Washukiwa wawili wakuu wa ghasia
za baada ya uchaguzi nchini Kenya, Uhuru Kenyatta na William Ruto
wanajadiliana kwa lengo la kuunda muungano wa kisiasa watakaotumia
kugombea uongozi wa nchi.
Taarifa za awali zilisema kuwa wawili hao tayari
wameunda muungano huo ingawa baadaye afisa wa mawasiliano wa vigogo hao
alikana kuwepo makubaliano yoyote.
Wawili hao ambao ni mahasimu wa jadi
kisiasa,wanaanda mkutano wa pamoja siku ya Jumamosi mjini Nakuru
mojawapo ya maeneo yaliyokumbwa na ghasia mbaya zaidi za kikabila baada
ya uchaguzi mkuu mwaka 2007.
Na hataua ya wawili hawa inakuja wakati mahakama
ikitarajiwa kutoa uamuzi kuhusu ikiwa wanaweza kugombea uongozi wakati
wanakbiliwa na tuhuma za kuhusikana ghasia za baada ya uchaguzi ambapo
mamia ya watu waliuawa.
Wanasema wameamua kuunda muungano watakaoutumia
kuwania nafasi ya rais na makamu wake katika uchaguzi mkuu mwaka ujao
kama ishara ya kuwapatanisha wakenya.
Wanatarajiwa kufika mbele ya mahakama ya ICC
baada ya uchaguzi mwaka ujao kujibu mashtaka ya kuhusika na ghasia
zilizotokea baada ya uchaguzi mwaka 2007-2008
Kenyatta ambaye ni naibu waziri mkuu na Ruto
ambaye ni mbunge , wanasema kuwa muungano wao utakuwa wenye kauli mbiu
ya kupigia debe umoja wa kitaifa, ustawi na kupatanisha wakenya .
Katika uchaguzi uliopita, wawili hao walikuwa
pande pinzani. Na ulikuwa uchaguzi ulioshuhudia upinzani mkali zaidi
katika historia ya Kenya.
Ulifuatiwa na ghasia za kikabila ambapo mamia ya watu waliuawa na maelfu wengine kuachwa bila makao mwaka 2007.
Wawili hao wamekanusha madai ya kuhusika na
ghasia za baada ya uchaguzi hasa kupanga makundi ya watu walioshambulia
makundi hasimu.
Na. BBCSwahili
No comments:
Post a Comment