Rais
Mpya wa Madagascar, Mhe. Henry Rajaonarimampianina akitoa hotuba yake
ya shukrani kwa nchi za Afrika kwa michango yao iliyopelekea uchaguzi wa
amani na demokrasia nchini Madagascar na pia kwa Madagascar kurejea
AU.
Waziri
Mkuu wa Ethiopia, Mhe. hailemariam Dessalegn akitoa hotuba kama
Mwenyekiti wa AU anayemaliza muda wake kabla ya kukabidhi nafasi hiyo
kwa Rais wa Mauritania, Mhe. Mohamed Ould Abdel Aziz.
Rais
wa Mauritania, Mhe. Mohamed Ould Abdel Aziz akitoa hotuba kama
Mwenyekiti Mpya wa Umoja wa Afrika kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi
Januari 2015.
Mwenyekiti
wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), Mhe. Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma
akisoma hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa
Umoja huo mjini Addis Ababa, tarehe 30 Januari, 2014. Katika hotuba yake
Dkt. Dlamini-Zuma alisisitiza umuhimu wa matumizi ya Lugha ya Kiswahili
kwani ni moja ya lugha kubwa Barani Afrika.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe
(Mb.) akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya
Mrisho Kikwete kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa
Afrika (AU) ambao umefunguliwa rasmi leo tarehe 30 Januari, 2014
mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Jopo
la Marais Wastaafu wakiwa kwenye mkutano huo. Kutoka kushoto ni Mhe.
Olusegun Obasanjo, Rais Mstaafu wa Nigeria, Mhe. Thabo Mbeki, Rais
Mstaafu wa Afrika Kusini na Mhe. Festus Mogae, Rais Mstaafu wa
Botswana.
Picha ya Pamoja ya Viongozi wa AU.
Mhe.
Membe akiongozana na Rais wa Zimbabwe, Mhe. Robert Mugabe mara baada ya
hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa AU
Mhe.
Membe akiteta jambo na Rais wa Afrika Kusini, Mhe. Jacob Zuma nje ya
Ukumbi wa Mikutano wa AU.Picha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa
---
*Kiswahili chazidi kupaa Umoja wa Afrika
Na Mwandishi wetu, Addis Ababa, 30/1/2014
Umoja
wa Afrika umeitaja Lugha ya Kiswahili kuwa ndiyo lugha kubwa na rasmi
Afrika na ndio Lugha inayofundishwa zaidi katika Vyuo Vikuu mbalimbali
duniani kutoka Afrika.
Hayo
yalisemwa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), Dkt.
Nkosazana Dlamini-Zuma wakati akifungua Mkutano wa 22 wa Wakuu wa Nchi
na Serikali wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia leo tarehe 30
Januari, 2013.
Dkt.
Zuma katika hotuba yake ya kusisimua ambayo ilielezea maendeleo
yaliyofikiwa Afrika katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, changamoto
mbalimbali zinazolikabili Bara hili na matarajio alisema kwamba katika
kipindi hiki ni muhimu kuitumia Lugha ya Kiswahili kuiunganisha Afrika.
“Wajukuu
zetu waliona ni kichekesho tulivyokuwa tukihangaika na tafsiri za
Lugha za Kiingereza, Kifaransa na Kireno wakati wa mikutano ya AU, na
vile tulivyokuwa tukizozana kwamba chapisho la Kiingereza halifanani na
lile la Kifaransa au Kiarabu, sasa tunayo Lugha yetu pamoja na hizo
lugha nyingine huo ndio ustaarabu wa sasa” alisema Dkt. Dlamini-Zuma.
Akizungumzia
maendeleo yaliyofikiwa Afrika katika kipindi cha miaka 50 iliyopita,
Mhe. Dkt. Dlamini-Zuma alisema kuwa Afrika sasa imepiga hatua kubwa
katika maendeleo ambapo kwa sasa Afrika ndio msafirishaji mkubwa wa
chakula nje na pia imekuwa kituo cha viwanda na kituo cha maarifa na
hivyo kuleta manufaa kwa maliasili zilizopo ikiwemo mazao ya kilimo kama
kichocheo cha mapinduzi ya viwanda.
“Rafiki
zangu, kwa hakika Afrika imepiga hatua kubwa katika maendeleo, kutoka
usafirishaji wa malighafi katika kipindi kilichopita na kuwa
msafirishaji mkuu wa chakula nje, hii itasaidia maliasili iliyopo Afrika
kubaki na kuwa kichocheo cha mapinduzi ya viwanda” alisema Dkt.
Dlamini-Zuma. Aidha aliongeza kuwa, Kampuni nyingi za Afrika kuanzia
zile za madini, fedha, chakula, vinywaji, utalii, madawa, uvuvi na
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ni miongoni mwa zinazoongoza duniani
katika sekta hizo.
Dkt.
Dlamini-Zuma alieleza kuwa Afrika sasa ni ya tatu duniani kiuchumi.
Hata hivyo alisisitiza bado kuna umuhimu kwa nchi za Afrika kuchangia
katika maendeleo. Vile vile, alisema kwamba njia pekee ya kuleta amani
ni kuwekeza kwa watu hususan kuwawezesha vijana na wanawake. ‘Afrika
inahitaji mapinduzi katika ujuzi kwa kubadilisha mfumo wa elimu ili
kuwaandaa vijana ambao ni wabunifu na wenye mawazo ya ujasiriamali ili
kuleta maendeleo katika Bara lao’ alisema Dkt. Zuma.
Kuhusu
hali ya amani na usalama huko, Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya
Kati, Dkt. Dlamini-Zuma alielezea kusikitishwa kwake na hali katika nchi
hizo na kusisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kufanya kazi kwa pamoja
ili kuleta amani ya kudumu katika nchi hizi.
"Tunavyouanza
mwaka 2014 mioyo yetu ipo na watu wa Sudan Kusini na wale wa Jamhuri
ya Afrika Kati hususan wanawake na watoto hivyo ni muhimu tufanye kazi
kwa pamoja ili nchi hizi zipate amani ya kudumu na kutimiza lengo letu
la kuzima kabisa mitutu ya bunduki katika Bara letu" alisisitiza Dkt.
Dlamini-Zuma.
Aidha,
alimtangaza Bibi Binta Diop kuwa Mjumbe Maalum wa Amani na Usalama
Afrika ambaye atakuwa na jukumu la kuhakikisha sauti za wanawake
zinasikika katika masuala ya kujenga amani na utatuzi wa migogoro.
Mkutano
wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika pia ulishuhudia
ubadilishanaji wa Uenyekiti wa Umoja wa Afrika kutoka kwa Waziri Mkuu wa
Ethiopia, Mhe. Hailemariam Dessalegn kwenda kwa Rais wa Mauritania,
Mhe. Mohamed Ould Abdel Aziz. Aidha, Mkutano huo ulimkaribisha Rais
mpya wa Madagascar, Mhe. Hery Rajaonarimampianina baada ya miaka minne
ya kufutwa uanachama wa AU.
Akitoa hotuba yake kabla ya kukabidhi uenyekiti, Mhe. Dessalegn alizishukuru nchi zote za Afrika kwa ushirikiano na kusisitiza umuhimu
wa kuweka vipaumbele vya maendeleo Barani Afrika katika Agenda ya
Maendeleo ya Kimataifa baada ya mwaka 2015 na ile ya Malengo ya
Maendeleo Endelevu.
Ujumbe
wa Tanzania kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa AU
uliongozwa na Mhe. Bernard K. Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa ambaye alimwakilisha Mhe. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
-Mwisho-
No comments:
Post a Comment