za wajumbe wa kikao hicho na kuongeza:

“Walizungumza mambo mengi, suala la kung’olewa kwa reli, kukatazwa kulima pamba, kuuawa kwa kilimo cha karanga na mkonge. Haya yote wanadai yamesababisha mkoa uendelee kuwa maskini na kwamba tumaini lao limebaki kwenye gesi. Wamesema wapo pamoja na wananchi.”

Murji kwa upande wake, alisema amekutana na umoja wa vyama vya siasa vilivyoratibu maandamano ya kupinga suala hilo na kuwapongeza kwa kazi nzuri akisema wananchi wana haki ya kutetea rasilimali yao.
Alisema yeye si mbunge anayewakilisha mawazo yake bungeni, bali ya wananchi... “Hivyo ni bora niungane na wananchi wangu kutetea masilahi yao; liwalo na liwe.”

“Nawapongeza viongozi wa vyama vya siasa kwa ujasiri na uthubutu wenu wa kutetea rasilimali hii (gesi)… Tusidharau hata kidogo malalamiko ya wananchi…” alisema Murji huku akishangiliwa na wajumbe na kuongeza:
“Nipo pamoja nanyi na hata ikibidi nivue ubunge, nipo tayari kufanya hivyo kwa masilahi ya wananchi….”

Chanzo: Mwanachi
 

No comments:

Post a Comment