Pages


Photobucket

Tuesday, January 1, 2013

WATANZANIA SASA WAFIKIA MILIONI 44.9


Watanzania wameongezeka kwa kasi tangu mwaka 1967 ambapo walikuwa 12,313,054 na sasa wako 44,929,002.
Hatua hiyo imemshitua Rais Jakaya Kikwete ambaye amesema idadi hiyo inaweza kuwa mzigo mkubwa kwa Taifa, jamii na uchumi wa nchi katika kuwahudumia na kukidhi mahitaji yao ya msingi.
"Lazima tuwe na mipango madhubuti ya kiuchumi ili idadi hii ya watu iweze kuhudumiwa," alisema Rais Kikwete na kuongeza: "Idadi hii ni kubwa na naomba familia zingatieni uzazi wa mpango, vinginevyo hali ya maisha itashuka kwani ushindani utakuwa mkubwa wa kupata huduma wakati raslimali zilizopo ni ndogo na hazitoshelezi idadi hiyo."
Matokeo ya Sensa iliyofanyika Agosti 26 mwaka jana yanaonesha kuwa idadi ya Watanzania kwa sasa ni milioni 44.9 na ifikapo mwaka 2016 itaongezeka hadi watu milioni 51.
Matokeo ya Sensa hiyo ambayo ni ya tano kufanyika nchini, yalitangazwa jana na Rais Kikwete ambaye alionesha kushitushwa na kasi kubwa ya ongezeko la watu nchini hadi akatoa mwito kwa Watanzania kuzingatia uzazi wa mpango.
Katika takwimu hizo ambazo zinaonesha kuwa jumla ya Watanzania ni 44,929,002 kati yao idadi ya watu Tanzania Bara ni 43,629.434 na Zanzibar idadi yao ni 1,303,568.
Mwaka 1967 ambako sensa ya kwanza ilifanyika wakati Tanzania ikiwa Jamhuri ya Muungano, Watanzania walikuwa 12,313,054 kati yao Bara walikuwa 11,958,954 na Zanzibar 354,400.
Sensa ya mwaka huu ilifanyika baada ya miaka 45 ya sensa ya kwanza kufanyika na ongezeko la Watanzania kwa kipindi hicho ni watu milioni 33.


Kutokana na takwimu hizo, kasi ya ongezeko la watu kwa sasa ni asilimia 2.6 ikilinganishwa na takwimu za sensa ya mwaka 2002 ambayo ilionesha kasi ya ongezeko la watu ilikuwa ni asilimia 2.9.
Sensa hiyo ilifanyika baada ya ile ya mwaka 2002 ambayo ilionesha kuwa wakati huo Watanzania walikuwa milioni 34.4, hivyo ndani ya miaka 10 Watanzania ambao wameongezeka ni milioni 10.5.
Rais Kikwete alisema idadi hiyo kwa mtazamo wa haraka haraka na kwa ukubwa wa nchi, inaweza kuonekana kuwa ndogo, lakini akaonya kuwa uwezo wa nchi kiuchumi ndio unafanya idadi hiyo ionekane kubwa.
"Idadi ya watu ni kubwa, maana yake ni kwamba Serikali tujipange vizuri kwa ongezeko hili kubwa na tutafanya sehemu yetu, lakini jamii nayo ifahamu kuwa ushindani wa kupata huduma utakuwa mkubwa hivyo nao wazingatie uzazi wa mpango," alisema Rais Kikwete.
Matokeo yaliyotangazwa jana kwa mujibu wa Rais Kikwete ni ya awali na ifikapo Februari takwimu za kujua idadi ya wanawake na wanaume zitatolewa na Aprili takwimu za kujua rika la watu kila wilaya zitatolewa na za mwisho zitatolewa Juni 2014.
Katika matokeo hayo mengine, pia itajulikana idadi ya wazee waliopo, vijana na nguvukazi inayofanya kazi sasa. Takwimu hizo kwa mujibu wa Rais Kikwete zitatumiwa na wadau wengine kama nchi wahisani na asasi zisizo za serikali.
Rais alisema sensa italigharimu Taifa Sh bilioni 140 ambapo kwa sasa tayari Sh bilioni 124 zimetumika. "Sensa inafanywa na kila Taifa duniani kote na ni gharama kubwa kuhesabu watu."
Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Sensa ambaye pia ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema sensa hiyo imegharimiwa kwa pamoja kati ya Serikali na washirika wa maendeleo. Alisema mchango wa Serikali katika kugharimia sensa umekuwa ukiongezeka kutoka sensa moja hadi nyingine.
Alisema sensa ya mwaka huu, Serikali imechangia asilimia 90 ya gharama zote kutoka asilimia 70 kwa sensa ya mwaka 2002. Alisema sensa hiyo pia kwa kiasi kikubwa imeendeshwa na wataalamu wa ndani kuliko ilivyokuwa kwa sensa iliyopita.
"Hii inaonesha kukua kwa wataalamu wa ndani katika uendeshaji wa sensa na utafiti mwingine hapa nchini," alisema Pinda na kufafanua kuwa utekelezaji wa kuhesabu watu ulitoa ajira ya muda mfupi kwa wananchi hususan vijana ambao hawakuwa na ajira.
Alitaja idadi ya watu 150 kuwa walipata ajira ya kutenga maeneo ya kuhesabia watu ambapo makarani na wasimamizi wa sensa walikuwa 200,000 wakati wachambuzi wa takwimu walikuwa 400 walioajiriwa kwa vipindi tofauti wakati wa kutekeleza sensa. Wazabuni wa ndani wapatao 29 walitoa huduma na vifaa mbalimbali kwa ajili ya la sensa kwa Sh bilioni 11.7.
Changamoto kadhaa zilizojitokeza zilitajwa na Pinda kuwa ni pamoja na watu wanne kupoteza maisha walipokuwa wakiwajibika na kazi hiyo na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Rais Kikwete alitaja pia changamoto zingine kuwa ni watendaji wa sensa kukumbana na purukushani kutokana na kundi la watu waliotishia kuvuruga sensa na wengine kufanya kampeni ya kushawishi watu wasusie kuhesabiwa.
"Wengine katika kipindi hiki ndicho walipanga kufanya maandamano na mikutano, lakini pamoja na changamoto zote hizi, tumefanikiwa," alisema Rais Kikwete.

No comments:

Post a Comment