Wanajeshi wa Nigeria wanaendeleza operesheni kali ya
kuwasaka wapiganaji wa Boko Haram katika eneo la Maiduguri Kaskazini
mashariki mwa nchi hiyo.
Wanajeshi hao wanatumia magari ya kivita na wanapewa usaidizi zaidi na helicopta za kijeshi.
Jeshi la Nigeria limedai kuwa limemuua kamanda mmoja mwandamizi wa Boko Haram Ibn Saleh Ibrahim.
Raia wa eneo hilo wamesema kuwa idadi kubwa ya watu wameuawa kwenye operesheni hiyo.
Msemaji wa jeshi la Nigeria amesema Ibn Saleh
Ibrahim aliuawa wakati wa makabiliano makali ya riasi wakati alipokuwa
na walinzi wake sita.
Maafisa wa ulinzi nchini Nigeria wanaamini kuwa
Bwana Saleh, alihusika na mauaji ya Generali mstaafu Mohammed Shuwa
mwezi uliopita.
Kundi hilo la Boko Haram, ambao limeua raia wengi tangu mwaka wa 2009, halijasema lolote kuhusiana na kifo cha kamanda huyo.
Historia ya Boko Haram
Mwanzilishi wa kundi hilo, Mohammed Yusuf, aliuawa na maafisa wa ulinzi mwaka wa 2009.
Kwa sasa kundi hilo linasemekana kuongozwa na Abubakar Shekau.
Msemaji wa jeshi Luteni Kanali Sagir Musa,
ameiambia BBC kuwa Bwana Ibrahim, alikuwa mshirika wa karibu wa Bwana
Shekau na amekuwa na sifa ya nguvu na ushawishi mkubwa.
Kanali Luteni Kanali Musa ameongeza kuwa operesheni ya kuwaska wapiganaji hao katika eneo hilo la Maiduguri inaendelea.
Tayari jeshi hilo la serikali limenasa shehena kubwa ya silaha ikiwa ni pamoja na vilipuzi, alisema Luteni Kanali Musa.
Aidha amedai kuwa Bwana Ibrahim alihusika na kifo cha Generali Shuwa baada ya kupokea agizo kutoka kwa Bwana Shekau.
Gen Shuwa ni miongoni mwa watu mashuhuri ambao
jeshi la Nigeria, linawaona kuwa mashujaa wa vita, kutokana na juhudi
zake katika harakati za kumaliza vita kati ya jeshi la serikali na waasi
wa Biafra waliotaka kujetenga miaka ya sitini.
No comments:
Post a Comment