Wakati 
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisema wabunge wa chama chake 
watasusia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba ikiwa hoja ya kuundwa kwa 
Serikali tatu itapingwa na wabunge wa CCM, Mwakilishi wa Mji Mkongwe 
(CUF), Ismail Jussa Ladhu ametaka kuvunjwa kwa Muungano.
Akihutubia 
kwenye Uwanja wa Tubuyu nje kidogo ya Mji wa Morogoro juzi, Mbowe 
alisema wabunge wa chama chake wataandamana nchi nzima kufikisha ujumbe 
kwa wananchi kwamba maoni yao yamepingwa na wabunge wa CCM walio wengi.
“Tutawaeleza
 wananchi kwamba maoni ya CCM ndiyo yameonekana ya maana kuliko ya 
wananchi ambao ni wengi zaidi,” alisema Mbowe kwenye mkutano huo ambao 
ni sehemu ya Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko - M4C Pamoja Daima.
Alisema Tume
 ya Mabadiliko ya Katiba ilikusanya maoni na kubaini kuwa asilimia 62 ya
 Watanzania wanataka Serikali tatu za Tanganyika, Zanzibar na ya 
Muungano.
“Serikali ya
 CCM haitaki kusikia maneno Serikali tatu wanasema sera yao ni ya 
Serikali mbili, wanafanya kila hila ili kuikataa hoja hiyo. Natangaza 
kwamba wakifanya hivyo tutasusia na kwenda kuwashtaki kwa wananchi,” 
alisema Mbowe.
Aliongeza kwamba wataandamana kuanzia Kagera hadi Mtwara kuwaeleza wananchi kwamba hoja yao imepingwa na CCM.
Mbowe 
alisema baadhi ya viongozi wa CCM wamekuwa wakitoa kashfa dhidi ya 
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kwamba 
amechukua maoni ya Chadema.
“Wanakosea hayo si maoni ya Chadema, bali ni maoni ya wananchi, Warioba amezingatia maoni ya wananchi,” alisema.
Mwenyekiti 
huyo alisema Katiba inayotafutwa si ya chama, bali ni ya Watanzania na 
kwamba inashangaza CCM kuipinga hoja Serikali tatu.
“Tunafahamu 
wanaogopa kuikubali hoja ya Serikali tatu kwa sababu wanafahamu huo 
ndiyo utakuwa mwisho wao wa kuwa madarakani,” alisema Mbowe huku 
akishangiliwa na wafuasi wa chama hicho.
Alisema CCM 
wanaelewa kwamba kukiwa na Serikali tatu, Chadema kitashinda Tanganyika 
na CUF Zanzibar katika uchaguzi wowote utakaoitishwa.
“Kwa hiyo 
hivi sasa wana wasiwasi kweli, wanatafuta kila njia ya kuichakachua hoja
 ya Serikali tatu lakini wafahamu kuwa Chadema wanaifuatilia hoja hiyo 
kwa ukaribu,” alisema.
Aliwataka 
wananchi kufuatilia Bunge Maalumu la Katiba litakapoanza mwezi ujao ili 
kuangalia wabunge wao wanavyowawalisha katika suala hilo muhimu.
Hata hivyo, 
Mbowe alisema chama hicho kikishinda katika uchaguzi wa mwaka 2015 
hakitahangaika kulipa kisasi kwa kuwachukulia hatua za kisheria 
viongozi, bali kitajikita kutafuta maendeleo.
“Wasituogope
 tutasamehe kama alivyosamehe aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Nelson 
Mandela. Hatutalipa kisasi tukiingia Ikulu, kwa sababu hakuna binadamu 
asiye na makosa. Tutaelekeza nguvu zetu kuwaletea maendeleo Watanzania,”
 alisema Mbowe.
Jussa na Muungano
Akihutubia 
mkutano wa kampeni katika Jimbo la Kiembesamaki jana, Jussa alisema 
hakutakuwa na maendeleo yatakayofikiwa Zanzibar ikiwa Muungano wa 
Tanganyika na Zanzibar hautang’oka.
Jussa ambaye
 pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa la CUF, alisema Zanzibar yenye 
watu milioni 1.5 haiwezi kuwa na tatizo la watu kukosa ajira lakini sera
 na mipango ya kiuchumi imekuwa ikikwama katika utekelezaji wake 
kutokana na kukosa mamlaka kamili.
Alisema 
Zanzibar haiwezi kukopa katika taasisi za kimataifa bila ya kuwekewa 
dhamana na Waziri wa Fedha wa Muungano wakati Zanzibar ni nchi na 
kuwataka wananchi kutumia kura zao katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kuleta 
mabadiliko ya kiutawala.
“Hakuna 
sababu ya vijana Zanzibar kukosa ajira, kuna watu wasiozidi milioni 1.5,
 Muungano umefika wakati ung’oke, ndiyo kikwazo cha maendeleo ya 
Zanzibar na watu wake kiuchumi na kisiasa,” alisema Jussa.
Alisema 
mradi wowote unaobuniwa Zanzibar hauwezi kupata mfadhili bila kuwekewa 
dhamana na Serikali ya Muungano na kukwama kwa juhudi zote za kujiunga 
na jumuiya za kimataifa akitolea mfano Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu 
(OIC).
Alisema Rais
 wa Zanzibar amepoteza mambo muhimu chini ya mfumo wa Muungano ikiwa ni 
pamoja na kutopigiwa mizinga 21 akiwa nje ya nchi, kupeperusha bendera 
ya Zanzibar, kutokagua gwaride na kupigiwa wimbo wa Taifa la Zanzibar.
“Haya ya 
sasa si mamlaka kamili, wapi Dk Shein alikokwenda akapigiwa mizinga 21 
au alipeperushwa wapi bendera ya Zanzibar wakati wa safari zake za nje?”
 alihoji Jussa.
 
 



















































