Pages


Photobucket

Saturday, January 12, 2013

Aomba asichaguliwe asipotimiza ahadi

 
                                MBUNGE wa Jimbo la Iringa ,Mchungaji Peter Msigwa
 
MBUNGE wa Jimbo la Iringa ,Mchungaji Peter Msigwa amewataka wakazi wa Kijiji cha Kigonzile, katika Manispaa ya Iringa kutomchagua katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ikiwa hatatimiza ahadi ya kuwapelekea maji na barabara katika kipindi hiki cha uongozi wake.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Kigonzile juzi, Msigwa alisema amepania kuwafikishia maji na barabara wakazi wa kijiji hicho ili kuwapunguzia kero ya kutafuta maji na adha ya usafiri.

“Ninajua kero ya maji na barabara ndizo zinazowatesa wakazi wa kijiji hiki hususani wakina mama, lakini niseme tu kwamba suala la maji, nimefurahi kuna mfuko mnaendelea kuuchangia deni lililobaki ninalimalizia sasa na kuhusu barabara tayari nimeshaleta greda nitahakikisha barabara hii inatengenezwa, nisipotimiza ahadi hizi msinipigie kura mwaka 2015,”alisema Msigwa.

Aliwataka wamhukumu kwa ahadi zake kwani atayafanya hayo katika kipindi cha miaka miwili.
Katika mkutano huo, Msigwa alitoa Sh1.06 milioni kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji unaotekelezwa kwa ubia na wananchi pamoja na Serikali kwa msaada kutoka Benki ya Dunia.
Katika mradi huo wananchi walitakiwa kuchanga Sh3 milioni ambapo hadi mbunge anakwenda kufanya mkutano juzi walikuwa wamechanga Sh1.04 milioni .

Mwenyekiti wa kamati ya maji wa kijiji hicho, Emsy Silla alisema fedha zilitakiwa kuchangiwa na wananchi ni Sh3 milioni ambapo zingechanganywa na michango mingine kutoka Benki ya Dunia na Serikali ya Manispaa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Katika mkutano huo wakazi wa kijiji hicho walilalamikia kukosekana kwa huduma mbalimbali za kijamii katika kijiji chao ikiwamo huduma za afya na maji safi na salama wakidai hali hiyo inahatarisha maisha yao.


Akijibu hoja hizo mbunge huyo alisema suala la kukosekana kwa huduma ni tatizo la kitaifa na kwamba limekuwa likilalamikiwa katika maeneo yote nchini lakini akasisitiza uchache wa idadi ya wabunge wa chama chake unachangia kupitishwa bajeti isiyokidhi huduma za afya.

No comments:

Post a Comment