Zitto Kabwe (Mb) |
Na Zitto Kabwe
Jumanne tarehe 20 Novemba 2012, baadhi ya vyombo vya habari
vimebeba habari zinazohusu matamshi ya Waziri wa Utawala Bora ndugu George
Mkuchika kuhusu sakata ya mabilioni ya Uswisi.
Waziri amesema kwamba Serikali
ya Uswisi inataka majina ya Watanzania walioficha fedha huko ndio waweze
kusaidia uchunguzi. Habari kama Hiyo, yenye maudhui na malengo hayo hayo
iliandikwa na Gazeti la The Guardian on Sunday la tarehe 18 Novemba 2012.
Nimeona ni vema nitoe kauli yangu rasmi kuhusu suala hili. Lengo
ni kuweka rekodi sawa juu ya Azimio la Bunge na kwamba Serikali inapaswa
kutekeleza Azimio na sio kutoa kauli tata za kukata tamaa.
Moja, Suala hili japo sio jipya lakini limeandikwa kama ni jambo
jipya. Suala la Serikali ya Uswisi kutaka majina lilisemwa na Mwanasheria Mkuu
wa Serikali wakati akichangia hoja binafsi niliyowasilisha Bungeni na pia
wakati akileta maombi yake ya kuiondoa hoja ambayo yalikataliwa na Bunge. Kama
sio sababu mpya ni kwanini imeibuka upya na kwa kasi? Ni wazi Serikali
inajihami kwa kuona kuwa itashindwa kutekeleza azimio la Bunge.
Watanzania
wasikubali propaganda hii ya Serikali. Bunge limeagiza Serikali kufanya
uchunguzi kwa kutumia njia za kiserikali au wachunguzi binafsi wa kimataifa.
Kwa nini Serikali inaanza kubwabwaja ilhali wala haijaanza kazi hiyo? Serikali
inajaribu kuficha nini? Kwa nini baada ya wiki iliyopita Benki Kuu kufanya
uchunguzi kwenye Mabenki ya Biashara jijini Dar es Salaam na namna fedha
zimekuwa zikipelekwa nje (international transfers), leo Serikali inakuja na
kauli za kukakata tamaa? Kunani?
Pili, Watanzania wajue kwamba Taifa la Swiss limejengwa na
linajengwa kwa fedha hizi za wizi ambazo watu mbalimbali duniani wanaiba au
kukwepa kodi kwenye nchi zao na kuzificha huko. Serikali ya Swiss hata siku
moja haiwezi kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania katika suala kama hili.
Ndio maana Azimio la Bunge linataka wachunguzi binafsi ambao hawatahitaji
ushirikiano wa Serikali ya Swiss.
Nawakumbusha kwamba mwaka 1997 mara baada ya
Joseph Desire Mobutu kuangushwa na Rais Joseph Kabila kule Kongo - Kinshasa,
Serikali ya Swiss iliitaka Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
kuonyesha ushahidi kuwa hela hizo za Mobutu zilikuwa zimepatikana kwa njia
haramu! Waswiss walitaka Kabila awakakikishie kuwa fedha zile zaidi ya dola
bilioni nane za Kimarekani Mobutu hakuzipata kihalali ndio waweze kuzirejesha.
Zaire ilikadiriwa kuwa na zaidi ya dola za Kimarekani bilioni thelathini katika
Mabenki ya nje ya nchi hiyo. Majibu ya aina aina hii ni majibu ‘standard’
ambayo kila nchi inapewa. Hata Marekani ilipokuwa inafuatilia wakwepa kodi wao
walijibiwa hivi hivi.
Hatimaye Serikali ya Marekani ikaamua kununua taarifa
hizo na kuwakamata wakwepaji kodi wao walioficha fedha Uswisi. Hao ndio Waswiss
ambao Serikali ya Tanzania inashabikia majibu yao. Bila Aibu Mawaziri wetu
wanayanukuu majibu ya Waswiss kama kasuku. Tunasahau historia haraka sana.
Tunakuwa kama mazezeta.
Tusiwe Taifa la mazezeta. Mabwege na mazezeta huimba kila
wanachoambiwa kuimba. Sasa Serikali ya Tanzania imekuwa msemaji wa Serikali ya
Swiss badala ya kuchunguza utoroshaji wa fedha haramu na kisha kutoa taarifa
Bungeni. Naitaka Serikali ianze uchunguzi mara moja kama namna ilivyoelekezwa
na Bunge.
Suala hili sio suala la kisiasa, sasa ni Azimio la Bunge ambalo
linahitaji kutekelezwa kikamilifu. Suala hili sio suala la Zitto Kabwe tena, ni
suala la Bunge, ni suala la Wananchi. Wananchi hawataki uzezeta wa watu
waliopewa dhamana ya kutekeleza Azimio lao. Kama hawawezi wapishe watu wenye
uwezo wa kusimamia maslahi ya Watanzania kwa kuchukua hatua stahili za
kuchunguza utoroshaji mkubwa wa fedha za kigeni, ukwepaji mkubwa wa kodi na
ufisadi uliopelekea Watanzania kuficha mabilioni kwenye mabenki nje ya
Tanzania.
Hatutakaa kimya mpaka tuone mwisho kamilifu wa suala hili.
Utekelezaji wa Azimio la Bunge itakuwa ni salamu tosha mafisadi na watoroshaji
wa fedha haramu kwamba hawana pa kujificha na Tanzania sio Taifa la
kuchezeachezea. Lazima tushinde vita hii. Anayeona hawezi kutuongoza kuishinda
atupishe mapema. Hatupaswi kuwa Taifa la Mazezeta. Watanzania sio mabwege tena,
Mwakyembe alipata kusema.
Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Kigoma Kaskazini.
No comments:
Post a Comment