Pages


Photobucket

Tuesday, January 22, 2013

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL AHUDHURIA MAZIKO YA ALIYEKUWA MAKAMU WA RAIS WA ZIMBABWE

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiweka shada la maua kwenye kaburi la Makamu wa Rais wa Zimbabwe Marehemu Dkt. Landa John Nkomo wakati wa mazishi yake yaliyofanyika jana  kwenye Makaburi ya Mashujaa jijini Harare.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal na Mkewe Mama Asha Bilal, wakiwa katika Viwanja vya Makaburi ya Mashujaa jijini Harare,  walipohudhuria maziko ya Makamu wa Rais wa Zimbabwe Marehemu Dkt. Landa John Nkomo  yaliyofanyika jana  jijini Harare Zimbwabwe.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal akizungumza jambo na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, wakati wakiwa Ikulu ya nchi hiyo jijini Harare, jana   baada ya kumaliza  mazungumzo yao.  Makamu wa Rais alimtembelea Rais Mugabe kwa lengo la  kumfariji kutokana na kifo cha Makamu wake Marehemu Dkt. Landa John Nkomo kilichotokea mwanzoni mwa wiki iliyopita.  Dkt. Nkomo   alizikwa jana kwenye Makaburi ya Mashujaa jijini Harare Zimbabwe.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal (kushoto) akizungumza na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe (kulia) alipomtembelea  Ikulu ya Harare  jana  kwa lengo la  kumfariji kutokana na kifo cha Makamu wa Rais wa nchi hiyo Marehemu  Dkt.  Landa John Nkoma, kilichotokea mwanzoni mwa wiki iliyopita na kuzikwa jana katika Makaburi ya Mashujaa jijini Harare. Katikati  ni Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe  Adadi Rajabu.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal akifurahia jambo na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, wakati akiondoka Ikulu ya nchi hiyo jijini Harare  baada ya kumaliza  mazungumzo yao. Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais
***************************
MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL AIWAKILISHA TANZANIA KATIKA MAZISHI YA MAKAMU WA RAIS WA ZIMBABWE HAYATI LANDA JOHN NKOMO
HARARE: JANUARI 21, 2012

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal ameiwakilisha Tanzania katika mazishi ya mpigania uhuru na mwanaukombozi wa Afrika Komredi Landa John Nkomo yaliyofanyika jijini Harare katika Makaburi ya Mashujaa wa Zimbabwe, jana Januari 21, 2013. Komredi Nkomo hadi anafikia mauti alikuwa Makamu wa Rais was Zimbabwe na Makamu Mwenyekiti wa Chama kilichopigania uhuru wa Zimbabwe ZANU-PF Kilicho chini ya Rais Robert Mugabe.

Makamu wa Rais Nkomo alifariki Januari 17, 2013 nchini Afrika Kusini alikopelekwa kwa matibabu baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa Kansa kwa miaka kadhaa na alifariki katika hospitali ya Mtakatifu Anne akiwa na umri wa miaka 79. Katika mazishi ya shujaa Nkomo yaliyofanyika jana na kuongozwa na Rais Mugabe pia yalihudhuriwa na Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, Zambia, Botswana na Namibia. Maelfu ya wananchi wa Zimbabwe walihudhuria mazishi hayo huku wakionekana kuguswa na msiba huo mkubwa, hali iliyowafanya kutokuondoka katika eneo la mazishi hata pale mvua ilipokuwa ikinyesha.

Rais Mugabe wakati akilihutubia taifa alisema, Hayati Nkomo alikuwa mfano thabiti wa amani katika Afrika na hata wakati anapelekwa Afrika Kusini kutibiwa kabla ya mauti kumfika, alikuwa kinara katika mazungumzo ya kufikia mkataba wa Makubaliano ya vyama vya siasa juu ya Katiba itakayotumika kwa jili ya uchaguzi mkuu ujao nchini Zimbabwe, makubaliano yaliyopitishwa mapema juma lililopita.

Akizungumza na Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Bilal Ikulu jijini Harare, Rais Mugabe aliishukuru Tanzania kwa kuwa mshirika na ndugu wa karibu katika hali zote za maisha ya wananchi wa Zimbabwe na akafafanua kuwa udugu katika nchi hizi ni wa kutukuka na unatakiwa kulindwa na kuenziwa kwa vizazi vingi vijavyo.

“Mheshimiwa Makamu, natumia nafasi hii kukuomba ufikishe salamu zangu kwa Rais Kikwete. Sisi tumefarijika sana kwa ujio wako hapa. Marehemu Nkomo alikuwa kiongozi madhubuti katika nchi yetu na sasa ametutoka. Kilichobaki kwetu ni kuendelea na kazi za kuijenga nchi yetu kwa misingi ya kuthamini amani,” alisema Rais Mugabe.

Katika ziara hiyo fupi, Mheshimiwa Makamu wa Rais licha ya kuhudhuria mazishi ya Hayati Nkomo, pia alipata fursa ya kumtembelea Rais Mugabe ofisini kwake Ikulu jijini Harare na kisha kukutana na baadhi ya Watanzania waishio Zimbabwe katika makazi ya Balozi wa Tanzania. Katika maelezo mafupi aliyoyatoa kwa wananchi wa Tanzania waishio Zimbabwe, Mheshimiwa Makamu wa Rais aliwataka kujiuliza kuhusu mambo yapi wanaona ni muhimu na bora kwa kuutangaza utanzania na Mtanzania na kuwataka kuyatumia hayo hasa sasa wakati tunapoendelea na mchakato wa mabadiliko ya Katiba ili yawe chachu ya uzalendo na taswira kwa kila mtanzania kama yalivyo mataifa mengine.

Watanzania hao pia waliitaka serikali ya awamu ya nne kuwaelimisha wananchi wa Mtwara kuhusu umuhimu wa gesi kutumika kwa maendeleo ya taifa na wakamuomba Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwaelimisha wananchi hao akifanua pia vyanzo vingine vya gesi vilivyopo nchini, hali inayoweza kuwafanya watambue kuwa gesi haiku Mtwara pekee. 

Kwa upande wa Mheshimiwa Makamu wa Rais akieleza kuhusu hoja hii alieleza kuwa, nchi iko katika kipindi cha kuandaa sera ya gesi na mafuta na sera hiyo ikikamilika wananchi watakuwa na kipindi cha kutazama kama inalenga kuwanufaisha lakini sasa hivi, wananchi wanapaswa kuwa watulivu kwa kuwa sera hiyo itazingatia maslahi ya wananchi wote wa Tanzania na maeneo yote ambapo gesi na mafuta vitapatikana.
.
Makamu wa Rais na Msafara wake wameondoka hapa leo Jumanne na kurejea nchini Tanzania tayari kuendelea na shughuli nyingine za kitaifa.

Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Januari 22, 2012

No comments:

Post a Comment