Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye akizungumza kwenye mkutano na
waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.Picha na Mpigapicha Wetu
SEKRETARIETI mpya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeapa kusimamia
utekelezaji wa Ilani ya chama hicho tawala kwa kufuatilia mienendo ya
watendaji wakuu wa Serikali wakiwamo mawaziri.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema jana jijini Dar
es Salaam kuwa mpango huo wenye lengo la kuongeza ufanisi wa Serikali,
utawabana pia wakuu wa mikoa, wilaya na watendaji wengine wanaosimamia
utekelezaji wa Ilani hiyo.
Alisema ikibainika mtendaji yeyote wa Serikali anabaronga katika
uwajibikaji wake, sekretarieti hiyo itamjulisha Rais Jakaya Kikwete na
kumshauri awafukuze kazi.
“Lengo ni kuhakikisha kila mmoja anawajibika kwa nafasi yake na endapo
itabainika watendaji wanaboronga, sekretarieti haitasita kumfahamisha
Rais ili awatimue ama kuwaondoa katika majukumu yao,” alisema.
Kauli ya Nape imekuja wakati kukiwa na taarifa kwamba moja ya majukumu
makubwa ya Sekretariti mpya ya CCM ni kurejea katika mwongozo wa chama
hicho wa 1982 unaoelekeza chama kuisimamia Serikali ipasavyo.
Hata hivyo, kumekuwapo na wasiwasi kwamba utekelezaji wa azma hiyo
unaweza kukwama kutokana na mawaziri na wabunge kuwa wajumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM (NEC).
Kada wa siku nyingi wa chama hicho, Steven Mashishanga mwishoni mwa wiki
iliyopita aliliambia gazeti hili kwamba, ikiwa CCM kinataka kufanikiwa
lazima kirejee kwenye mwongozo wake wa 1982 ambao unakielekeza kusimamia
Serikali.
“Hofu yangu ni moja tu kwamba, ikiwa wabunge na mawaziri ni wajumbe wa
NEC, basi hapo itakuwa vigumu kuikosoa Serikali. Mimi ninapendekeza
Serikali ibaki kuwa Serikali na chama kibaki kuwa chama,”alisema
Mashishanga na kuongeza: “Huwezi kuwa chama na hapohapo kuwa Serikali.”
Kadhalika, kauli ya Nape imekuja baada ya karibu miaka 30 ya kampeni
zilizowahi kuanzishwa na Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi
aliyetaka kila mmoja awajibike, vinginevyo atakumbwa na fagio la chuma.
Rais Mwinyi aliyekuwa madarakani tangu mwaka 1985 hadi 1995, alitoa
agizo kwamba kila Mtanzania anapaswa kuwajibika mahala pake pa kazi ili
kuleta ufanisi.
Lakini jana Nape alisema: “Tunaweka utaratibu. Tunataka watu wawajibike
katika chama na Serikali na watakaobainika kuzembea, watachukuliwa hatua
mara moja badala ya kusubiri uamuzi wa Bunge,” alisema Nape.
"Kwa sasa tumeamua kwamba hatutasubiri wabunge ndiyo wawafichue mawaziri
wanaoboronga kazi zao. Sisi (chama), tutahakikisha tunawafuatilia kwa
karibu kwani kufanya hivyo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM na kuipa
ridhaa ya kuendelea kushika dola.
"Chama kimeingia mkataba na wananchi, hatuwezi kuwaacha waendelee
kuboronga kwa sababu wakati wa uchaguzi chama ndiyo kinaumizwa,"
alisema Nape.
Ziara mikoani
Nape alieleza kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na
sekretarieti yake, wanatarajiwa kufanya ziara ya kichama mikoani
kuzungumzia masuala mbalimbali ya maendeleo.
Alisema katika ziara hizo, Kinana ambaye atakuwa akiambatana na baadhi
ya mawaziri anapanga kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya CCM tangu mwaka
2010.
“Ziara hiyo itaanza kesho mkoani Mtwara. Watazungumza na wakulima wa
korosho na bandari. Watakwenda pia Sumbawanga na Geita ambako watakutana
na wachimbaji wadogo wadogo na kumalizia mkoani Arusha,” alisema.
Elimu ya sekondari
Katika hatua nyingine, Nape alisema suala la kutaka elimu ya sekondari
itolewe bure nchini si la Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, bali
ni maazimio yaliyopitishwa kwenye Mkutano Mkuu wa chama hicho
uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma.
Juzi Lowassa alikaririwa akisema kuwa wakati umefika kwa elimu ya
sekondari nchini kutolewa bure na kumwondolea mwananchi wa kawaida mzigo
wa kubeba gharama za elimu.
Lowassa alisema mjadala kuhusu elimu kutolewa bure hadi sekondari
haukwepeki, hivyo kuwataka wadau wa elimu kuanza kujadili suala hilo na
kwamba CCM inapaswa kulifanya kuwa moja ya ajenda zake katika Uchaguzi
Mkuu wa 2015.
Nape jana alisema: "Hilo siyo wazo lake (Lowassa) binafsi. Suala hilo
lilijadiliwa kwenye mkutano huo na tulikubaliana kwamba ni vyema kufanya
hivyo ili kumshushia mwananchi gharama.”
Aliendelea: “Suala la utoaji wa elimu bure mwanzilishi wake alikuwa ni
Mwalimu Julius Nyerere, labda tatizo ni kwamba watu wengi hawajui
historia ya mambo. Elimu bure ilianzishwa tangu enzi za TANU, hadi wao
wamesoma bure.”
Nape aliendelea kueleza kuwa “Kadri Serikali inavyoongeza uwezo wake
kiuchumi, ndivyo suala hili litakavyotekelezwa ingawa tayari
tumeshashusha gharama za ada kwa shule za sekondari. Pia hii inalenga
kukuza hali ya kiwango cha elimu, ada ni ndogo sasa ukifuatilia unaweza
kulibaini hilo," alisema.
No comments:
Post a Comment