WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na mtoto wa Rais Jakaya Kikwete,
Ridhiwan wamezungumzia tuhuma ambazo zimekuwa zikielekezwa kwao kwamba
wanamiliki rasilimali zenye thamani ya mabilioni ya shilingi.
Ridhiwan Kikwete
Lowassa kwa upande wake amekuwa akidaiwa kuwa tajiri anayemiliki kampuni
kubwa za kibiashara na kumekuwa na taarifa kwamba ana ukwasi ambao
vyanzo vyake vinatia shaka na siyo rahisi kuvitolea maelezo.
Kwa upande wake Ridhiwan naye amekuwa akidaiwa kuwa na utajiri mkubwa na
amekuwa akihusishwa na biashara za kampuni za kusafirisha mafuta ambayo
hupelekwa kwenye migodi, umiliki wa hoteli na majengo kadhaa ya
kifahari.
Wote wawili wamekuwa wakidaiwa kwamba baadhi ya mali zao wamekuwa
wakiziendesha chini ya kivuli cha wafanyabiashara wengine wakubwa nchini
ili kukwepa kuhojiwa walikotoa utajiri huo, taarifa ambazo hata hivyo
imekuwa vigumu kuzithibitisha.
Hata hivyo jana kwa nyakati na mazingira tofauti, Lowassa na Ridhiwan
walijitokeza hadharani na kukanusha madai kwamba wao ni matajiri wa
kupindukia.
Lowassa kwa upande wake akiwa mjini Mbeya alisema yeye siyo tajiri kama
ambavyo imekuwa ikidaiwa lakini wakati huohuo akasema “sijafilisika”.
“Wengi wanasema kuwa mimi ni tajiri siyo kweli, lakini sijafilisika
kutokana na kuchangia makanisa kwani nina marafiki wengi ambao
wananisaidia katika kuchangia makanisa nao pia hawajafilisika,”alisema
Lowassa.
Lowasa alitoa kauli hiyo alipokuwa akiendesha harambee ya kuchangia
ujenzi wa hosteli ya wanachuo wanawake ambao ni wanafunzi wa Chuo Kikuu
cha Theofilo Kisanji cha mkoani Mbeya, kinachomilikiwa na Kanisa la
Moraviani Tanzania, Jimbo la Kusini Magharibi.
Kiongozi huyo ambaye alichangia kaisi cha Sh25 milioni, alisema kila mtu
ana wajibu wa kuchangia elimu na kwamba mwanamke anapaswa kutazamwa kwa
karibu zaidi kwani ndiye anayebeba jukumu kubwa la kutunza familia.
Kwa upande wake Ridhiwan alisema: “Ikiwa mimi ni tajiri wa kiasi
kinachosemwa, basi mimi ninamzidi Bakhressa (Said Salim, mfanyabiashara
maarufu Afrika Mashariki), maana nimepewa kila hoteli hapa mjini,
kampuni za mafuta na kila biashara kubwa inayoanzishwa hapa mjini ni ya
Ridhiwan”.
Said Salim Bakhressa ni mfanyabiashara ambaye anatajwa kuwa tajiri
kuliko wote nchini na anashika nafasi ya pili katika nchi za Afrika
Mashariki na Kati, huku akiwa miongoni mwa wafanyabiashara 10
wanaonyemelea kuingia katika nafasi za juu za utajiri Afrika.
Hata hivyo Ridhiwan ambaye hivi karibuni alichaguliwa kuwa Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), aliongeza: “Ninaweza kuwa nafanya
biashara moja au mbili, lakini siwezi kuwa mmiliki kiasi chote hicho
cha mali.
Mtoto huyo wa Rais Kikwete alikuwa akijibu tuhuma kwamba magari yake
kumi ya kusafirisha mafuta yamekamatwa na kuzuiwa katika mpaka wa Kenya
na Tanzania, Namanga mkoani Arusha kutokana na kukwepa kodi, taarifa
ambayo aliikanusha.
No comments:
Post a Comment