Pages


Photobucket

Monday, November 12, 2012

SHIRIKA LA NDEGE LA PRECISION LAPATA NDEGE YA KISASA AINA YA ATR 42-600


 Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Precision, Alfonse Kioko (Kushoto) akipokea funguo za ndege mpya ya shirika hilo ya ATR 42-600 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ndege ya ATR Filippo Bagnato (kulia) wakati wa makabidhiano ya ndege hiyo yaliyofanyika katika kituo cha ATR jijini Toulouse, Ufaransa mwishoni mwa wiki. 
 Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ndege ya ATR Filippo Bagnato (kushoto) akimuonyesha Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Precision Alfonse Kioko (kulia) sehemu mbali mbali kwenye ndege mpya ya Kampuni hiyo aina ya ATR 42-600 wakati wa makabidhiano ya ndege hiyo yaliyofanyika katika kituo cha ATR jijini Toulouse, Ufaransa mwishoni mwa wiki.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ndege ya ATR Filippo Bagnato (kushoto) akimuonyesha Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Precision Alfonse Kioko (kulia) sehemu ya rubani kwenye ndege mpya ya Kampuni hiyo aina ya ATR 42-600 wakati wa makabidhiano ya ndege hiyo yaliyofanyika katika kituo cha ATR jijini Toulouse, Ufaransa mwishoni mwa wiki. Picha na mpiga picha wetu.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Precision, Alfonse Kioko (wa kwanza) na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuani ya Ndege ya ATR Filippo Bagnato wakishuka kwenye ndege ATR 42-600 baada ya kuifanyia ukaguzi kabla ya makabidhiano rasmi ya ndege hiyo yaliyofanyika katika kituo cha ATR jijini Toulouse, Ufaransa mwishoni mwa wiki. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Precision Air, Alfonse Kioko (kushoto) akipokea zawadi kutoka  kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ndege ya ATR Filippo Bagnato (kulia) wakati wa makabidhiano ya ndege hiyo yaliyofanyika katika kituo cha ATR jijini Toulouse, Ufaransa mwishoni mwa wiki. (Na Mpiga Picha Wetu)

Na Mwandishi Wetu, Toulouse
SHIRIKA la Ndege la Precision Air limekuwa shirika la kwanza kwenye bara ya Afrika na dunia kwa ujumla kumiliki ndege ya  kisasa aina ya ATR 42-600 baada ya kukamilisha mchakato wa kununua ndege hiyo jana , Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya  ndege ya ATR iliyopo jijini Toulouse , Ufaransa Filippo Bagnato amesema.

Ndege hiyo yenye thamani ya dola za kimarekani 16.4 milioni (Takribani shilingi bilioni 26.24) ni ndege bora katika sekta ya usafiri wa anga duniani na inazingatia usalama wa abiria kwa hali ya juu pamoja na kutoa aina mbali mbali za burudani kwa abiria wanaosafiri.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhiwa ndege hiyo kwenye kiwanda cha ndege  aina ya ATR kilichopo jijini Toulouse, Ufaransa, mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mtendaji wa Precision Air Alfonse Kioko alisema kuwa shirika lake litawekeza zaidi ya dola za kimarekani milioni 100 kuongeza uwezo pamoja na kutanua safari za shirika hilo katika kipindi cha miaka michache ijayo.

Kioko alisema kuwa ndege hiyo mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 50 iitatumika kupanua safari ya shirika hilo ya Dar es Salaam – Kilimanjaro na kuongeza kuwa safari hizo zitaanza rasmi ndani ya wiki mbili zijazo baada kuwasili kwa ndege jijini Dar es Salaam wiki hii.

“Uwekezaji wa dola milioni 100 utatuwezesha kuwa na jumla ya ndege mpya tano (nne zikiwa ni ATR 42-600 na moja ikiwa ni ATR 72-600 pamoja na  injini moja mpya  ya dharura) katika kipindi cha miaka mitatu ijayo. Ujio wa ndege hizi utaongeza idadi ya ndege zetu za ATR kufikia 14 na kutuwezesha kutoa huduma bora zenye uhakika,” alisema Kioko.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ATR Filippo Bagnato alisema kuwa Tanzania itaendelea kuwa soko muhimu la kampuni yake na kuongeza kuwa atafanya kila jitihada kuhakikisha kuwa mahusiano baina nchi hizo yanaendelea kuimarika.

 “Utoaji wa ndege ya kwanza ya ATR 42-600 kwa Shirika la Precision ni swaala la kihistoria katika bara la Afrika na duniani.  Baada ya kukabidi ndege hii Shirika la Ndege la Precision litakuwa miongoni mwa mashirika mengine yanayotoa huduma bora na zenye uhakika.

“Kwa kutumia ATR 42-600, Shirika la Precision itaendelea kujitanua kibiashara na kukumbana na changamoto zilizopo katika sekta ya usafiri wa anga Afrika na kutoa huduma zenye gharama nafuu,” alisema.

Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Ukaguzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Abubakar Kiroge wakati wa tukio hilo alisema kuwa uchunguzi katika ndege hiyo umeshakamilika na kuongeza kuwa ndege hiyo inakidhi vigezo na taratibu zote zinazotakiwa nchini Tanzania.

“Ndege hii imekidhi vigezo vya kiusalama vinavyotakiwa. Mamlaka husika sasa ipo tayari kuipatia Precision Air cheti cha kuwezesha ndege hiyo kutumika nchini Tanzania. Ukweli ni kwamba ndege hii inazingatia usalama wa abiria kwa haki ya juu,” alisema.

No comments:

Post a Comment