SEKRETARIETI mpya ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) iliyoingia madarakani hivi karibuni chini ya uongozi wa
Rais Jakaya Kikwete, imesema itahakikisha vitendo vya rushwa hasa kwenye
chaguzi za chama hicho vinakoma mara moja, tofauti na ilivyokuwa
imezoeleka.
Kauli hiyo ya viongozi wa juu wa
CCM, Mwenyekiti Taifa (Rais Kikwete), Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara
(Phillip Mangula) na Katibu Mkuu (Abdulrahman Kinana) imetolewa jana na
viongozi hao wakati wakizungumza na wana-CCM Mkoa wa Dar es Salaam
katika mkutano wa kumpongeza Rais Kikwete kuchaguliwa kushika nafasi
hiyo tena.
Akizungumza na umati wa wanachama
hao, Rais Kikwete aliwataka viongozi wapya kufanya kazi ya ziada ya
kuhakikisha wanarejesha imani ya Watanzania kwa CCM, ambayo haiko kama
ilivyokuwa zamani. “Lazima kujiuliza nini kimekifanya chama hiki kufikia
hapo kilipo na kuangalia nini cha kufanya ili kuondokana na hali hiyo.
Pale mnapohisi hali ya kuungwa mkono inapungua lazima tujiulize,
kulikoni..! Nini cha kufanya ili kuimarisha chama,” alisema na kuongeza
kuwa kazi nyingine ni kuhakikisha wanakijenga chama na kuimarisha zaidi
ili kiendelee kuwaongoza Watanzania.
“Chama chetu hakifanyi
mikutano…wenzetu wanafanya kwanini sisi hatufanyi, sasa tutatengeneza
utaratibu maalumu kuhakikisha viongozi wa chama kwa nafasi zao wanafanya
kazi yao ipasavyo ndani na nje ya chama,” alisema Rais Kikwete. Alisema
ipo haja ya kujipanga na kuangalia namna ya kupambana na propaganda
hasi za baadhi ya vyombo vya habari na wapinzani ili kukabiliana na hali
hiyo. Aliwataka wanaCCM kuacha makundi na chuki ambayo yamekuwa
yakikigawa chama hicho.
Awali akizungumza Kinana alisema
vitendo vya rushwa ndani ya CCM watahakikisha vinakoma mara moja ili
kurejesha imani ya Watanzania iliyopungua kutokana na tuhuma za wachache
dhidi ya vitendo viovu. Alisema chini ya uongozi wake atahakikisha
mashaka yaliotawala kwa wananchi dhidi ya CCM yanaondoka kwa kuwaengua
wale wanaoendeleza vitendo vya rushwa, majumbu na vitendo vinavyo leta
sifa mbaya ya chama hicho.
“Hatuwezi kuiongoza nchi yetu
wakati watu wanamashaka na sisi, lazima tuondoe mashaka akisimama
mwana-CCM wote waseme naam huyu anaweza kusema…sio akisimama mwana-CCM
kusema watu wanahoji haaah, na huyu naye anakemea rushwa? Aliwataka
wana-CCM kushirikiana katika kukisafisha chama na si kuwaachia viongozi
jukumu hilo, ambalo wao kama viongozi wamekubali kuongoza mapambano
hayo.
No comments:
Post a Comment