MAMIA ya wakazi wa vijiji vinne katika kata ya Kalambi, wilaya
ya Muleba, mkoani Kagera, hawana mahali pa kuishi baada ya nyumba zao
kuvunjwa chini ya Operesheni Okoa Mazingira iliyosimamiwa na vyombo vya
dola likiwemo jeshi la polisi, usalama wa taifa na TAKUKURU.
Umati mkubwa wa watu, wakiwemo wanawake wajawazito na wenye watoto
wachanga, uliangua vilio kuona nyumba zake zikichomwa moto na kubomolewa
na askari hao kwa madai kuwa ni wahamiaji haramu huku wakiwa wameishi
katika vijiji hivyo kwa miaka mingi.
Vijiji vilivyokumbwa na zahama hiyo, ni vya Bitunzi, Nyabilanda,
Kasharara na Kyebitembe, ambapo sasa hawana mahali pa kuishi huku
wengine wakiweka kambi kwenye nyumba za ibada.
Wakizungumza na Tanzania Daima Jumamosi, iliyotembelea eneo la tukio
na kushuhudia uharibifu mkubwa uliofanywa katika operesheni hiyo, baadhi
ya wanawake walidai kujifungua wakiwa hawana msaada wowote wala mahali
pa kuishi na kwamba wamekuwa wakikesha na kulala chini ya miti na watoto
wao.
Aidha wananchi hao waliwashutumu baadhi ya askari polisi kwa kupora
pesa na mifugo yao kinyume cha sheria na baadhi ya wananchi waliopinga
ukandamizaji huo, walikamatwa na kubambikiwa kesi.
Walidai kuwa polisi hao wamepora sh milioni 40 wakati wa operesheni
hiyo na magunia 140 ya nafaka huku wakiwaacha wananchi hao wakiteseka
kwa njaa.
Walisema mbali ya polisi hao waliokuwa na silaha za moto na mabomu ya
machozi, pia walifyeka mazao yao na hata walipohoji walitishiwa kufungwa
jela kwa vile wamevamia na kujenga maeneo yasiyoruhusiwa kisheria.
Imedaiwa kuwa zaidi ya nyumba zao 105 zimechomwa moto na polisi hao kwa siku moja tu ya Novemba mosi mwaka huu.
Siyengo Sanane, mkazi wa maeneo hayo, alisema kuwa jitihada zao za
kuwaona viongozi wa wilaya zimekwama na wamekuwa wakitishwa ili wasidai
haki zao.
“Unajua haya maeneo yetu yanataka kumilikishwa kwa Wanyarwanda wala
siyo kweli kwamba sisi tumevamia na kujenga hapa…tumeishi hapa zaidi ya
miaka 15 iweje leo ndiyo tuonekane wavamizi?
“Sijawahi kuona serikali isiyojali watu wake..hii ni danganya
toto..sisi tuna taarifa kuwa hizi ni njama za kuwaleta wahamiaji haramu
ili tukishaondolewa hapa, wao ndio wamilikishwe maeneo yetu nasi
hatutakubali na lazima damu imwagike,” alisema.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kyebitembe, Paschal Mnyangote, alikiri
kupata fununu za kuwepo njama ya kutaifishwa kwa maeneo hayo ili
wakabidhiwe wawekezaji na kuahidi kuwaamuru wananchi hao kupambana na
wahamiaji hao na kuwataka wasikubali kuondoka kwenye maeneo hayo kwa
kuwa ni unyanyaswaji na ni kinyume cha haki za binadamu.
“Ni kweli hizi taarifa zipo na hii ni danganya toto kwamba wamevamia
hifadhi…nimewaahidi wananchi wangu iwapo serikali haitazinduka
nitawaamuru wananchi wangu wawafanye watakavyo hawa Wanyarwanda maana
sintokubali waonewe nami kama kiongozi wao ninaona,” alisema mwenyekiti.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Lembiris Kipuyo, alipohojiwa kwa njia ya
simu alikiri nyumba za wananchi hao kuchomwa na kubomolewa na kuwa
wamefanya hivyo, ili kulinda mazingira ya mkoa huo.
“Kuna operesheni okoa mazingira ya mkoa wa Kagera inaendelea kwenye
wilaya tatu za Biharamlo, Kagera na Mleba kwenye mkoa wetu, ili
kuwahamisha wahamiaji haramu wanaoingia na makundi makubwa ya ng’ombe
katika misitu ya hifadhi.
“Ni operesheni ya wazi maana inaendeshwa na polisi na inasimamiwa na
maafisa usalama wa taifa, TAKUKURU na wanasheria..hivyo wanaolalamika
hawajui kwamba kuishi kwenye ardhi kinyume cha sheria ni kosa,” alisema
Kivuyo.
No comments:
Post a Comment