KINANA, NAPE WAZOMEWA SUMBAWANGA
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuwa kinafurahi
kuona kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kinatekeleza sera walizozianzisha
wao.
Wakati CHADEMA wakijivunia CCM kutumia sera zao, hali si shwari kwa
mahasimu wao hao baada ya Katibu Mkuu wake mpya, Abdullahman Kinana,
pamoja na wajumbe wenzake wa Sekretarieti kukumbana na zomeazomea mjini
Sumbawanga jana.
Kauli ya CHADEMA ilitolewa na Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa,
wakati akifungua rasmi Baraza la Mashauriano la Mkoa wa Kagera ambalo
linaundwa na viongozi kutoka katika kila jimbo la mkoa huo,
linalofanyika kwa muda wa siku tatu katika wilaya ya Karagwe.
Dk. Slaa alisema CHADEMA waliwezesha kufutwa kwa kodi za manyanyaso
katika wilaya ya Karatu baada ya kulikalia kidete suala hilo, na ndipo
CCM ilitumia sera hiyo na kuondoa kodi za namna hiyo takriban nchi
nzima.
Aliongeza kuwa walianzisha pia sera ya kujenga zahanati kila kata
wilayani Karatu, ambayo nayo CCM baadaye ilichukua na kisha kutangaza
kuanzisha utaratibu wa kujenga zahanati kila kata nchi nzima.
“Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu 2010, CHADEMA tuliahidi sera ya
kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi nchi nzima kama tungeingia
madarakani. Wakati huo CCM ilidai haiwezekani ila sasa nao wametangaza
kupunguza gharama za bidhaa hizo,” alisema.
Alifafanua ni wazi kuwa CCM ikiweza kutekeleza sera ya CHADEMA ya
kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi na kutoa elimu bure kabla ya mwaka
2015, watafurahi maana hawana wivu, lakini wakishindwa itakuwa ndiyo
njia yao ya kuondoka madarakani.
Dk. Slaa aliongeza kuwa CHADEMA haiwezi kuchukia kutokana na CCM
kutekeleza sera zake maana zinapotekelezwa wananchi wanapata mabadiliko
na unafuu wa maisha.
Alisema kuwa kelele zao zinahitaji uchumi wa nchi usimamiwe vizuri na
kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi wote, na kwamba mpaka sasa
inashangaza kuona CCM imeshindwa kupata majibu yanayosababisha wananchi
kuendelea kuwa maskini.
Dk. Slaa alichanganua kuwa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere,
aliweza kuanzisha viwanda ambavyo sasa vingi vimefungwa, bila kuchimba
dhahabu na wala kuuza samaki nje ya nchi, lakini akahoji ni kwa nini
wakati huu ambao tunauza madini, samaki nje ya nchi maendeleo yamedumaa.
“Mfano Waingereza hawana mashamba makubwa lakini hata siku moja
hawakuwahi kulia njaa. Sisi Tanzania tuna mabonde makubwa ambayo
yakitumiwa ipasavyo mawili yanaweza kutosha kulisha nchi nzima, lakini
bado tunalia njaa,” alisema.
Alibainisha kuwa kutokana na kutokuwa na mpangilio mzuri, mawazo mgando
yaliyopo hayawezi kuleta maendeleo. Alitolea mfano kuwa inashangaza
kuona bado tuna treni inayosafiri siku tatu kutoka Dar es Salaam hadi
Mwanza.
Katibu huyo aliwataka viongozi wa chama hicho kutoogopa kukemea maovu
yanayofanywa na baadhi ya viongozi walioko madarakani na kwamba kiongozi
bora lazima aonyeshe madadiliko katika eneo lake.
Alisema CHADEMA iko katika harakati za kuboresha na kuimarisha utendaji
kazi wa ndani kwa kununua pikipiki kila kata nchi nzima, kuajiri
makatibu na kutafuta ofisi za kudumu na zenye hadhi.
CCM wazomewa
Mjini Sumbawanga mambo yalikuwa magumu kwa viongozi wapya wa CCM
wakiongozwa na Katibu Mkuu wao, Kinana, baada ya kukumbana na zomeazomea
ya wananchi kwenye mkutano wake.
Kinana aliingia mjini humo jana kwa ndege akiongozana na Katibu wa
Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, Katibu wa Organizesheni Seif Khatib na
Naibu Waziri wa Tamisemi, Agrey Mwandri, na kisha kwenda eneo la Isesa
kufanya mkutano.
Kwa kuwa eneo hilo ni ngome kuu ya CHADEMA, viongozi hao walianza
kuzomewa na hivyo wakati wakiondoka wafuasi wao waling’oa bendera na
mlingoti kwenye shina la wapinzani wao na hivyo kuzidisha chuki.
Wakiwa katika mkutano wao wa ndani, uliibuka mzozo mkubwa baina ya
viongozi na waendesha bodaboda waliokuwa wamekodishwa kubeba bendera kwa
ujira wa kujaziwa mafuta na sh 10,000.
“Walitaka kuwageuka vijana wale ambao kimsngi wengi wao si wafuasi wao
kwa kuwalipa sh 2,000 badala ya 10,000 lakini baadaye walilazimika
kuwalipa kulingana na makubaliano,” kilisema chanzo chetu.
Mchana wakiwa kwenye mkutano wa hadhara eneo la Liboli, Nape aliwaudhi
baada ya kuanza kutoa matusi ya nguoni na hivyo akazomewa kwa nguvu
kiasi cha kudai wanaozomea wana mimba.
Hata Mwanri naye alipata wakati mgumu wakati akitoa ufafanuzi wake na
hata Mkuu wa Mkoa, Stella Manyanya, alipoitwa na Kinana afafanue naye
alizomewa hatua iliyomfanya Katibu huyo kutumia busara ya hali ya juu
kuwatuliza wananchi na mkutano ukamalizika.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment